Methali 24
BHNTLK

Methali 24

24
- 19 -
1Usiwaonee wivu watu waovu,
wala usitamani kuwa pamoja nao,
2maana fikira zao zote ni juu ya ukatili,
hamna jema lolote litokalo midomoni mwao.
- 20 -
3Nyumba hujengwa kwa hekima,#24:3-4 Nyumba hujengwa kwa hekima: Taz maelezo ya Hekima anavyojenga nyumba yake (9:1).
na kuimarishwa kwa busara.
4Kwa maarifa vyumba vyake hujazwa
vitu vya thamani na vya kupendeza.
- 21 -
5Kuwa na hekima ni bora kuliko kuwa na nguvu,
naam, maarifa ni bora kuliko nguvu.#24:5 Hekima …maarifa ni bora kuliko nguvu: Au: “Mwenye hekima anampita mwenye nguvu”.
6Maana kwa mwongozo mzuri waweza kupigana vita,
na kwa washauri wengi ushindi hupatikana.
- 22 -
7Kwa mpumbavu hekima ni ngumu kuielewa;
penye mkutano wa mashauri hafungui mdomo.
- 23 -
8Afikiriaye kutenda maovu daima
ataitwa mtu mwenye fitina.
9Mpango anaofikiria mpumbavu ni dhambi;
mwenye dharau huchukiwa na kila mtu.
- 24 -
10Ukifa moyo wakati wa shida,
basi wewe ni dhaifu kweli.
- 25 -
11Mwokoe mtu anayechukuliwa kuuawa bure;
usisite kumwokoa anayeuawa bila hatia.#24:11-12 Usisite kumwokoa mtu anayeuawa bila hatia …: Mtunzi wa methali anaona kuwa kuacha nafasi ya kumwokoa mtu anayeuawa bila hatia ni dhambi, kama vile pia kuacha kumsaidia maskini na mhitaji (Isa 58:6-7; Yak 2:14-15). Taz pia 1Yoh 3:16. Mtu hataweza kuepa lawama kwani Mungu anajua mawazo ya ndani kabisa ya mtu (6:2; 21:2).
12Usiseme baadaye: “Hatukujua!”
Maana Mungu apimaye mioyo ya watu huona;
yeye atakulipa kulingana na matendo yako!
- 26 -
13Mwanangu, ule asali maana ni nzuri;
sega la asali ni tamu mdomoni.
14Ndivyo ilivyo hekima nafsini mwako;
ukiipata utakuwa na matazamio mema,
wala tumaini lako halitakuwa la bure.
- 27 -
15Usivizie kama mwovu kushambulia makao ya mtu mwema,
wala usijaribu kuiharibu nyumba yake,
16maana mtu mwema huanguka mara nyingi lakini huinuka,
lakini mtu mwovu huangamizwa na janga.
- 28 -
17Usishangilie kuanguka kwa adui yako;
usifurahie moyoni mwako kujikwaa kwake,
18maana Mwenyezi-Mungu aonaye hayo hatapendezwa;
huenda akaacha kumwadhibu.
- 29 -
19Usihangaike kwa sababu ya watenda mabaya,
wala usiwaonee wivu watu waovu,
20maana mwovu hatakuwa na mema baadaye;
taa ya uhai wake itazimwa.
- 30 -
21Mwanangu, umche Mwenyezi-Mungu na kumheshimu mfalme,
wala usishirikiane na wale wasio na msimamo,
22maana maangamizi yao huwapata ghafla.
Hakuna ajuaye maafa watakayozusha.
Misemo zaidi
23 # 24:23 Methali zinazotajwa katika 24:23-34 zinafanana na zile za 22:17-21 lakini si dhahiri ni nani aliyezitunga. Ifuatayo pia ni misemo ya wenye hekima:
Kupendelea watu katika hukumu si vizuri.#24:23-25 Kupendelea …hukumu si vizuri: Mahakimu walitakiwa kuamua kwa haki (18:5). Taz pia Lawi 19:15; Kumb 1:16-17; 16:18-19.
24Anayemwachilia mtu mwenye hatia,
hulaaniwa na watu na kuchukiwa na mataifa.
25Lakini wanaowaadhibu waovu watapata furaha,
na baraka njema zitawajia.
26Jibu lililo la haki,
ni kama busu la rafiki.
27Kwanza fanya kazi zako nje,
tayarisha kila kitu shambani,
kisha jenga nyumba#24:27 … tayarisha … shambani, kisha jenga nyumba: Huenda msemo huo ulikuwa na shabaha ya kuonya kufanya vitu vya maana kwanza. yako.
28Usishuhudie bure dhidi ya jirani yako,
wala usiseme uongo juu yake.
29Usiseme, “Nitamtenda kama alivyonitenda!
Ni lazima nilipize kisasi!”
30Nilipitia karibu na shamba la mvivu;
shamba la mzabibu la mtu mpumbavu.
31Nilishangaa kuona limemea miiba,
magugu yamefunika eneo lake lote,
na ukuta wake wa mawe umebomoka.
32Nilitazama, nikawaza,
mwishowe nikapata funzo:
33Lala tu kidogo; sinzia tu kidogo!
Kunja mikono yako tu upumzike!
34Lakini kumbuka kwamba uwapo usingizini,
umaskini utakuvamia#24:30-34 Shamba la mvivu …umaskini utakuvamia …: Aya hizi zinamalizia sehemu iliyoanza katika 22:17. Na kuhusu kufanya kazi kwa bidii taz pia 6:6-11. kama mnyang'anyi,
ufukara kama mtu mwenye silaha.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza