Zaburi 135
BHNTLK

Zaburi 135

135
Sifa kwa Mungu#135 Zaburi hii ni utenzi ulio na lengo la kumsifu na kumtangaza Mwenyezi-Mungu kama mkuu wa miungu yote, Bwana wa ulimwengu wote na Mwokozi wa watu wake.
1Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Lisifuni jina la Mwenyezi-Mungu,
msifuni enyi watumishi wake.
2Msifuni enyi mkaao katika nyumba yake,#135:2 Mkaao katika nyumba yake: Hapa si dhahiri kwamba hao wakaao katika nyumba yake ni wahudumu wa hekalu (yaani makuhani na Walawi) au wanaomwabudu Mungu wakati huo.
ukumbini mwa nyumba ya Mungu wetu!
3Msifuni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema;
mtukuzeni kwa nyimbo maana inafaa.#135:3 Maana inafaa: Au: “maana ni mwema”.
4Mwenyezi-Mungu amemchagua Yakobo#135:4 Yakobo: Ingawa Yakobo ni jina la babu wa Waisraeli hapa linatumika kwa maana ya Waisraeli wenyewe (mstari wa 2). kuwa wake,
nyinyi watu wa Israeli kuwa mali yake mwenyewe.
5Najua hakika kuwa Mwenyezi-Mungu ni mkuu;
Bwana wetu ni mkuu juu ya miungu yote.
6Mwenyezi-Mungu hufanya chochote anachotaka,
mbinguni, duniani, baharini na vilindini.#135:6 Vilindini: Neno hili linatumika kutaja bahari pana mno ambayo ilifikiriwa kuwa chini ya dunia (24:2).
7Ndiye aletaye mawingu kutoka mipaka ya dunia;
afanyaye gharika kuu kwa umeme,
na kuvumisha upepo kutoka ghala zake.
8Ndiye aliyewaua wazaliwa wa kwanza huko Misri,
wazaliwa wa watu na wanyama kadhalika.
9Ndiye aliyefanya ishara na maajabu#135:9 Ishara na maajabu: Yaani mapigo ambayo Mungu aliwaadhibu nayo Wamisri (Kut 7:14—10:29). kwako, ee Misri,
dhidi ya Farao na maofisa wake wote.
10Ndiye aliyeyaangamiza mataifa mengi,
akawaua wafalme wenye nguvu:
11kina Sihoni mfalme wa Waamori,
Ogu mfalme wa Bashani,#135:11 Sihoni …Ogu mfalme wa Bashani: Sihoni hakupenda Waisraeli wapite katika nchi yake (Hes 21:21-33; Kumb 2:26-37). Na kuhusu Ogu, (taz Hes 21:33-35; Kumb 3:1-6).
na wafalme wote wa Kanaani.
12Alichukua nchi zao na kuwapa watu wake;
naam, ziwe riziki ya watu wake Israeli.
13Jina lako, ee Mwenyezi-Mungu, ladumu milele,
utakumbukwa kwa fahari nyakati zote.
14Mwenyezi-Mungu atawatetea watu wake;
na kuwaonea huruma watumishi wake.
15Miungu ya uongo ya mataifa ni fedha na dhahabu,
imetengenezwa kwa mikono ya binadamu.
16Ina vinywa, lakini haisemi;
ina macho, lakini haioni.
17Ina masikio, lakini haisikii;
wala haiwezi hata kuvuta pumzi.
18Wote walioifanya wafanane nayo,
naam, kila mmoja anayeitegemea!
19Enyi watu wa Israeli, mtukuzeni Mwenyezi-Mungu!
Enyi makuhani, mtukuzeni Mwenyezi-Mungu!
20Enyi Walawi, mtukuzeni Mwenyezi-Mungu!
Enyi wachaji wa Mwenyezi-Mungu, mtukuzeni!
21Atukuzwe Mwenyezi-Mungu katika Siyoni,
atukuzwe katika makao yake Yerusalemu.
Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza