Mika 2
BHNTLK

Mika 2

2
Mika na wapinzani wake
1Ole wao wanaopanga kutenda maovu
wanaolala usiku wakiazimia uovu!
Mara tu kunapopambazuka,
wanayatekeleza kwani wanao uwezo.
2Hutamani mashamba na kuyatwaa;
wakitaka nyumba, wananyakua.
Huwadhulumu wenye nyumba na jamaa zao,
huwanyang'anya watu mali zao.#2:2 Hutamani …kuyatwaa … huwanyang'anya watu mali zao: Ardhi ilichukuliwa katika Israeli kuwa urithi kutoka kwa wazee na haikuruhusiwa kuiachia (rejea 1Fal 21:1-40) ila kukabidhiwa watoto waliofuata (rejea Lawi 25:23-28). Wenye mali na viongozi waliwatendea watu wa kawaida na maskini vibaya sana kuhusu hilo na manabii wengi walipinga ukatili huo (Isa 5:8-10; Hos 5:10; Amo 2:6-8; 4:1; 5:10-13; Sef 1:9).
3Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Ninapanga kuwaleteeni nyinyi maafa,
ambayo kamwe hamtaweza kuyakwepa.
Utakuwa wakati mbaya kwenu,
wala hamtaweza kwenda kwa maringo.
4Siku hiyo watu watawasimanga kwa wimbo,
watalia na kuomboleza kwa uchungu, wakisema:
‘Tumeangamia kabisa;
Mwenyezi-Mungu amechukua nchi yetu,
naam, ameiondoa mikononi mwetu.
Mashamba yetu amewagawia waliotuteka.’”#2:4 Waliotuteka: Makala ya Kiebrania: “waasi”.
5Kwa hiyo hamtagawiwa sehemu yoyote ya ardhi
miongoni mwa watu wake Mwenyezi-Mungu.
Wapinzani wa nabii
6“Usituhubirie sisi.
Mambo kama hayo si ya kuhubiriwa.
Sisi hatutakumbwa na maafa!#2:6 Isa 30:10. Mika aliendelea kuwahubiria watu ingawa ujumbe wake ulikuwa mchungu kwa wale waliowakandamiza wanyonge.
7Je, yafaa kusema hivyo, wazawa wa Yakobo?
Je, Mwenyezi-Mungu ameacha uvumilivu wake?
Je, yeye hufanya mambo kama haya?”#2:7 Si dhahiri ni nani anayeongea hapa; labda ni maadui wa Mika ambao wanawakabili wale ambao wanamuunga mkono. Katika 2:8 ni wazi Mika anasema tena ujumbe wa Mwenyezi-Mungu.
Mika
Sivyo! Maneno yangu huwafaa watendao mambo mema.
8Lakini Mwenyezi-Mungu awaambia hivi:
“Nyinyi mnawavamia watu wangu kama adui.
Mnawanyang'anya mavazi yao watu watulivu;
watu wanaopita kwenda zao bila wasiwasi,
na wasio na fikira zozote za vita.
9Mnawafukuza wake za watu wangu
kutoka nyumba zao nzuri;
watoto wao mmewaondolea fahari yangu milele.
10Inukeni mwende zenu!
Hapa hamna tena pa kupumzika!
Kwa utovu wenu wa uaminifu
maangamizi makubwa yanawangojea!
11Kama mtu angetokea akatamka maneno matupu ya uongo
na kusema: ‘Nawatabirieni divai na pombe kwa wingi’,
mhubiri wa namna hiyo angependwa na watu hawa!#2:11 Mika anaeleza kwa kebehi nabii ambaye anahubiri ili kuwavuta na kuwapendekeza watu. Rejea Mika 3:5.
12“Lakini kweli nitawakusanya nyote enyi watu wa Yakobo,
naam, nitawakusanya enyi Waisraeli mliobaki,
niwalete pamoja kama kondoo katika zizi,
kama kundi kubwa la kondoo malishoni;
nanyi mtakuwa kundi la watu wengi.”#2:12 Mika anaongeza hapa maneno yenye matumaini ya kurekebishwa kwa Waisraeli “watakaosalia” katika siku ngumu za usoni. Tofauti na viongozi wao ambao walitumia vibaya madaraka yao na kuwanyima haki, Mungu atakuwa mchungaji mwema kwa wale watakaorejea Yuda. Viongozi safi walioteuliwa na Mungu walipaswa kuwa wachungaji wema wenye kutafuta maslahi ya watu wao (Yer 23:4-6; Eze 34:2-10). Taz pia Zab 23; Yoh 10:14.
13Yule atakayetoboa njia atawatangulia,
nao watalivunja lango la mji na kutoka nje,
watapita na kutoka nje.
Mfalme wao atawatangulia;
Mwenyezi-Mungu mwenyewe atawatangulia.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza