4
Mungu atatawala watu wote kwa amani
(Isa 2:1-4)
1Utakuja wakati#4:1 Utakuja wakati: Nabii anaeleza juu ya wakati ujao ambapo watu wa Yuda watarudi makwao na kujenga upya mji wa Yerusalemu na hekalu lake (2Nya 36:22-23). ambapo
mlima wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu#4:1 Mlima wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu: Yaani, Mlima siyoni.
utakuwa mkubwa kuliko milima yote.
Naam, utakwezwa juu ya vilima vyote.
Watu wengi watamiminika huko,#4:1—5:14 Mika anaahidi kwamba katika siku za usoni, watu wa mataifa yote watamwabudu Mwenyezi-Mungu huko Yerusalemu. Watu watakapoishi kulingana na sheria ya Mungu kutakuwa na amani. Watu wa Mungu watarudi Yuda na kujenga upya mji wa Yerusalemu baada ya kupata adhabu. Mungu atateua mtawala wa kuwatawala na kuleta amani. Adui watashindwa na vinyago vya miungu vitaangamizwa.
2mataifa mengi yataujia na kusema:
“Twendeni juu kwenye mlima wa Mwenyezi-Mungu,
twende katika nyumba ya Mungu wa Yakobo,
ili atufundishe njia zake,
nasi tufuate nyayo zake.
Maana mwongozo utatoka huko Siyoni;
neno la Mwenyezi-Mungu huko Yerusalemu.”
3Mungu atasuluhisha mizozo ya mataifa mengi,#4:3 Atasuluhisha mizozo ya mataifa mengi: Isa 2:4; Yoe 3:10.
atakata mashauri ya mataifa makubwa ya mbali.
Nayo yatafua mapanga yao kuwa majembe,
na mikuki yao kuwa miundu ya kupogolea.
Taifa halitapigana na taifa lingine,
wala hayatafanya tena mazoezi ya vita.
4Kila mtu atakaa kwa amani
chini ya mitini na mizabibu yake,
bila kutishwa na mtu yeyote.
Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ametamka yeye mwenyewe.
5Mataifa mengine hufuata njia zao,
kwa kuitegemea miungu yao,
lakini sisi twafuata njia zetu kwa kumtegemea Mwenyezi-Mungu,
Mungu wetu, milele na milele.#4:5 Mataifa mengine …lakini sisi … kwa kumtegemea … Mungu wetu, milele na milele: Isa 2:5.
Waisraeli watarudi kutoka utumwani
6Mwenyezi-Mungu asema,
“Siku ile#4:6 Siku ile: Taz Isa 13:6; Rejea pia Eze 13:5; Yoe 1:15; 2:1,11; Amo 5:18; Oba aya 15; Sef 1:7,14; Mal 4:1-6. nitawakusanya walemavu,
naam, nitawakusanya waliochukuliwa uhamishoni,
watu wale ambao niliwaadhibu.#4:6-7 Wazo la kuwakusanya pamoja watu waliotawanywa ni mfano unaotajwa mara kwa mara katika Biblia. Rejea Isa 40:11; 56:8; Yer 23:3; 29:14; 31:8-10; Eze 11:17; 34:11-16; Mika 2:12-13; Sef 3:18-19; Zek 10:8; Yoh 10:7-16.
7Hao walemavu ndio watakaobaki hai;
hao waliochukuliwa uhamishoni watakuwa taifa lenye nguvu.
Nami Mwenyezi-Mungu nitawatawala mlimani Siyoni,
tangu wakati huo na hata milele.”
8Nawe kilima cha Yerusalemu,
wewe ngome ya Siyoni,
ambamo Mungu anafanya ulinzi juu ya watu wake,
kama mchungaji juu ya kondoo wake;
wewe utakuwa tena mji maarufu kama hapo awali,
Yerusalemu utakuwa tena mji mkuu wa mfalme.#4:8 Tafsiri ya makala ngumu ya Kiebrania. Huenda nabii alikuwa anafikiria wakati wa kurekebishwa kwa Yerusalemu na hali yake ya fahari kama nyakati za Daudi na Solomoni, Yerusalemu ilipokuwa mji mkuu wa taifa lote. Rejea 2Sam 5:6-9.
9Sasa kwa nini mnalia kwa sauti?
Je, hamna mfalme tena?
Mshauri wenu ametoweka?
Mnapaza sauti ya uchungu,
kama mama anayejifungua!#4:9 Kama mama anayejifungua: Manabii hulinganisha mateso yatakayowapata watu nyakati za mwisho na uchungu wa mama anayejifungua mtoto. Rejea Isa 66:7-9; Yer 4:31; 6:24; 22:23; Mat 24:19-22.
10Enyi watu wa Siyoni,
lieni na kugaagaa kama mama anayejifungua!
Maana sasa mtaondoka katika mji huu
mwende kukaa nyikani,
mtakwenda mpaka Babuloni.#4:10 Babuloni: Yamkini yahusu mateso yaliyowapata wengi waliobakia baada ya jeshi la Nebukadneza wa Babuloni kuteketeza mji wa Yerusalemu mwaka 587 K.K. (rejea 2Fal 24—25; 2Nya 36:5-21; Yer 52:3-11).
Lakini huko, mtaokolewa.
Huko Mwenyezi-Mungu atawakomboa makuchani mwa adui zenu.
11Mataifa mengi yamekusanyika kuwashambulia.
Yanasema: “Acheni mji wao utiwe najisi,
nasi tuyaone magofu ya Siyoni!”
12Lakini wao
hawafahamu mawazo ya Mwenyezi-Mungu
wala hawaelewi mpango wake:
kwamba amewakusanya pamoja,
kama miganda mahali pa kupuria.#4:12 Miganda mahali pa kupuria: Hapo kale watu walipovuna nafaka mashambani walikusanya miganda ya nafaka na kuitandaza mahali pakavu na pagumu, wakapitisha juu yake chombo cha kupuria na hivyo punje za nafaka zikaondolewa. Mika anatumia mfano huo kueleza hukumu ya adhabu ya Mungu lakini pia yenye matumaini kwani mbegu zinapatikana (taz pia Yer 51:33; Mat 3:12).
13Mwenyezi-Mungu asema,
“Enyi watu wa Siyoni,
inukeni mkawaadhibu adui zenu!
Nitawapeni nguvu kama fahali
mwenye pembe za chuma na kwato za shaba.
Mtawasaga watu wa mataifa mengi;
mapato yao mtaniwekea wakfu mimi,
mali zao mtanitolea mimi Bwana wa dunia yote.”#4:13 Bwana wa dunia yote: Zek 4:14; 6:5.
14Jumuikeni mkajikusanye enyi watu wa Yerusalemu;
mkisema: “Tumezingirwa, tumesongwa;
naye kiongozi wa Israeli wanampiga shavuni kwa fimbo.”