36
Urithi wa wanawake walioolewa#36:1-13 Sheria inayotajwa hapa inatimiza agizo lililotajwa katika Hes 27:1-11 kwamba mama ambaye alirithi mali alipaswa kuolewa katika kabila lake na sio nje ya kabila hilo kusudi urithi usiende kwa kabila jingine.
1Viongozi wa jamaa katika ukoo wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, mwana wa Yosefu, walikwenda kuzungumza na Mose na viongozi wengine wa koo za Waisraeli. 2Wakasema, “Bwana wetu, Mwenyezi-Mungu alikuamuru kuwagawia watu wa Israeli nchi kwa kura, kuwa urithi wao; alikuamuru pia uwape binti za Selofehadi ndugu yetu urithi wa baba yao. 3Lakini wao wakiolewa na Waisraeli wa makabila mengine, urithi wao utatoka kwetu na kuwaendea watu wa kabila watakamoolewa; kwa hiyo urithi wetu sisi utapungua. 4Katika sikukuu ya ukumbusho#36:4 Sikukuu ya ukumbusho: Taz Lawi 25:8-16 juu ya sikuu ya miaka hamsini au kwa jina lingine “Yubile”. urithi wao utahesabiwa pamoja na ule wa kabila watakamoolewa na hivyo kabila letu halitapata urithi huo tena.”
5Basi, Mose akawapa Waisraeli agizo lifuatalo kutoka kwa Mwenyezi-Mungu, akawaambia, “Watu wa ukoo wa kabila la Yosefu, wamesema ukweli. 6Na hivi ndivyo anavyoamuru Mwenyezi-Mungu kuhusu binti za Selofehadi; wako huru kuolewa na mtu yeyote wampendaye, lakini waolewe katika kabila lao, 7ili urithi wa Waisraeli usihamishiwe kwa kabila lingine; kila Mwisraeli atazingatia urithi wa kabila lake. 8Mwanamke yeyote mwenye urithi katika kabila mojawapo la Israeli ni lazima aolewe na mtu wa kabila lake, ili kila Mwisraeli achukue urithi wa babu zake. 9Hivyo hapatakuwa na urithi wowote utakaohamishwa kutoka kabila moja hadi jingine. Kila kabila la Waisraeli litashikilia urithi wake.”
10Binti za Selofehadi walifanya kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. 11Wote: Mala, Tirza, Hogla, Milka na Noa wakaolewa na binamu zao. 12Waliolewa katika jamaa za ukoo wa Manase mwana wa Yosefu, na urithi wao ukabaki katika kabila la baba yao.
13Hizo ndizo amri na maagizo ambayo Mwenyezi-Mungu aliwapa Waisraeli kwa njia ya Mose katika tambarare za Moabu, ng'ambo ya Mto Yordani karibu na mji wa Yeriko.#36:13 Yahusu jumla ya sheria alizopewa Mose kwenye tambarare za Moabu (sura 22—36). Historia inaendelea katika Kumb 31—34 na katika kitabu cha Yoshua.