Methali 13
BHNTLK

Methali 13

13
1Mtoto mwenye hekima husikia maagizo ya baba yake,
lakini mwenye dharau hasikilizi maonyo.
2Mtu mwema hupata mema kutokana na maneno yake,
lakini wadanganyifu huishi kwa ukatili.
3Achungaye mdomo wake huyahifadhi maisha yake,
anayeropoka ovyo hujiletea maangamizi.
4Mvivu hutamani lakini hapati chochote,
hali mwenye bidii#13:4 Mvivu …mwenye bidii: Taz 6:10-11 maelezo. hujaliwa riziki kwa wingi.
5Mwadilifu huuchukia uongo,
lakini mwovu hutenda kwa aibu na fedheha.
6Uadilifu huwalinda wenye mwenendo mnyofu,
lakini dhambi huwaangusha waovu.
7Baadhi hujidai kuwa matajiri kumbe hawana kitu;
wengine hujiona kuwa maskini hali wana mali tele.
8Fidia ya mtu ni mali yake,
lakini maskini hana cha kutishwa.
9Mwadilifu hung'aa kama taa iwakayo vizuri,
lakini waovu ni kama taa inayozimika.
10Kiburi husababisha tu ugomvi,
lakini kwa wanaokubali shauri jema mna hekima.
11Mali ya harakaharaka hutoweka,
lakini akusanyaye kidogokidogo ataiongeza.
12Tumaini la kungojangoja huumiza moyo,
lakini tazamio linalotimia ni mti wa uhai.#13:12 Ni mti wa uhai: Taz 3:14-18 maelezo.
13Anayedharau mawaidha anajiletea maangamizi,
lakini anayetii amri atapewa tuzo.
14Mafundisho ya wenye hekima ni chemchemi ya uhai;#13:14 Chemchemi ya uhai: Viumbe viishivyo haviwezi kudumu bila maji. Vivyo hivyo na mafundisho ya Hekima ni muhimu kwa binadamu kama maji kwa viumbe hai (taz pia 14:27).
humwezesha mtu kuiepa mitego ya kifo.
15Kuwa na akili huleta fadhili,
lakini njia ya waovu ni ya taabu#13:15 Tafsiri yamkini ya makala ngumu ya Kiebrania.
16Mwenye busara hutenda kila kitu kwa akili,
lakini mpumbavu hutembeza upumbavu wake.
17Mjumbe mbaya huwatumbukiza watu taabuni,#13:17 Huwatumbukiza watu taabuni: Au, “huanguka taabuni”. Mjumbe mbaya huweza kusababisha matatizo kwa kutoa habari zisizo sahihi. Lakini mjumbe mzuri, kwa maneno yake mazuri huweza kuwaburudisha watu wakasikiliza. Taz pia 12:18 na 25:13.
lakini mjumbe mwaminifu huleta nafuu.
18Umaskini na fedheha humpata asiyejali mafundisho,
lakini mwenye kusikia maonyo huheshimiwa.
19Inafurahisha upatapo kile unachotaka,
kwa hiyo wapumbavu huchukia kuepa uovu.
20Anayeandamana na wenye hekima hupata hekima,
lakini anayejiunga na wapumbavu atapata madhara.
21Watendao dhambi huandamwa na balaa,
lakini waadilifu watatuzwa mema.
22Mtu mwema huwaachia urithi uzao wake,
lakini mali ya mwenye dhambi imerundikiwa waadilifu.
23Shamba la maskini hutoa mazao mengi,
lakini bila haki hunyakuliwa.#13:23 Makala ya Kiebrania ya aya hii si dhahiri.
24Asiyemwadhibu mtoto wake hampendi;
lakini ampendaye mwanawe humrudi mapema.#13:24 Adhabu na nidhamu daima vilichukuliwa kuwa njia mojawapo ya kuwaepuesha watoto kukua kijinga au kipumbavu na hivyo kujidhuru wao wenyewe na pia watu wengine. Rejea pia methali ya Kiswahili: “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo”. Taz pia Meth 19:18; 29:15,17.
25Mwadilifu anacho chakula cha kumtosheleza,
lakini tumbo la waovu hutaabika kwa njaa.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza