22
1Afadhali kuwa na sifa nzuri kuliko mali nyingi;
wema ni bora kuliko fedha au dhahabu.
2Matajiri na maskini wana hali hii moja:
Mwenyezi-Mungu ni Muumba wao wote.
3Mtu mwangalifu huona hatari akajificha,
lakini wajinga hujitokeza mbele wakaumia.
4Ukinyenyekea na kumcha Mwenyezi-Mungu,#22:4 Kumcha Mwenyezi-Mungu: Taz 1:7 maelezo.
utapata tuzo: fanaka, heshima na uhai.
5Njia ya waovu imejaa miiba na mitego;
anayetaka kuhifadhi maisha yake ataiepa.
6Mfunze mtoto namna ya kuishi#22:6 Mfunze mtoto …kuishi: Mfunze hekima (4:1-5; 6:20-22); mpe nidhamu na kumkosoa au kumrudi (3:12). vizuri,
naye hatasahau njia hiyo hata uzeeni.
7Tajiri humtawala maskini;
mkopaji ni mtumwa wa mkopeshaji.#22:7 Mkopaji ni mtumwa wa mkopeshaji: Mara nyingine mkopaji aliyeshindwa kulipa mkopo wake alifanywa kuwa mtumwa ili aufanyie kazi mkopo wake jambo ambalo lilikuwa mzigo mzito kwa watu.
8Apandaye dhuluma atavuna janga;
uwezo wake wa kutenda mabaya utavunjwa.
9Mtu mkarimu atabarikiwa,
maana chakula chake humgawia maskini.#22:9 Mkarimu atabarikiwa …maskini: Yaani Mungu atambariki. Taz 14:31 maelezo; rejea pia 19:17 maelezo.
10Mfukuze mwenye dharau na fujo itatoweka,
ugomvi na matusi vitakoma.
11Mwenye nia safi na maneno mazuri,
atakuwa rafiki wa mfalme.
12Mwenyezi-Mungu hulinda elimu ya kweli,
lakini huyavuruga maneno ya waovu.
13Mvivu#22:13 Mvivu …kuna simba huko, ataniua: Taz 26:13. husema, “Siwezi kutoka nje;
kuna simba huko, ataniua!”
14Kinywa cha mwasherati ni shimo refu;#22:14 Kinywa cha mwasherati …shimo refu: Huenda hapa “shimo refu” ni lugha ya mfano kuashiria Kuzimu.
anayechukiwa na Mwenyezi-Mungu atatumbukia humo.
15Mtoto hupenda mambo ya kijinga moyoni,
lakini fimbo ya nidhamu humwondolea hayo.
16Anayemdhulumu maskini atamfanya afaidike mwishowe,
anayewapa matajiri zawadi ataishia kuwa maskini.#22:16 Anayemdhulumu maskini …maskini: Tafsiri ngumu. Tafsiri nyingine yamkini: “Anayemdhulumu maskini na anayewapa matajiri zawadi wote watapata hasara”.
Misemo thelathini ya wenye hekima#22:17—24:34 Misemo thelathini ya wenye hekima: Hao “wenye hekima” (aya 1) ni akina nani haisemwi lakini msemo huo huenda lengo lake ni kutumika kama kichwa cha sehemu inayofuata. Baadhi ya hiyo Misemo thelathini ya wenye hekima (22:17—24:22) inafanana na misemo ya hekima kutoka mkusanyo wa Misri unaojulikana kama “Mafunzo ya Amenemope” ambao uligawanyika katika “nyumba” au sehemu thelathini. Nyingi ya misemo ya sehemu ni ya namna ya mafunzo na inahusu namna ya kujistahi katika jamii (nambari 6,8), watu wa kuepa (nambari 2,17,19,27,28), ulafi: yaani kula na kunywa bila kiasi (namba 15,18), kujichukulia madeni ya mtu mwingine (namba 3), kuondoa alama za mipaka ya vishamba (nambari 4,10), n.k.
17Tega sikio usikie maneno ya wenye hekima,
elekeza moyo wako uzingatie maarifa yangu.
18Wewe utafurahi endapo utayaweka moyoni,
na kuyakariri kila wakati.
19Ninayependa kumfundisha leo ni wewe,
ili tegemeo lako liwe kwa Mwenyezi-Mungu.#22:19 Tegemeo …kwa Mwenyezi-Mungu: Lengo la kujifunza hekima sio tu kufanikisha akili bali hasa kukua kiroho.
20Nimekuandikia misemo thelathini,
misemo ya maonyo na maarifa,
21ili kukufundisha yaliyo sawa na kweli;
na mtu akikuuliza uweze kumpa jibu sahihi.
- 1 -
22Usimdhulumu maskini kwa kuwa ni maskini,
wala usimnyime fukara haki yake mahakamani.
23Maana Mwenyezi-Mungu atawatetea;#22:22-23 Usimdhulumu maskini …Mwenyezi-Mungu atawatetea: Rejea 14:31; 19:17 maelezo.
atawapokonya maisha yao wale watakaowadhulumu.
- 2 -
24Usifanye urafiki na mtu wa hasira,
wala usiandamane na mwenye ghadhabu,
25usije ukajifunza mwenendo wake,
ukajinasa kabisa katika mtego.
- 3 -
26Usiwe mmoja wao wenye kuweka ahadi,
watu ambao hujiweka wadhamini wa madeni.
27Ikiwa huna chochote cha kulipa,
hata kitanda unacholalia kitachukuliwa!
- 4 -
28Usiondoe alama ya mipaka ya zamani
ambayo iliwekwa na wazee wako.
- 5 -
29Je, yuko mtu mwenye maarifa kazini mwake?
Huyo atawatumikia wafalme;
hatawapa huduma yake watu wasiofaa.