126
Kuomba nguvu mpya#126 Mazingira ya Zaburi hii ni yale ya wakati mara baada ya kurudi kutoka uhamishoni Babuloni. Zaburi yenyewe ina sehemu mbili: Ya kwanza (126:1-3) watu wanakumbuka Mungu alivyowaokoa wakati mmoja; na ya pili (126:4-6) wanamwomba afanye vivyo hivyo hata wakati huo.
(Wimbo wa Kwenda Juu)
1Mwenyezi-Mungu alipoturekebisha na kuturudisha Siyoni,#126:1 Alipoturekebisha na kuturudisha Siyoni: Maneno haya aghalabu yahusu Waisraeli waliporudi kutoka uhamishoni kule Babuloni.
tulikuwa kama watu wanaoota ndoto!
2Hapo tuliangua kicheko;
tulishangilia kwa furaha.
Nao watu wa mataifa mengine walisema:
“Mwenyezi-Mungu amewatendea mambo makubwa!”
3Kweli Mwenyezi-Mungu alitutendea mambo makubwa,
tulifurahi kwelikweli!
4Ee Mwenyezi-Mungu, urekebishe tena hali yetu,
kama mvua inavyotiririsha maji katika mabonde makavu.
5Wanaopanda kwa machozi,
watavuna kwa shangwe.
6Wanaokwenda kupanda mbegu wakilia,
watarudi kwa furaha wakichukua mavuno.#126:6 Maneno mwafaka kabisa ambayo kwa picha kamili yanaonesha jinsi watu wa Mungu walivyo na matumaini hata wakati wa magumu ya maisha.