Malaki 4
BHNTLK

Malaki 4

4
Siku ya Mwenyezi-Mungu inakuja
1Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema: “Tazama, siku yaja, nayo inawaka kama tanuri. Wenye kiburi na waovu wote watatupwa humo na kuteketea kama mabua makavu; watateketea kabisa pasibaki hata alama. 2Lakini kwa ajili yenu nyinyi mnaonicha, uwezo wangu wa kuokoa utawachomozea kama jua lililo na nguvu za kuponya kwenye mionzi yake.#4:2 Uwezo wangu wa kuokoa utawachomozea kama jua lililo na nguvu za kuponya kwenye mionzi yake: Maneno haya yanahusu ushindi, wokovu na kusimikwa tena uadilifu wa Mungu ambao utathibitisha ushindi wa wema na kulinda haki za wale wanaomwamini (rejea Zab 22:30-31; 40:10; Isa 45:8; 46:13; 51:7-8). Kichwa “Jua la Haki” au “Jua la Uadilifu” kilitumiwa kwa Kristo tangu zamani katika maisha ya kanisa la Kikristo (rejea Luka 1:78; 2:32). Mtatoka mkirukaruka kama ndama watokapo zizini mwao. 3Siku hiyo mtawakanyagakanyaga waovu, nao watakuwa kama majivu chini ya nyayo zenu. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
4“Kumbukeni sheria, kanuni na maagizo yangu niliyomwamuru Mose mtumishi wangu kule mlimani Horebu,#4:4 Maagizo …mlimani Horebu: Rejea Kut 19:16-20:20; 24:1-17; Kumb 5:1-3. ili awaamuru watu wote wa Israeli.
5“Tazama, kabla ya kufika siku ile kuu na ya kutisha, nitamtuma nabii Elia. 6Nabii Elia atawapatanisha wazazi na watoto wao; la sivyo, nitakuja na kuiangamiza nchi yenu.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza