Marko 8
BHNTLK

Marko 8

8
Yesu anawapa chakula watu elfu nne#8:1-10 Yesu anawapa chakula watu elfu nne: Kisa hiki ni sambamba na kile cha kwanza katika Marko 6:40-44. Injili zote nne zimehifadhi tukio la kwanza, lakini ni Mathayo na Marko peke yao wanaotupatia tukio hili la pili.
(Mat 15:32-39)
1Wakati huo, umati mkubwa wa watu ulikusanyika tena, na hawakuwa na chakula. Basi, Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, 2“Nawaonea huruma watu hawa kwa sababu wamekuwa nami kwa siku tatu, wala hawana chakula. 3Nikiwaacha waende nyumbani wakiwa na njaa watazimia njiani, maana baadhi yao wametoka mbali.”
4Wanafunzi wake wakamwuliza, “Hapa nyikani itapatikana wapi mikate ya kuwashibisha watu hawa wote?” 5Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakamjibu, “Saba.”
6Basi, akawaamuru watu wakae chini. Akaitwaa ile mikate saba, akamshukuru Mungu, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu, nao wakawagawia. 7Walikuwa pia na visamaki vichache. Yesu akavibariki,#8:7 Akavibariki: Kulingana na desturi ya Kiyahudi aliye mkubwa katika jamii au wakati wa chakula alichukua mkate na kusema: “Shukrani kwako e Bwana, Mungu wetu, mtawala wa ulimwengu unayezalisha mkate wa dunia”, na waliopo waliitikia “Amina”. Kisha aligawa mkate. akaamuru vigawiwe watu vilevile. 8Watu wakala, wakashiba. Wakakusanya makombo wakajaza vikapu saba. 9Nao waliokula walikuwa watu wapatao 4,000. Yesu akawaaga, 10na mara akapanda mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda wilaya ya Dalmanutha.#8:10 Dalmanutha: Mahali ambapo hapajulikani sasa ila kwa kukisia ni upande wa magharibi wa ziwa Galilaya. Baadhi ya hati zina “Magadani” na nyingine “Magdala” (taz Mat 15:39).
Mafarisayo wanataka ishara
(Mat 16:1-4)
11Mafarisayo walikuja, wakaanza kujadiliana na Yesu. Kwa kumjaribu, wakamtaka afanye ishara#8:11 Ishara: Mat 12:38; Luka 11:16; Yoh 6:30. “Kutoka mbinguni”: Yaani kutoka kwa Mungu; taz Mat 16:1. Hapa ni dhahiri kwamba lengo la ishara hiyo ni kuonesha kwamba Yesu anayo idhini kutoka kwa Mungu. kutoka mbinguni. 12Yesu akahuzunika rohoni, akasema, “Mbona kizazi hiki kinataka ishara? Kweli nawaambieni, kizazi hiki hakitapewa ishara yoyote.” 13Basi, akawaacha, akapanda tena mashua, akaanza safari kwenda ng'ambo ya pili ya ziwa.
Chachu ya Mafarisayo na Herode
(Mat 16:5-12)
14Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate; walikuwa na mkate mmoja tu katika mashua. 15Yesu akawaonya, “Angalieni sana! Jihadharini na chachu#8:15 Chachu: Kitu ambacho kikiwekwa katika donge la kutengeneza mkate hulipenya na kulifanya lichache na kuumuka. Chachu inatumika hapa kama mfano wa uovu uliofichika ambao hupotosha kwa siri (taz pia 1Kor 5:6; Gal 5:9). ya Mafarisayo na chachu ya Herode.” 16Wanafunzi wakaanza kujadiliana wao kwa wao, “Anasema hivyo kwa kuwa hatuna mikate.” 17Yesu alitambua hayo, akawaambia, “Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate? Je, bado hamjafahamu, wala hamjaelewa? Je, mioyo yenu ni mizito? 18Je, mnayo macho na hamwoni?#8:18 Mnayo macho na hamwoni?: Mara nyingi manabii waliwakaripia Waisraeli kwamba ni watu waliokuwa vipofu na viziwi rohoni (Yer 5:21; Eze 12:2; rejea Marko 4:12). Mnayo masikio na hamsikii? Je, hamkumbuki 19wakati ule nilipoimega ile mikate mitano na kuwapa watu 5,000? Mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki.” Wakamjibu, “Kumi na viwili.” 20“Na nilipoimega ile mikate saba na kuwapa watu 4,000, mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki?” Wakamjibu, “Saba.” 21Basi, akawaambia, “Na bado hamjaelewa?”
Yesu anamponya kipofu wa Bethsaida#8:22-26 Sehemu hii inafanana na ile ya 7:32-37 kuhusu hatua Yesu anazochukua kumponya huyo kipofu wa Bethsaida.
22Yesu alifika Bethsaida pamoja na wanafunzi wake. Huko watu wakamletea kipofu, wakamwomba amguse. 23Yesu akamshika huyo kipofu mkono, akampeleka nje ya kijiji.#8:23 Akampeleka nje ya kijiji: Labda ambako hakukuwa na watu wengi. Baada ya kumponya anamwambia asirudi mjini (8:26). Akamtemea mate machoni,#8:23 Akamtemea mate machoni: Taz maelezo ya 7:33. Taz pia Yoh 9:6. akamwekea mikono, akamwuliza, “Je, unaweza kuona kitu?” 24Huyo kipofu akatazama, akasema, “Ninawaona watu wanaoonekana kama miti inayotembea.”#8:24-25 Hatuwezi kuelewa sasa kwa nini kitendo cha kumponya huyo kipofu kinafanyika katika hatua mbili. 25Kisha Yesu akamwekea tena mikono machoni, naye akakaza macho, uwezo wake wa kuona ukamrudia, akaona kila kitu sawasawa. 26Yesu akamwambia aende zake nyumbani na kumwamuru, “Usirudi kijijini!”#8:26 Usirudi mjini: Kwa maana ya kumzuia asije akatangaza habari za Yesu; jambo ambalo ni la kawaida katika Injili ya Marko. Baadhi ya hati za kale zinaongeza hapo: “Usimwambie mtu yeyote”.
Petro anamkiri Yesu kuwa Kristo#8:27-30 Tamko hili la Petro la kumkiri au kumuungama Kristo linafikia kilele cha sehemu ya kwanza ya Injili hii. (1:16—8:30) ambayo inadhihirisha kwamba kwa matendo yake na mafundisho yake, Yesu anaonesha yeye ni Masiha.
(Mat 16:13-20; Luka 9:18-21)
27Kisha Yesu na wanafunzi wake walikwenda katika vijiji vya Kaisarea Filipi.#8:27 Kaisarea Filipi: Mji kaskazini mwa ziwa Galilaya, eneo ambamo kwa wingi waliishi watu wasio Wayahudi. Mji huo ulijengwa na Herode Filipo kwa heshima ya mtawala mkuu wa Waroma yaani Kaisari. Walipokuwa njiani, Yesu aliwauliza wanafunzi wake, “Watu wanasema mimi ni nani?” 28Wakamjibu, “Wengine wanasema wewe ni Yohane Mbatizaji,#8:28 Yohane Mbatizaji: Marko 6:14-15; Luka 9:7-8. wengine Elia#8:28 Elia: Rejea 1Fal 17—2Fal 2 Wayahudi walitazamia kurudi kwake kabla ya ile siku ya Bwana (Mal 4:5-6); taz pia Mat 16:14. na wengine mmojawapo wa manabii.” 29Naye akawauliza, “Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?” Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Kristo.”#8:29 Kristo: Rejea Yoh 6:68-69. Kristo ni tafsiri ya Kigiriki ya jina la Kiebrania “Masiha”, maana yake “Aliyepakwa mafuta”, yaani aliyewekwa wakfu na Mungu kwa ajili ya wadhifa au kazi fulani. 30Kisha Yesu akawaonya#8:30 Akawaonya: Au, akawakaripia. Taz Marko 1:34 maelezo. wasimwambie mtu yeyote habari zake.
Yesu anasema juu ya mateso, kifo na kufufuka kwake#8:31—9:1 Hii ni sehemu ya pili ya Injili ya Marko, nayo yaanza na tangazo la Yesu mwenyewe kwamba atakufa na kufufuka (Mt 16:21-28; Luka 9:22-27). Yesu anasema juu ya kifo na ufufuo wake mara tatu, hapa, na katika 9:31-32; 10:32-34. Mara hizo zote tatu Yesu anaongea na wanafunzi wake peke yao.
(Mat 16:21-28; Luka 9:22-27)
31Yesu alianza kuwafundisha wanafunzi wake kwamba ni lazima Mwana wa Mtu#8:31 Mwana wa Mtu: Taz 2:10. Hapa mkazo uko katika mateso yake. apatwe na mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na waalimu wa sheria. Kwamba atauawa, na baada ya siku tatu atafufuka. 32Yesu aliwaambia jambo hilo waziwazi. Hapo, Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea. 33Lakini Yesu akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro akisema, “Ondoka mbele yangu Shetani! Mawazo yako si ya kimungu ila ni ya kibinadamu.”
34Kisha akauita umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Kama mtu yeyote anataka kuwa mfuasi wangu, lazima ajikane mwenyewe,#8:34 Ajikane mwenyewe: Au, ajiache mwenyewe. Taz 14:30-31,72; vilevile Mat 10:38; Luka 14:27. auchukue msalaba#8:34 Msalaba: Ulikuwa chombo cha kuwatesa waliotakiwa kuuawa (Taz 15:21,30,32). Taz pia matumizi yake katika Rom 6:2-11; Gal 2:19; 6:14; Kol 3:3-5. wake, anifuate. 35Maana mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza, lakini mtu anayepoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Habari Njema, atayaokoa. 36Je, kuna faida gani mtu kuupata ulimwengu wote na kuyapoteza maisha yake? 37Ama mtu atatoa kitu gani badala ya maisha yake? 38Mtu yeyote katika kizazi hiki kiovu na kisicho na uaminifu kwa Mungu,#8:38 Kizazi kiovu na kisichomjali Mungu: Kama vile Mat 12:39. anayenionea aibu mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Mtu atamwonea aibu mtu huyo, wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza