9
Hekima na upumbavu#9:1-18 Katika sura hii kuna uwezekano kwamba maandishi ya istiara yanahusika: 9:1-12 Mwaliko wa Hekima; 9:13-18 Mwaliko wa mwanamke mpumbavu. Ya kwanza ni nyumbani kwa “uhai” (9:6); ya pili ni nyumbani kwa “kifo” (9:8).
1Hekima amejenga nyumba yake,
nyumba yenye nguzo saba.#9:1 Nyumba yenye nguzo saba: Maana ya “nyumba yenye nguzo saba” si dhahiri. Hizo nguzo au minara saba huenda zinahusu misingi au minara ambayo Mwenyezi-Mungu alijenga wakati wa kuumba ulimwengu (taz 8:29-30) au, yahusu idadi saba ambayo hutumika mara kwa mara katika Biblia kama mfano wa ukamilifu, na hivyo kuwa na maana hapa kwamba nyumba ya Hekima ni kamilifu kabisa.
2Amechinja wanyama wa karamu,
divai yake ameitayarisha,
ametandika meza yake.#9:2 Karamu ya Hekima huleta uhai na nguvu ya kuishi vizuri.
3Amewatuma watumishi wake wa kike mjini,
waite watu kutoka kwenye vilele vya miinuko:
4“Yeyote aliye mjinga na aje hapa!”
Na yeyote aliye mpumbavu humwambia:
5“Njoo ukale chakula,
na unywe divai niliyotengeneza.
6Achana na ujinga upate kuishi;
fuata njia ya akili.”
7Anayemkosoa mwenye dharau hupata matusi,
amkaripiaye mwovu huishia kwa kuumizwa.
8Usimwonye mwenye dharau maana atakuchukia;
mwonye mwenye hekima naye atakupenda.
9Mfunze mwenye hekima naye atazidi kuwa na hekima;
mfundishe mwadilifu naye atazidi kuelimika.
10Kumcha Mwenyezi-Mungu ni msingi wa hekima;#9:10 Kumcha Mwenyezi-Mungu …msingi wa hekima: Taz 1:7 maelezo; rejea pia Yobu 28:28; Zab 111:10.
na kumjua yule Mtakatifu ni kupata akili.
11Kwa msaada wangu mimi Hekima siku zako zitaongezwa;
utaongezewa miaka mingi maishani mwako.
12Kama una hekima, itakufaa wewe mwenyewe;
kama ukiidharau, mwenyewe utapata hasara.
13Mwanamke mpumbavu#9:13 Mwanamke mpumbavu: Picha iliyo hapa ni kinyume cha ile ya Hekima na maneno “mwanamke mpumbavu” yamkini yanatumika kuupa upumbavu hadhi ya nafsi inayopinga kazi ya Hekima. Mwaliko wake unajumuisha kila namna ya mwenendo wa kipumbavu ambao mwisho wake ni kuwaongoza wahusika katika kifo (9:18). ana kelele,
hajui kitu wala hana haya.
14Hukaa kitako mlangoni mwa nyumba yake,
huweka kiti chake mahali pa juu mjini,
15na kuwaita watu wapitao njiani,
watu wanaokwenda kwenye shughuli zao:
16“Yeyote aliye mjinga na aje hapa!”
Na yeyote aliye mpumbavu humwambia:
17“Maji ya wizi ni matamu#9:17 Maji ya wizi ni matamu: Maneno ambayo yamkini yanatumika kimfano kuashiria kitendo cha kujamiiana kusiko halali. Matumizi ya maji kwa maana hiyohiyo ni katika 5:15. Katika mstari wa pili “mkate wa wizi” si dhahiri; wengine huona hapa kwamba mstari huo unatilia mkazo mstari wa kwanza; lakini wengine wanafikiri maana ya mkate wa wizi ni ya jumla na ni onyo kwa vijana wanaotaka kutajirika haraka haraka kwa njia zisizo halali (1:11; 4:14-17). sana;
mkate unaoliwa kwa siri ni mzuri sana.”
18Lakini mjinga hajui kwamba humo mna wafu,
wageni wa mwanamke huyo wamo chini Kuzimu.