Mika 1
BHNTLK

Mika 1

1
1Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Mika, mwenyeji wa Moreshethi,#1:1 Moreshethi: Mahali yapata kilomita 40 kusini-mashariki ya Yerusalemu, ambapo panajulikana pia kwa jina Moresheth-gathi (aya 4). wakati Yothamu, Ahazi na Hezekia#1:1 Yothamu, Ahazi na Hezekia: Yothamu mwaka 740-736 K.K. (2Fal 15:32-38); Ahazi mwaka 736-716 K.K. (2Fal 16:1-20); Hezekia mwaka 716-687 K.K. (2Fal 18:1—20:21). walipokuwa wafalme wa Yuda. Mika aliona mambo yote haya kuhusu Samaria na Yerusalemu.
Mwenyezi-Mungu aja kuhukumu
2Sikilizeni enyi watu wote;
sikiliza ewe dunia na vyote vilivyomo.
Mwenyezi-Mungu anakuja kuwashtaki,#1:2 Mwenyezi-Mungu …kuwashtaki: Hukumu ya Mungu dhidi ya Waisraeli na mataifa mengine mara nyingine inaelezwa na manabii kama kesi (Kumb 30:19; Yer 2:9,35; Mika 6:1-2). Mungu, hakimu, anasema ulimwengu wote utateseka kwa sababu watu wameabudu miungu (1:5-7).
Bwana anena kutoka hekalu lake takatifu.#1:2-3 Hekalu lake takatifu …makao yake: Dokezo kwa mbinguni kama makazi ya Mwenyezi-Mungu (Zab 11:4; Isa 63:15; Hab 2:20). Rejea Amo 4:13.
3Naam! Mwenyezi-Mungu yuaja kutoka makao yake;
atashuka na kutembea juu ya vilele vya dunia.
4Milima itayeyuka chini ya nyayo zake,
kama nta karibu na moto;
mabonde#1:4 Milima …mabonde: Kuweko kwake Mwenyezi-Mungu kunasababisha vitendo katika maumbile, katika nchi na majini (Kut 19:18; Amu 5:4-5; Zab 18:6-15). yatapasuka,
kama maji yaporomokayo kwenye mteremko.
5Haya yote yatatukia
kwa sababu ya makosa ya wazawa wa Yakobo,
kwa sababu ya dhambi za wazawa wa Israeli.
Je, uhalifu wa Yakobo waonekana wapi?
Katika mji wake mkuu Samaria!
Je, uhalifu wa Yuda waonekana wapi?
Katika Yerusalemu kwenyewe!
6Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Mji wa Samaria nitaufanya magofu nyikani,
shamba ambalo watu watapanda mizabibu.
Mawe yaliyoujenga nitayatupa bondeni,
na misingi yake nitaichimbuachimbua.
7Sanamu zake zote zitavunjwavunjwa,
kila kilichochumwa kitateketezwa kwa moto.
Vinyago vyake vyote nitaviharibu.
Vilirundikwa kutokana na ujira wa malaya,
navyo vitatumiwa tena kulipia umalaya.”#1:7 Sanamu zake …vinyago vyake … vitatumiwa tena kulipia umalaya: Katika mahali pengi pa kuabudia miungu ya uongo watu walijamiiana na malaya kama njia moja ya kuiabudu miungu hiyo na fedha zilizopatikana kwa njia hiyo kutumiwa kuendeleza ibada za miungu. Kuabudu miungu ya Kanaani, ya kiume na ya kike, ilikuwa tatizo kubwa katika Israeli (Hos 4:9-19).
Nabii anaomboleza juu ya Yerusalemu na Yuda#1:8-16 Katika maombolezo haya miji kadha wa kadha iliyokuwa kusini-mashariki ya Yerusalemu iliharibiwa kwa vita. Maneno ya Kiebrania yanayotumiwa kwa miji hiyo mara nyingine yana vigezo vya sauti inayofanana na majini ya miji hiyo ambayo makala ya maneno yanayosemwa yana sauti ya pekee ambayo haiwezi kutolewa katika tafsiri za lugha nyingine. Mtindo huo wa kishairi unatumika pia katika Isa 10:28-30.
8Kwa sababu hiyo, mimi nitalia na kuomboleza;
nitatembea uchi na bila viatu.
Nitaomboleza na kulia kama mbweha,
nitasikitika na kulia kama mbuni.
9Majeraha ya Samaria hayaponyeki,
nayo yameipata pia Yuda;
yamefikia lango la Yerusalemu,
mahali wanapokaa watu wangu.
10Msiitangaze habari hii huko Gathi,
wala msilie machozi!
Huko Beth-leafra#1:10-12 Gathi …Beth-leafra: Gathi ulikuwa mji wa Wafilisti; Beth-leafra haujulikani, ila maana yake katika Kiebrania ni kama “Mji wa vumbi”. Shafiri, Zaanani na Marothi inatajwa tu hapa katika A.K. Vile vile mji Beth-ezeli nao unafikiriwa kuwa karibu na Gathi. mgaegae mavumbini kwa huzuni.
11Nendeni enyi wakazi wa Shafiri,
mkiwa uchi na wenye haya.
Wakazi wa Zaanani msitoke nje ya mji wenu.
Watu wa Beth-ezeli wanalia;
msaada wao kwenu umeondolewa.
12Wakazi wa Marothi wanangojea msaada kwa hamu kubwa,
lakini maangamizi yaja kutoka kwa Mwenyezi-Mungu
karibu kabisa na lango la Yerusalemu.
13Enyi wakazi wa Lakishi,
fungeni farasi wepesi na magari ya vita.
Nyinyi mlikuwa mmeiga dhambi ya watu wa Siyoni,
makosa ya Waisraeli yalikuwa kwenu.#1:13 Huu ulikuwa mji wenye ngome na huenda Mika alikosea tegemeo la wakazi wake kwa farasi wao na magari ya kukokotwa ya vita.
14Hivyo, mnapaswa kuagana na kuwaacha wakazi wa Morasheth-gathi.#1:14 Morasheth-gathi: Jina lingine la Moreshethi (1:1).
Nao mji wa Akzibu hautawasaidia wafalme wa Israeli,
15Enyi wakazi wa Maresha,
Mungu atawaleteeni tena adui atakayewateka.
Viongozi waheshimiwa wa Israeli
watakimbilia pangoni huko Adulamu.#1:15 Adulamu: Mahali ambapo Daudi alijificha mbali na Sauli (1Sam 22:1-2).
16Enyi watu wa Yuda, nyoeni upara
kuwaombolezea watoto wenu wapenzi;
panueni upara wenu uwe mpana kama wa tai,
maana watoto wenu watawaacha kwenda uhamishoni.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza