16
1Binadamu hupanga mipango yake,
lakini kauli ya mwisho ni yake Mwenyezi-Mungu.
2Matendo ya mtu huonekana kwake kuwa sawa,
lakini Mwenyezi-Mungu hupima nia ya mtu.#16:2 Taz 21:2 maelezo.
3Mwekee Mwenyezi-Mungu kazi yako,
nayo mipango yako itafanikiwa.
4Mwenyezi-Mungu ameumba kila kitu kwa kusudi lake;#16:4 Ameumba …kwa kusudi lake: Linganisha na Mhub 3:1-15. Hayo malengo au makusudi ya Mungu mara nyingi sana si dhahiri kwa binadamu. Ling Yobu 21:30; Isa 43:7; Rom 9:22; 11:36.
hata waovu kwa ajili ya siku ya maangamizi.
5Kila mwenye kiburi ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu;
hakika mtu wa namna hiyo hataacha kuadhibiwa.
6Kwa utii na uaminifu mtu huondolewa dhambi,#16:6 Kwa utii …huondolewa dhambi: Wanaoacha dhambi na kumrudia Mungu wanaweza kusamehewa dhambi. Taz pia Zab 51:1-14; Hos 14:1,8-9.
kwa kumcha Mwenyezi-Mungu huepuka uovu.
7Mwenyezi-Mungu akipendezwa na mwenendo wa mtu,
huwageuza hata adui zake kuwa marafiki.
8Afadhali mali kidogo kwa uadilifu,
kuliko mapato mengi kwa udhalimu.
9Mtu aweza kufanya mipango yake,
lakini Mwenyezi-Mungu huongoza hatua zake.
10Mfalme huamua kwa maongozi ya Mungu;
anapotoa hukumu hakosei.#16:10 Mfalme …hakosei: Si rahisi kuelewa msemo huu hapa kuwa kweli. Kulingana na Biblia kulipata kuwa wafalme wabaya tena sana. Lakini katika Israeli ya kale wafalme walichukuliwa kuwa wanaotawala badala ya Mungu na kama vile Mungu daima hutenda yaliyo sawa wao pia walichukuliwa kwamba wangetenda daima yaliyo sawa. Aya 12 inataja dhahiri kwamba ni chukizo kwa mfalme kuwa mwovu.
11Mwenyezi-Mungu hutaka kipimo na mizani halali;#16:11 Kipimo na mizani halali: Taz aya ya 11:1 maelezo; ling Lawi 19:36.
mawe yote mfukoni ya kupimia ni kazi yake.
12Ni chukizo kubwa wafalme kutenda uovu,
maana msingi wa mamlaka yao ni haki.
13Mfalme hupendelea mtu asemaye kwa unyofu;
humpenda mtu asemaye ukweli.
14Hasira ya mfalme ni kama mjumbe wa kifo;
mtu mwenye busara ataituliza.
15Uso wa mfalme uking'aa kuna uhai;
wema wake ni kama wingu la masika.
16Kupata hekima ni bora kuliko dhahabu;
kupata akili ni chaguo bora kuliko fedha.
17Njia ya wanyofu huepukana na uovu;
anayechunga njia yake huhifadhi maisha yake.
18Kiburi hutangulia maangamizi;#16:18 Kiburi hutangulia maangamizi: Taz 11:2 maelezo.
majivuno hutangulia maanguko.
19Afadhali kuwa mnyenyekevu na kuwa maskini,
kuliko kugawana nyara na wenye kiburi.
20Anayezingatia mafundisho atafanikiwa;
heri mtu yule anayemtumainia Mwenyezi-Mungu.
21Mwenye hekima moyoni huitwa mwenye akili;
neno la kupendeza huwavutia watu.
22Hekima ni chemchemi ya uhai#16:22 Hekima ni chemchemi ya uhai: Taz 13:14 maelezo. kwake aliye nayo,
bali upumbavu ni adhabu ya wapumbavu.
23Moyo wa mwenye hekima humwezesha kusema kwa busara;
huyafanya maneno yake yawe ya kuvutia.
24Maneno mazuri ni kama asali;
ni matamu rohoni na yenye kuupa mwili afya.
25Mtu aweza kuona njia yake kuwa sawa,
lakini mwishowe humwongoza kwenye kifo.
26Hamu ya chakula humhimiza mfanyakazi,
maana njaa yake humsukuma aendelee.#16:26 Njaa yake humsukuma aendelee: Njaa inaweza kumsukuma mtu kulima, kupanda na kupata chakula. Taz pia 2Thes 3:10.
27Mtu mwovu hupanga uovu;
maneno yake ni kama moto mkali.
28Mtu mpotovu hueneza ugomvi,
mfitini hutenganisha marafiki.
29Mtu mkatili humshawishi jirani yake;
humwongoza katika njia mbaya.
30Anayekonyeza jicho kwa hila amepanga maovu;
anayekaza midomo#16:30 Anayekonyeza jicho …anayekaza midomo: Taz 6:13 maelezo. Kitenzi “anayekonyeza jicho” kinatumiwa hapa tu katika A.K. na kinaweza kuwa na maana nyingi katika tamaduni tofauti. Hapa ni ishara inayoashiria kwamba kitu kiovu kinapangwa kufanyika na huyo mwenye kufanya hivyo. Mstari wa pili unaonekana kumwambia huyo anayekonyezewa asitoe siri ya mpango huo mbaya. amekwisha nuia mabaya.
31Kuwa na mvi za uzee ni taji la utukufu;
hupatikana kwa maisha ya uadilifu.#16:31 Mvi za uzee …taji la utukufu, hupatikana kwa maisha ya uadilifu: Inamaanisha kwamba huyo mtu amezingatia hekima, akaishi sawa (1:3) akajaliwa maisha marefu (3:16; 20:29).
32Asiye mwepesi wa hasira ni bora kuliko mwenye nguvu;
aitawalaye nafsi yake ni bora kuliko autekaye mji.
33Kura hupigwa kujua yatakayotukia,
lakini uamuzi ni wake Mwenyezi-Mungu.