Mathayo 18
BHNTLK

Mathayo 18

18
Ni nani aliye mkubwa?
(Marko 9:33-37; Luka 9:46-48)
1Wakati ule wanafunzi walimwendea Yesu, wakamwuliza, “Ni nani aliye mkubwa zaidi katika ufalme wa mbinguni?”#18:1-35 Simulizi kuu la nne la Yesu ambalo lahusu maana ya kuwa mmoja wa jamii ya wanafunzi wake (sura 18). Tazama pia utangulizi wa Injili hii. 2Yesu akamwita mtoto mmoja, akamsimamisha kati yao, 3kisha akasema, “Nawaambieni kweli, msipogeuka na kuwa kama watoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.#18:3 Mat 19:13-14; Marko 10:15; Luka 18:17. Yesu anataja watoto wadogo kama mfano kamili wa kuiga kuhusu utawala wa Mungu. Watoto wadogo ni wapole, hawana makuu na ni wenye hali thabiti ya kuwategemea wazazi wao. Mfano huo ndio unaofaa kwa wanafunzi wake. Watakaopewa fursa ya kuingia katika ufalme wa mbinguni ni wale wanaopokea zawadi za Mungu kwa furaha na kwa kumtegemea kama vile watoto wadogo. 4Yeyote anayejinyenyekesha kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkubwa katika ufalme wa mbinguni. 5Yeyote anayempokea mtoto mmoja kama huyu kwa jina langu, ananipokea mimi.
Vikwazo
(Marko 9:42-48; Luka 17:1-2)
6“Yeyote atakayemkosesha mmoja wa hawa wadogo#18:6 Hawa wadogo: Hapa Yesu anatumia maneno hayo kuwataja wanafunzi wake na pia waumini (11:25; Marko 10:14). wanaoniamini, ingekuwa afadhali afungwe shingoni jiwe kubwa la kusagia#18:6 Jiwe kubwa la kusagia: Yahusu jiwe kubwa ambalo punda alilivingirisha wakati watu waliposaga nafaka na sio jiwe linalotumiwa kusagia ambalo ni dogo. na kuzamishwa kwenye kilindi cha bahari. 7Ole wake ulimwengu#18:7 Ulimwengu: Latumika kwa maana ya jumla ya watu wote (taz pia 4:8; 5:14; 26:13) au walimwengu. kwa sababu ya vikwazo#18:7 Ole …kwa … vikwazo: Taz Luka 17:1 maelezo. Kutokana na neno hili na pia lugha kali inayotumiwa (Ole) ni dhahiri kwamba Yesu alitaka kutilia mkazo kwamba ni kosa kubwa mno kusababisha yeyote katika jumuiya yake apoteze imani yake kwake. vinavyowaangusha wengine. Vikwazo hivyo ni lazima vitokee lakini ole wake mtu yule atakayevisababisha.
8“Kama mkono au mguu wako ukikukosesha, ukate na kuutupa mbali nawe.#18:8-9 Hapa pana mtindo wa kusema ambao tunaweza kusema umetiwa chumvi; lengo lake mi kutilia mkazo kabisa umuhimu wa kuachia au kutupilia mbali kitu au vitu vyenye thamani kubwa ikiwa kuwa na vitu hivyo kutamfanya mtu atende dhambi. Uhusiano na Mungu unapaswa kudumishwa hata kama kwa kufanya hivyo itabidi mtu apate maumivu makali kama yale ya kukatwa mkono au mguu. Afadhali kwako kuingia katika uhai#18:8 Kuingia katika uhai: Sio kuzaliwa bali kushiriki wokovu, kuingia katika uhai wa milele (7:14; 19:16,29; 25:46). bila mkono au mguu, kuliko kutupwa katika moto wa milele ukiwa na mikono miwili na miguu yako miwili. 9Na jicho lako likikukosesha, ling'oe na kulitupa mbali nawe. Afadhali kwako kuingia katika uhai ukiwa chongo, kuliko kutupwa katika moto wa Jehanamu ukiwa na macho yako yote mawili.
Mfano wa kondoo aliyepotea#18:10-14 Mfano huu upo pia katika Luka (15:3-7) lakini matumizi yake huko ni tofauti kabisa na matumizi yake hapa ambapo Yesu anawahimiza wawatafute wale waliopotea miongoni mwao.
(Luka 15:3-7)
10“Jihadharini! Msimdharau mmojawapo wa wadogo hawa. Nawaambieni, malaika wao huko mbinguni#18:10 Malaika wao huko mbinguni: Malaika hapa ni wawakilishi au walinzi wa hao “wadogo”. Angalia pia Mate 12:15. wako daima mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.#18:10 Baadhi ya hati za kale zina aya ya 11: “Maana Mwana wa Mtu alikuja kuwaokoa wale waliopotea” (taz Luka 19:10). 12Mnaonaje? Mtu akiwa na kondoo 100, akimpoteza mmoja, hufanyaje? Huwaacha wale tisini na tisa mlimani, akaenda kumtafuta yule aliyepotea.#18:12 Taz Isa 40:11; Eze 34:16 na Luka 15:4-7 kuhusu mfano au picha inayotumiwa hapa kwa mchungaji. 13Akimpata, nawaambieni kweli, humfurahia huyo kuliko awafurahiavyo wale tisini na tisa ambao hawakupotea. 14Hali kadhalika, Baba yenu wa mbinguni hapendi hata mmoja wa hawa wadogo#18:14 Hawa wadogo: Tazama maelezo katika 18:6. apotee.
Kusahihishana#18:15-17 Aya hizi zinautumia ule mfano wa kondoo aliyepotea kwa kutoa mwongozo wa namna ya kumrudisha katika jumuiya mfuasi ambaye amepotea kwa kutenda dhambi.
15“Ndugu yako akikukosea,#18:15 Ndugu yako akikukosea: Hati nyingine za kale zina “akikosa” (taz Luka 17:3). mwendee ukamwonye mkiwa nyinyi peke yenu. Akikusikia utakuwa umempata ndugu yako. 16Asipokusikia, chukua mtu mmoja au wawili pamoja nawe, ili kwa mawaidha ya mashahidi wawili au watatu, kila tatizo litatuliwe.#18:16 Rejea Kumb 19:15, maneno ambayo yamekaririwa pia katika 2Kor 13:1. Taz pia 1Tim 5:19. 17Asipowasikia hao, liambie kanisa. Na kama hatalisikia kanisa,#18:17 Kanisa: Kigiriki “eklesia” yaani jumuiya ya waumini wa Kristo. Taz pia maelezo ya 16:18. Matumizi yake hapa yanahusu kanisa la mahali jumuiya hiyo ilipo na sio kanisa yaani jumuiya yote ya waumini kama katika 16:18. na awe kwako kama watu wasiomjua Mungu na watozaushuru.
Kukataza na kuruhusu
18“Nawaambieni kweli, mtakachofunga duniani kitafungwa mbinguni,#18:18 Mtakachofunga duniani kitafungwa mbinguni: Maneno aliyoambiwa Petro katika 16:19 sasa Yesu anayarudia kwa wanafunzi wote (taz pia Yoh 20:23). na mtakachofungua duniani kitafunguliwa mbinguni. 19Tena nawaambieni, wawili miongoni mwenu wakikubaliana hapa duniani kuhusu jambo lolote la kuomba, Baba yangu wa mbinguni atawafanyia jambo hilo. 20Kwa maana popote pale wanapokusanyika wawili au watatu kwa jina langu, mimi nipo hapo#18:20 Wanapokusanyika wawili au watatu kwa jina langu, mimi nipo hapo: Kuweko kwa Bwana Yesu katika jumuiya yake ndiko kunakosababisha maombi yao na maamuzi yao yafanikishwe na Mungu. kati yao.”
Mfano wa mtumishi asiyesamehe
21Kisha Petro akamwendea Yesu, akamwuliza, “Je, ndugu yangu akinikosea, nimsamehe mara ngapi? Mara saba?” 22Yesu akamjibu, “Sisemi mara saba tu, bali sabini mara saba.#18:22 Sabini mara saba: Au “mara sabini na saba”. Tarakimu saba inatumika mara nyingi kama picha ya ukamilifu na msemo huo una shabaha ya kuonesha kwamba kuhusu jambo la kusamehe hakuna mpaka au kikomo. Rejea Luka 17:3-4. 23Ndiyo maana ufalme wa mbinguni unafanana na mfalme mmoja aliyeamua kukagua hesabu za watumishi wake.#18:23-35 Mfano huu unandeleza wazo la msamaha lililotajwa katika 18:21-22. 24Ukaguzi ulipoanza, akaletewa mtu mmoja aliyekuwa na deni la fedha talanta 10,000.#18:24 Talanta elfu kumi: Ni fedha nyingi. Talanta moja ilikuwa kiasi cha fedha aliyolipwa kibarua kama angefanya kazi kwa mwaka mmoja; kwa hiyo ni kiasi kikubwa sana wakati huo. 25Mtu huyo hakuwa na chochote cha kulipa; hivyo bwana wake aliamuru auzwe, yeye, mke wake, watoto wake na vitu vyote alivyokuwa navyo, ili deni lilipwe. 26Basi, huyo mtumishi akapiga magoti mbele yake, akasema, ‘Unisubiri nami nitakulipa deni lote’. 27Yule bwana alimwonea huruma, akamsamehe lile deni, akamwacha aende zake.
28“Lakini huyo mtumishi akaondoka, akamkuta mmoja wa watumishi wenzake aliyekuwa na deni lake fedha dinari 100.#18:28 Denari mia moja: Denari moja wakati huo ilikuwa kiasi cha fedha aliyolipwa kibarua kwa kutwa. Ndiyo kusema, ikilinganishwa na kiasi kile cha kwanza (aya 24), kiasi hiki ni kidogo sana na hivyo ndivyo mwandishi anavyoonesha uovu wa huyo mtumishi. Akamkamata, akamkaba koo akisema, ‘Lipa deni lako!’ 29Huyo mtumishi mwenzake akapiga magoti, akamwomba, ‘Unisubiri nami nitakulipa’. 30Lakini yeye hakutaka, bali alimtia gerezani mpaka hapo atakapolipa lile deni.
31“Basi, watumishi wenzake walipoona jambo hilo walisikitika sana, wakaenda kumpasha habari bwana wao juu ya mambo hayo yaliyotukia. 32Hapo yule bwana alimwita huyo mtumishi, akamwambia, ‘Wewe ni mtumishi mbaya sana! Uliniomba, nami nikakusamehe deni lako lote. 33Je, haikukupasa nawe kumhurumia mtumishi mwenzako kama nilivyokuhurumia?’
34“Basi, huyo bwana alikasirika sana, akamtoa huyo mtumishi aadhibiwe mpaka hapo atakapolipa deni lote. 35Na baba yangu aliye mbinguni atawafanyieni vivyo hivyo kama kila mmoja wenu hatamsamehe ndugu yake kwa moyo wake wote.”#18:35 Kama …hatamsamehe ndugu yake kwa moyo wake wote: Msamaha kutoka kwa Mungu unapatikana tu ikiwa nasi tunawasamehe wengine (6:12, 14-15).

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza