Methali 7
BHNTLK

Methali 7

7
1Mwanangu, yashike maneno yangu,
zihifadhi kwako amri zangu.
2Zifuate amri zangu nawe utaishi;
yalinde mafundisho yangu kama mboni ya jicho lako.
3Yafunge vidoleni mwako;
yaandike moyoni mwako.#7:3 Yafunge vidoleni mwako; yaandike moyoni mwako: Taz 1:8-9 maelezo.
4Iambie Hekima: “Wewe ni dada yangu”,
na Busara “Wewe ni rafiki yangu”.
5Vitakulinda mbali na mwanamke mbaya,
vitakuepusha na maneno matamu ya mwanamke mgeni.
Mwanamke mwasherati
6Siku moja dirishani mwa nyumba yangu,
nilichungulia nje kupitia viunzi vya dirisha,
7nikawaona vijana wengi wajinga,
na mmoja hasa aliyekuwa mpumbavu.
8Huyo alikuwa akitembea kwenye barabara ile,
karibu na kona alikoishi mwanamke fulani.
Basi akashika njia iendayo nyumbani kwa mwanamke huyo.
9Ilikuwa yapata wakati wa jioni,
giza na usiku vilikuwa vimeanza kuingia.
10Punde kijana akakutana na huyo mwanamke;
amevalia kama malaya, ana mipango yake.
11Alikuwa mwanamke wa makelele na mkaidi;
miguu yake haitulii nyumbani:
12mara barabarani, mara sokoni,
katika kila kona ya njia hakosekani akivizia.
13Alimkumbatia kijana huyo na kumbusu,
na kwa maneno matamu, akamwambia:
14“Ilinilazimu kutoa tambiko zangu;
leo hii nimekamilisha nadhiri#7:14 Tambiko zangu …nimekamilisha nadhiri: Hapa huenda yahusu tambiko na nadhiri zilizofanywa kwa heshima ya miungu ya rutuba ya Kanaani. Mtu aliyetambika tambiko ya amani kama hapa, au tambiko ya upatanisho alipokea sehemu ya kafara hiyo ale pamoja na jamaa zake. Kwa maneno haya huyo mwanamke anataka kumwambia huyo mtu kwamba anacho chakula kwa wingi. yangu.
15Ndio maana nimetoka ili nikulaki,
nimekutafuta kwa hamu nikakupata.
16Nimetandika kitanda changu vizuri,
kwa shuka za rangi za kitani kutoka Misri.
17Nimekitia manukato, manemane, udi na mdalasini.#7:17 Manukato, manemane, udi na mdalasini: Katika Zab 45:8 na Wimbo 4:14 viungo hivi vinatajwa pia katika mazingira ya mapenzi kati ya mwanamume na mwanamke.
18Njoo tulale pamoja mpaka asubuhi;
njoo tujifurahishe kwa mahaba.
19Mume wangu hayumo nyumbani,
amekwenda safari ya mbali.
20Amechukua bunda la fedha;
hatarejea nyumbani karibuni.”
21Alimshawishi kwa maneno mengi ya kubembeleza;
kijana akashawishika kwa maneno yake matamu.
22Hapo akamfuata huyo mwanamke moja kwa moja,
kama ng'ombe aendaye machinjioni,
kama paa arukiaye mtegoni.
23Hakutambua kwamba hiyo itamgharimu maisha yake,
mpaka alipojikuta amekuwa kama amechomwa mshale moyoni,
amekuwa kama ndege aliyenaswa wavuni.
24Sasa wanangu, nisikilizeni;
yategeeni sikio maneno ya kinywa changu.
25Msikubali kuongozwa na mwanamke kama huyo,
wala msipitepite katika mapito yake.
26Maana amewaangusha wanaume wengi;
ni wengi mno hao aliowachinja.
27Nyumba yake ni njia ya kwenda kuzimu,
ni mahali pa kuteremkia mautini.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza