27
1Usijisifie ya kesho,#27:1 Usijisifie ya kesho …: Taz mfano katika Luka 12:16-21; ling Yak 4:13-16.
hujui nini kitatokea leo mpaka kesho.
2Acha watu wengine wakusifu,#27:2 Acha watu wengine wakusifu …: Taz onyo la namna hiyo katika 25:6-7.
kuliko mdomo wako wewe mwenyewe.
3Jiwe ni zito na mchanga kadhalika,
lakini usumbufu wa mpumbavu ni mzito zaidi.
4Ghadhabu ni katili na hasira huangamiza;
lakini ni nani awezaye kuukabili wivu?
5Afadhali mtu anayekuonya waziwazi,
kuliko yule afichaye upendo.
6Makaripio ya rafiki yaonesha uaminifu,
lakini busu la adui ni udanganyifu.
7Aliyeshiba hata asali huikataa,
lakini kwa mwenye njaa kila kichungu ni kitamu.
8Mtu aliyepotea mbali na kwake,
ni kama ndege aliyepotea mbali na kiota chake.
9Mafuta na manukato huufurahisha moyo,
lakini taabu hurarua roho.#27:9 Lakini taabu hurarua roho: Tafsiri yamkini. Maana katika Kiebrania si dhahiri.
10Usisahau rafiki zako wala wa baba yako.#27:10 Usisahau rafiki zako wala wa baba yako: Hapa kuna misemo mitatu ambayo imekuja pamoja kwa sababu ya matumizi ya maneno yanayofanana kimsingi: rafiki, ndugu (au jamaa) na jirani. Ni onyo dhidi ya kuwategemea tu watu wa jamaa. Taz misemo inayofanana katika 27:5-6,9; 17:17; 18:24.
Ukipatwa na janga usikimbilie kwa nduguyo;
afadhali jirani aliye karibu kuliko ndugu aliye mbali.
11Uwe na hekima mwanangu upate kunifurahisha moyo,
nami sitakosa la kumjibu yeyote anayenilaumu.#27:11 Hekima mwanangu …sitakosa la kumjibu … anayenilaumu.: Sifa za wazazi ziliambatana na mienendo ya watoto wao. Taz 10:1; 23:15-16.
12Mwenye busara huona hatari akajificha,
lakini mjinga hujitokeza mbele akaumia.
13Mtu akiahidi mbele yako kumdhamini mgeni, chukua nguo yake;
mfanye awajibike kwa kuwadhamini wageni.
14Amwamkiaye jirani kwa kelele alfajiri,
itaeleweka kwamba amemtakia laana.
15Mke mgomvi daima,
ni sawa na tonatona ya maji siku ya mvua.
16Kumzuia ni sawa na kuzuia upepo,
au kukamata mafuta kwa mkono.#27:16 Kumzuia …kukamata mafuta kwa mkono: Maana katika Kiebrania ya maneno “kukamata mafuta kwa mkono” si dhahiri. Tofauti kati ya mwanamke mgomvi na mwema ni wazo linalorudiwa mara kwa mara katika kitabu hiki (ling 21:19 na 25:24 pamoja na 31:10-31). Kuzuia upepo ni jambo lisilowezekana; na mafuta huteleza. Taz Mhub 1:14,17; 2:26.
17Chuma hunoa chuma,
kadhalika mtu hufundishwa na wenzake.
18Anayeutunza mtini hula tini,
anayemhudumia bwana wake ataheshimiwa.
19Kama uso ujionavyo wenyewe majini,
ndivyo ujijuavyo mwenyewe moyoni.
20Kuzimu na Uharibifu kamwe havishibi,
kadhalika na macho ya watu hayashibi.#27:20 Kuzimu na Uharibifu kamwe havishibi: Kuzimu na Uharibifu (Kiebrania: “Abadoni”) kulifikiriwa kuwa ni shimo kuu ndani ya dunia ambamo waliokufa walikwenda (30:15-16).
21Ubora wa fedha au dhahabu hupimwa kwa moto,#27:21 Ubora wa fedha au dhahabu hupimwa kwa moto: Kuhusu wazo lingine juu ya msemo huu taz 17:3.
na mtu hupimwa kutokana na sifa zake.
22Mtwange mpumbavu katika kinu pamoja na nafaka,
lakini hutafaulu kumtenganisha na upumbavu wake.
23Angalia vizuri hali ya mifugo yako;
tunza vizuri wanyama wako.
24Maana utajiri haudumu milele,
wala taji haidumu vizazi vyote.
25Baada ya kukata nyasi na kuzihifadhi,
kata majani toka milimani,
huku nyasi zinachipua upya.
26Kondoo watakupatia sufu kwa mavazi,
mbuzi nao utauza na kujinunulia mashamba;
27watakupa maziwa ya kukutosha wewe na jamaa yako,
na kwa ajili ya watumishi wako wa kike.