Methali 26
BHNTLK

Methali 26

26
1Heshima apewayo mpumbavu haimfai;
ni kama theluji ya kiangazi,
au mvua ya wakati wa mavuno.#26:1 Theluji ya kiangazi …mvua ya wakati wa mavuno: Huko Mashariki ya Kati mvua (na theluji) hainyeshi wakati wa miezi ya Juni hadi Septemba. Mtunzi wa methali anasema kumpa mpumbavu heshima ni kitu kisichowezekana.
2Kama shomoro au mbayuwayu wasiotua,
kadhalika laana asiyostahili mtu haimtui.
3Mjeledi kwa farasi, lijamu kwa punda,
na fimbo kwa mgongo wa mpumbavu.#26:3 Fimbo kwa mgongo wa mpumbavu: Kama vile mnyama aongozwavyo kwa fimbo ndivyo naye mpumbavu, apate kuelekea njia iliyo sawa.
4Usimjibu mpumbavu kipumbavu,
usije ukafanana naye.
5Mjibu mpumbavu kama ustahilivyo upumbavu wake,
asije akajiona kuwa mwenye hekima zaidi.
6Kumtuma mpumbavu ujumbe,
ni kama kujikata miguu au kujitafutia shida.
7Methali mdomoni mwa mpumbavu,
ni kama miguu ya kiwete inayoning'inia.
8Kumpa mpumbavu heshima,
ni kama kufunga jiwe kwenye kombeo.#26:8 Kufunga jiwe kwenye kombeo: Jiwe halifungwi kwenye kombeo bali linawekwa hapa kusudi anayelirusha aliachie lielekee linakotakiwa. Lakini likifungwa huko wakati wa kulirusha linaweza kumrudia mwenye kulirusha. Ndiyo maana ya methali hii: kumpa heshima mpumbavu utajiumiza mwenyewe.
9Mpumbavu anayejaribu kutumia methali,
ni kama mlevi anayejaribu kung'oa mwiba mkononi.
10Mtu amwajiriye mpumbavu au mlevi,
ni kama mpiga upinde anayejeruhi kila mtu.#26:10 Makala ya Kiebrania si dhahiri.
11Mpumbavu anayerudiarudia upumbavu wake,
ni kama mbwa anayekula matapishi yake.#26:11 Mpumbavu …mbwa anayekula matapishi yake: Sehemu ya methali hii imenukuliwa katika 2Pet 2:22.
12Wamwona mtu ajionaye kuwa mwenye hekima?
Nakuambia mpumbavu ni nafuu kuliko huyo.
13Mvivu husema: “Huko nje kuna simba;
siwezi kwenda huko.”#26:13 Mvivu … “kuna simba; siwezi kwenda huko”: Taz methali hiyohiyo katika 22:13. Uvivu na wavivu ni wazo linalotajwa mara nyingi katika sura hii (rejea 26:13-16). Kuepa kuliwa na simba ni kisingizio cha kutokwenda kazini. Mvivu anafikiri amewapita wengine kwa akili.
14Kama vile mlango uzungukiapo bawaba zake,
ndivyo mvivu juu ya kitanda chake.
15Mvivu huutia mkono wake katika sahani ya chakula,
lakini hawezi kuuinua hadi mdomoni.
16Mvivu hujiona kuwa mwenye hekima
kuliko watu saba wawezao kujibu kwa busara.
17Ajiingizaye katika ugomvi usiomhusu,
ni kama mtu amshikaye masikio mbwa anayepita.
18Kama mwendawazimu achezeavyo mienge,
au mishale ya kifo,
19ndivyo alivyo mtu ampotoshaye jirani,
kisha aseme, “Nilikuwa natania tu!”
20Bila kuni, moto huzimika;
bila mchochezi, ugomvi humalizika.
21Kama vile makaa au kuni huchochea moto,
ndivyo mgomvi achocheavyo ugomvi.
22Maneno ya msengenyaji ni kama kitoweo;
hushuka mpaka ndani kabisa tumboni.
23Kama rangi angavu iliyopakwa kigae,
ndivyo yalivyo maneno matamu yenye nia mbaya.#26:23 Rangi angavu …kigae … maneno matamu… nia mbaya: Kigae kilichopakwa rangi hakibadiliki; ndivyo na maneno ya nia mbaya yaliyopakwa utamu.
24Mwenye chuki huficha chuki yake kwa maneno mazuri,
lakini huwa ana hila moyoni mwake.
25Akiongea vizuri usimwamini,
moyoni mwake mna chuki chungu nzima.
26Huenda akaficha chuki yake,
lakini nia zake mbaya zitajulikana kwa wote.
27Amchimbiaye mwenzake shimo, hutumbukia mwenyewe;#26:27 Amchimbiaye …hutumbukia mwenyewe: Huu ni msemo unaorudiwa pia katika vitabu vya hekima. Taz k.m. Zab 7:15-16; Mhub 10:8; Sira 27:25-27.
abingirishaye jiwe litamrudia mwenyewe.
28Asemaye uongo huwachukia hao anaowaumiza,
naye abembelezaye huleta maangamizi.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza