Methali 5
BHNTLK

Methali 5

5
Onyo dhidi ya uasherati
1Mwanangu, sikia hekima yangu,
tega sikio usikilize elimu yangu.
2Ndipo utakapoweza kuhifadhi busara,
na midomo yako izingatie maarifa.
3Mdomo wa mwanamke mpotovu#5:3 Mdomo wa mwanamke mpotovu: Hapa yahusu yamkini mwanamke wa mtu mwingine ambaye huenda pia akawa ni mwanamke mpotovu. Taz 2:16-17. ni mtamu kama asali,
maneno yake ni laini kuliko mafuta;
4lakini hatimaye ni mchungu kama pakanga,
ni mkali kama upanga wenye makali kuwili.
5Nyayo zake zaelekea chini mautini,
hatua zake zaenda kuzimu.#5:5 Kuzimu: Yaani makao ya wafu, mahali ndani ya dunia ambapo ilifikiriwa kwamba roho za watu waliokufa zilikwenda humo (Yobu 30:23; Zab 139:7-8; Eze 31:16-18; Mat 2:27). Katika 15:11 jina Kuzimu linatumiwa pamoja na jina Abadoni kutaja mahali hapo hapo pa wafu ingawa la pili linagusia mahali pa uharibifu.
6Yeye haijali njia ya uhai,
njia zake ni za kutangatanga, wala hajui.
7Sasa enyi wanangu, nisikilizeni,
wala msisahau maneno ya kinywa changu.
8Iepushe njia yako mbali naye,
wala usiukaribie mlango wa nyumba yake.
9Usije ukawapa wengine heshima yako,
na wakatili miaka yako;
10wageni wasije wakajishibisha kwa mali yako,
na jasho lako likaishia nyumbani kwa mgeni.
11Mwishoni mwa maisha yako utaomboleza
wakati mwili wako utakapoangamizwa.
12Hapo utasema, “Jinsi gani nilivyochukia nidhamu,
na kudharau maonyo moyoni mwangu!
13Sikuisikiliza sauti ya waalimu wangu,
wala kuwategea sikio wakufunzi wangu.
14Sasa niko karibu kuangamia kabisa
mbali na jumuiya ya watu.”
15Mkeo ni kama kisima cha maji safi:
Kunywa maji ya kisima chako mwenyewe.#5:15-18 Kunywa maji ya kisima chako mwenyewe: Aya hizi zinatilia mkazo jambo la uaminifu katika ndoa na mwanamethali anatumia methali hiyo hapo juu kusisitiza hilo. Hapo kale, hasa katika mazingira ya uhaba wa maji nyikani, kuchota maji kutoka kisima cha mtu mwingine ilikuwa kosa kubwa la jinai. Kuhusu uaminifu huo wa ndoa taz pia Lawi 20:10; Kumb 22:22-27.
16Ya nini chemchemi zako zitawanywe mbali,
na vijito vya maji barabarani?
17Hiyo ni yako wewe mwenyewe,
wala usiwashirikishe watu wengine.
18Chemchemi yako na ibarikiwe,
umfurahie mke uliyemwoa ukiwa kijana.
19Ni mzuri kama ayala, apendeza kama paa.
Mahaba yake yakufurahishe kila wakati,
umezwe daima na pendo lake.
20Mwanangu, ya nini kutekwa na mwanamke mwasherati?
Ya nini kumkumbatia kifuani mwanamke mgeni?
21Kumbuka njia za mtu zi wazi mbele ya Mwenyezi-Mungu;
yeye anaona kila hatua anayochukua binadamu.
22Mtu mwovu hunaswa kwa uovu wake mwenyewe;
hukamatwa katika tanzi za dhambi yake mwenyewe.#5:22 Mtu mwovu hunaswa kwa uovu wake …katika … dhambi yake mwenyewe: Taz 1:17-18.
23Yeye hufa kwa utovu wa nidhamu,
huangamia kwa sababu ya upuuzi wake mkuu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza