2
Wageni kutoka mashariki#2:1-12 Wageni kutoka mashariki: Habari hii ya wataalamu wa elimu ya nyota kumtembelea Yesu ni ya Mathayo peke yake nayo ina shabaha ya kutilia mkazo kwamba kuzaliwa kwa Yesu kunauthiri ulimwengu wote. Habari yenyewe haisemi hao walikuwa wangapi, walakini kutokana na zawadi zao tatu pengine walikuwa watatu.
1Yesu alizaliwa mjini Bethlehemu,#2:1 Bethlehemu: Huu ni mji ulio yapata kilomita 8 kusini mwa Yerusalemu; ulikuwa mji wa kuzaliwa wa mfalme Daudi (1Sam 16:1). Rejea Luka 2:4-7. Wayahudi walitazamia kwamba Mwokozi angezaliwa huko. mkoani Yudea, wakati Herode#2:1 Herode: Anaitwa pia Herode Mkuu. Utawala wa Roma ulimteua kuwa mfalme mwaka wa 40 K.K. lakini alitawala tangu mwaka 37 K.K. mpaka mwaka wa 4 B.K. Alikuwa baba yake Arkelao (taz Mat 2:22), Herode Antipa (taz Mat 14:1) na Filipo (rejea Luka 3:1). alipokuwa mfalme. Punde tu baada ya kuzaliwa kwake, wataalamu wa nyota#2:1 Wataalamu wa nyota: Kigiriki ni “magoi”. Tafsiri nyingine yamkini “wanajimu”. Ni vigumu kusema hao walitoka wapi hasa, ila Inaonekana hawakuwa Wayahudi. Hao wanawawakilisha kwa kutangulia watu wasio Wayahudi ambao watamtambua Yesu kuwa Kristo Mwokozi. kutoka mashariki walifika Yerusalemu, 2wakauliza, “Yuko wapi mtoto, Mfalme wa Wayahudi, aliyezaliwa? Tumeiona nyota yake#2:2 Nyota yake: Katika Hes 24:17 tuna “Nyota itatokea kwa wazawa wa Yakobo”. Kuonekana kwa nyota hiyo kulikuwa kama tangazo kwa hao wataalamu wa nyota kwamba amezaliwa Mwokozi, mfalme wa Wayahudi. ilipotokea mashariki, tukaja kumwabudu.”
3Mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, yeye pamoja na wakazi wote wa Yerusalemu. 4Basi, akawaita pamoja makuhani wakuu#2:4 Makuhani wakuu: Hawa walikuwa makasisi waliokuwa na jukumu la kusimamia mambo yote ya ibada hekaluni Yerusalemu. Waalimu wa Sheria walikuwa nao wataalamu wa mafundisho na maagizo ya sheria za Agano la Kale. wote na waalimu wa sheria, akawauliza, “Kristo atazaliwa wapi?” 5Nao wakamjibu, “Mjini Bethlehemu, mkoani Yudea. Ndivyo nabii alivyoandika:
6‘Ee Bethlehemu nchini Yudea,
wewe si mdogo kamwe kati ya miji maarufu ya Yudea;
maana kwako atatokea kiongozi
atakayewaongoza#2:6 Atakayewaongoza: Au: “atakayewachunga”. Mfano wa mchungaji anayewaongoza au kuchunga mifugo yake ulitolewa katika maisha ya kawaida ya vijijini na kutumiwa tangu nyakati za kale kama mfano. Taz Yoh 10:11. watu wangu, Israeli.’”#2:6 Maneno hayo yamedondolewa kutoka Mika 5:1.
7Hapo, Herode aliwaita faraghani hao wataalamu wa nyota, akawauliza wakati hasa ile nyota ilipowatokea. 8Kisha akawatuma Bethlehemu akisema, “Nendeni mkachunguze kwa makini habari za mtoto huyo. Mkisha mpata nileteeni habari ili nami niende kumwabudu.”
9Baada ya kumsikiliza mfalme, hao wataalamu wa nyota wakaenda. Kumbe ile nyota waliyokuwa wameiona upande wa mashariki iliwatangulia hata ikaenda kusimama juu ya mahali pale alipokuwa mtoto. 10Walipoiona hiyo nyota, walifurahi mno. 11Basi, wakaingia nyumbani, wakamwona yule mtoto pamoja na Maria mama yake; wakapiga magoti, wakamsujudia. Kisha wakafungua hazina zao, wakampa zawadi: dhahabu, ubani#2:11 Ubani: Au “uvumba”. Huo ulitumika katika kutambikia. Yafaa kukumbuka hapa kwamba zawadi hizo zilifaa kwa mfalme na siyo kwa mtu wa kawaida. na manemane.#2:11 Wakampa Zawadi: …Manemane: Haya yalitengenezwa kutoka utomvu wa mti fulani, nayo yalitumika kama marashi na mara nyingine tunaambiwa kwamba yalichanganywa katika divai na kupewa mtu ili kumpunguzia maumivu. Aghalabu yalitumika kupaka maiti.
12Mungu aliwaonya katika ndoto wasimrudie Herode; hivyo wakarudi makwao kwa njia nyingine.
Kukimbilia Misri
13Baada ya wale wageni kuondoka, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto, akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapokuambia, maana Herode anakusudia kumuua huyu mtoto.”
14Hivyo, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akaondoka usiku, akaenda Misri. 15Akakaa huko mpaka Herode alipokufa. Jambo hilo lilifanyika ili neno alilosema Bwana kwa njia ya nabii litimie:
“Nilimwita Mwanangu kutoka Misri.”#2:15 Nilimwita Mwanangu kutoka Misri: Taz Hos 11:1; ling Kut 4:22-23; Kumb 1:31. Katika Agano la Kale msemo huu ulitumika kuhusu ahadi ya Mungu ya kuwaokoa watu wake, Waisraeli, utumwani Misri. Maneno hayo sasa yanamhusu Yesu Kristo na yanaonesha kwamba Mwana wa Mungu kweli ndiye Yesu Kristo, na kwamba yaliyotukia kwa Waisraeli yalikuwa mfano wa yale yatakayotukia kuhusu Mwana halisi wa Mungu, Yesu Kristo.
Watoto wachanga wanauawa
16Herode alipogundua kwamba wale wataalamu wa nyota walikuwa wamemhadaa, alikasirika sana. Akaamuru watoto wote wa kiume mjini Bethlehemu na kandokando yake wenye umri wa miaka miwili na chini yake wauawe. Alifanya hivyo kufuatana na muda aliopata kujua kutoka kwa wale wataalamu wa nyota. 17Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyosemwa kwa njia ya nabii Yeremia:
18“Sauti imesikika huko Rama,
kilio na maombolezo mengi.
Raheli anawalilia watoto wake,
wala hataki kutulizwa,
maana wote wamefariki.”#2:18 Wamefariki: Taz Yer 31:15. Rama ni mahali ambapo alizikwa Raheli, mkewe Yakobo (1Sam 10:2), kilomita 8 kaskazini ya Yerusalemu.
Kutoka Misri
19Baada ya kifo cha Herode, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto kule Misri, 20akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, urudi tena katika nchi ya Israeli, maana wale waliotaka kumuua mtoto huyo wamekwisha kufa.” 21Basi, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akarejea nchini Israeli.
22Lakini Yosefu aliposikia kwamba Arkelao,#2:22 Arkelao: Huyu alikuwa mwanawe Herode Mkubwa. Alitawala tangu mwaka wa 4 K.K. hadi mwaka 6 B.K. kule Yudea, Samaria na Idumea. Alitawala mahali pa baba yake yaani Herode ambaye alikufa mnamo mwaka wa 4 K.K. Kwa vile Arkelao hakuwa na madaraka juu ya eneo la Galilaya Yosefu, Maria na mwanawe wangeweza kukaa huko kwa usalama. mwanawe Herode, alikuwa mfalme wa Yudea mahali pa baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye, baada ya kuonywa katika ndoto, alikwenda pande za Galilaya, 23akahamia katika mji uitwao Nazareti. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyonenwa kwa njia ya manabii:
“Ataitwa Mnazare.”#2:23 Mnazare: Maana yake ni “mkazi wa Nazareti”. Wakati huo eneo la Nazareti katika milima ya Galilaya lilikuwa la watu wasio maarufu (rejea Luka 2:39-59; Yoh 1:45). Jina hili lilitumika kumtambulisha Yesu (ling Mat 21:11) na kutokana na Mate 24:5 wafuasi wa Yesu, yaani Wakristo wa kwanza, walitambuliwa vivyo hivyo. Yesu anaitwa hivyo kwa maana ya kwamba yeye ndiye kweli aliyewekwa wakfu awaokoe watu wake (taz matumizi ya neno la Kiebrania “nazir” katika simulizi la Samsoni, Amu 13:5,7).