Zaburi 132
BHNTLK

Zaburi 132

132
Sifa ya nyumba ya Mungu
(Wimbo wa Kwenda Juu)
1Ee Mwenyezi-Mungu, mkumbuke Daudi,
kumbuka taabu zote alizopata.
2Ukumbuke ahadi aliyokupa,#132:1-2 Mkumbuke …taabu zote alizopata … ahadi aliyokupa: Neno “kumbuka” hapa ni namna ya kusema Mungu akumbuke na kuchukua hatua ipasayo kutokana na kumbukumbu hiyo. ee Mwenyezi-Mungu,
kiapo alichokuapia, ewe Mwenye Nguvu wa Yakobo:#132:2 Mwenye Nguvu wa Yakobo: “Mwenye Nguvu” ni jina la sifa la Mungu (taz majina ya Mungu katika Kutoka 3). “Mwenye Nguvu wa Yakobo” maana yake ni Mwenye Nguvu ambaye Yakobo (babu wa Waisraeli) alimwabudu.
3“Sitaingia ndani ya nyumba yangu,
wala kulala kitandani mwangu;#132:3-5 Kuhusu nia ya Daudi ya kumjengea Mungu nyumba taz 2Sam 7:1-3; Mat 7:46.
4sitakubali kulala usingizi,
wala kusinzia;
5mpaka nikupatie wewe Mwenyezi-Mungu mahali pa kukaa,
makao yako, ewe Mwenye Nguvu wa Yakobo!”
6Huko Efratha tulisikia habari za sanduku la agano,
tukalikuta katika mashamba ya Yearimu.#132:6 Efratha …Yearimu: Efratha labda ni eneo karibu na Bethlehemu na Yearimu ni jina lingine la Kiriath-yearimu mahali ambapo lile sanduku la agano lilirudishwa baada ya kutekwa na Wafilisti (1Sam 6:1—7:2).
7“Haya! Twende nyumbani kwa Mungu,
tuabudu mbele ya kiti chake cha enzi!”
8Inuka ee Mwenyezi-Mungu, nenda kwenye maskani yako;
inuka pamoja na sanduku la agano la uwezo wako!
9Makuhani wako wawe waadilifu daima;
na waaminifu wako wapige vigelegele vya furaha!
10Kwa ajili ya Daudi, mtumishi wako,
usimkatae huyo mfalme uliyemweka wakfu.
11Mwenyezi-Mungu alimwapia Daudi kiapo thabiti,
kiapo ambacho hatakibatilisha:
“Nitamtawaza mmoja wa wazawa wako mwenyewe,
kuwa mfalme baada yako.
12Watoto wako wakishika agano langu,
na kuzingatia mafundisho nitakayowapa,
watoto wao pia watakuwa wafalme kama wewe.”
13Mwenyezi-Mungu ameuchagua mji wa Siyoni,
ametaka uwe makao yake:
14“Hapa ndipo nitakapokaa milele,
ndipo maskani yangu maana nimepachagua.
15Nitaubariki sana mji wa Siyoni kwa mahitaji yake;
nitawashibisha chakula maskini wake.
16Nitawafanikisha makuhani wake kwa wokovu;
waaminifu wake watapiga vigelegele vya furaha.
17Humo nitamchipusha mfalme shujaa wa ukoo wa Daudi:
kama taa iwakayo nitamtegemeza mfalme niliyemteua.
18Maadui zake nitawavika aibu;
lakini yeye nitamvika fahari ya kifalme.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza