5
Kiongozi mpya kutoka Bethlehemu#5:1-14 Hesabu ya aya ya sura hii kama 1-15 ni sawa na 4:14, 5:2-14 katika Biblia ya Kiebrania.
1Mwenyezi-Mungu asema,
“Lakini wewe Bethlehemu katika Efratha,#5:1 Efratha: Neno hili ambalo linatokana na kishina cha neno lenye maana ya “kuzaa” (kwa mimea) lilitaja hapo kwanza ukoo fulani uliojiunga na ukoo wa Kalebu (rejea 1 Nya 2:19,24,50), ambao ulikaa katika eneo la Bethlehemu (rejea Rut 1:2; 1Sam 17:12; 1 Nya 4:4). Waandishi wa Injili wanatambua Bethlehemu kuwa ni mahali pa kuzaliwa kwa Masiha (Mat 2:6; Yoh 7:42).
wewe ni mdogo tu kati ya jamii za Yuda,
lakini kwako kutatoka mtawala
atakayetawala juu ya Israeli kwa niaba yangu.
Asili yake ni ya zama za kale.”#5:1 Asili yake ni ya zama za kale: Labda hapa ni dokezo kwa mfalme Daudi na ukoo wake wa kifalme. Daudi ambaye naye alitoka Bethlehemu (1Sam 16:1,13), alipokea ujumbe wa Mungu kupitia nabii Nathani ujumbe uliomtangazia kwamba ufalme wake utaimarishwa daima (2Sam 7:4-16). Rejea Zab 89:3-4; 132:11-12; Isa 9:2-7; 11:1-10.
2Hivyo Mungu atawaacha watu wake kwa maadui,
mpaka yule mama mjamzito atakapojifungua.#5:2 Mama mjamzito atakapojifungua: Wafafanuzi wengine wanafikiri hapa ni dokezo kwa Isa 7:14; wengine wanahusisha maneno haya na Mika 4:9-10 ambapo inasemwa kwamba watu wa Israeli kwa mfano wa mama aliye na uchungu wa kujifungua mtoto, watapata mfalme mwadilifu atakayewatoa uhamishoni.
Kisha ndugu zake waliobakia,
watarudi na kuungana na Waisraeli wenzao.
3Huyo mtawala atawachunga watu wake kwa nguvu ya Mwenyezi-Mungu,
kwa fahari yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wake.
Watu wake wataishi kwa usalama,
maana atakuwa mkuu mpaka miisho ya dunia.
4Yeye ndiye atakayeleta amani.#5:4 Ndiye atakayeleta amani: Tafsiri yamkini ya makala ngumu. Rejea Zab 72:7; Isa 9:6; 11:6-9; Zek 9:10. Taz pia Efe 2:14 maelezo.
Ukombozi na adhabu
Waashuru wakivamia nchi yetu,
na kuupenya ulinzi wetu,
tutapeleka walinzi wawakabili,
naam, tutawapeleka viongozi wetu kwa wingi.
5Kwa silaha zao wataitawala nchi ya Ashuru,
na kuimiliki nchi ya Nimrodi.#5:5 Nimrodi: Kadiri ya Mwanzo 10:8-11 Nimrodi alikuwa babu wa watu walioishi huko Mesopotamia. Na hapa ni jina lingine la Ashuru.
Watatuokoa mikononi mwa Waashuru,
watakapowasili mipakani mwa nchi yetu
na kuanza kuivamia nchi yetu.
6Wazawa wa Yakobo watakaobaki hai
wameenea miongoni mwa mataifa mengi,
watakuwa kama umande wa Mwenyezi-Mungu uburudishao,
kama manyunyu yaangukayo penye nyasi
ambayo hayasababishwi na mtu
wala kumtegemea binadamu.
7Wazawa wa Yakobo watakaobaki hai,
wameenea miongoni mwa mataifa na watu wengi
watakuwa na nguvu kubwa
kama simba kati ya wanyama wa porini,
kama mwanasimba miongoni mwa makundi ya kondoo,
ambaye kila mahali apitapo,
huyarukia na kuyararua mawindo yake,
asiwepo mtu yeyote wa kuyaokoa.
8Waisraeli watawashinda adui zao
na kuwaangamiza kabisa.
9Mwenyezi-Mungu asema,
“Wakati huo nitawaondoa farasi wenu,
na kuyaharibu magari yenu ya farasi.#5:9 Nitawaondoa farasi …magari yenu ya farasi: Waisraeli waliiga matumizi ya farasi kwa ajili ya vita wakati wa Solomoni (rejea 1Fal 10:26-29); baadaye, kwa kufuata mfano wa mataifa mengine, waliongeza majeshi yao na magari yao ya vita ya kukokotwa (rejea 1Fal 9:19; 10:26; 2Nya 1:14-17; 9:25-28). Kwa muda mrefu farasi walitumiwa kwa ajili ya vita (Yobu 39:19-25; rejea Zek 6:1-8; Ufu 6:1-8). Rejea Esta 6:8-11; Mhub 10:7. Manabii walikosoa fikira hizo za kutegemea farasi na magari ya vita maana hizo zilikuwa alama ya ukosefu wa kutegemea nguvu ya Mungu. Rejea Zab 20:7; Isa 2:4; 30:15-17; Hos 10:13; 14:3; Hag 2:22; Zek 9:10.
10Nitaiharibu miji ya nchi yenu,
na kuzibomolea mbali ngome zenu.
11Nitatokomeza matendo yenu ya uchawi,
nanyi hamtakuwa tena na wapiga ramli.
12Nitaziharibu sanamu zenu,
na nguzo zenu za ibada;
nanyi mtakoma kuabudu vitu mlivyotengeneza wenyewe.
13Nitazing'oa sanamu za Ashera#5:13 Sanamu za Ashera: Au: nguzo za Ashera, mungu wa kike wa watu wa Kanaani ambaye mfano wake ulikuwa nguzo au mti. kutoka kwenu,
na kuiangamiza miji yenu.
14Kwa hasira na ghadhabu yangu,
nitalipiza kisasi mataifa yote yasiyonitii.”