Zaburi 136
BHNTLK

Zaburi 136

136
Wimbo wa shukrani#136 Zaburi hii ni utenzi wa kumsifu Mwenyezi-Mungu muumba wa ulimwengu, mwokozi na mlinzi wa watu wake.
1Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema;
kwa maana fadhili zake zadumu milele.#136:1 1 Nya 16:34; 2Nya 5:11-13; Ezra 3:11; Zab 100:5; 106:1; 107:1; 118:1; Yer 33:11. Fungu la maneno linalorudiwa (kwa maana fadhili zadumu milele) huenda yalikuwa majibu ya watu wakati zaburi hiyo ilipoimbwa katika ibada.
2Mshukuruni Mungu wa miungu;
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
3Mshukuruni Bwana wa mabwana;
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
4Ndiye peke yake atendaye makuu ya ajabu;#136:4 Makuu ya ajabu: Au, “miujiza mikubwa”.
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
5Ndiye aliyeziumba mbingu kwa hekima;
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
6Ndiye aliyeitengeneza nchi juu ya vilindi vya maji;
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
7Ndiye aliyeumba jua, mwezi na nyota;
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
8Jua liutawale mchana;
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
9Mwezi na nyota vitawale usiku;#136:5-9 Aliyeziumba mbingu kwa hekima …nyota vitawale usiku: Kuhusu hekima ya Mungu na kuumbwa ulimwengu taz Meth 3:19-20; 8:22-31; Yer 10:12.
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
10Ndiye aliyewaua wazaliwa wa kwanza wa Misri;
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
11Akawaondoa watu wa Israeli kutoka huko;
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
12Kwa mkono wake wenye nguvu na enzi;
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
13Ndiye aliyeigawa Bahari ya Shamu sehemu mbili;
kwa maana fadhili zake zadumu milele,
14akawapitisha watu wa Israeli humo;
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
15Lakini akawazamisha#136:10-15 Aliyewaua …akawazamisha: Mwanazaburi anakumbuka jinsi Mungu alivyowaokoa Waisraeli kutoka Misri na kuwaongoza salama kupita Bahari ya Shamu (Kut 12:29-42; 51:14). humo Farao na jeshi lake;
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
16Ndiye aliyewaongoza watu wake jangwani;
kwa maana fadhili zake zadumu milele.#136:16-22 Mwanazaburi anataja mambo yaliyotokea muda wa miaka 40 kule jangwani hadi kuinyakua nchi ya Kanaani.
17Ndiye aliyewapiga wafalme wenye nguvu;
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
18Akawaua wafalme maarufu;
kwa maana fadhili zake zadumu milele;
19akamuua Sihoni, mfalme wa Waamori,
kwa maana fadhili zake zadumu milele;
20na Ogu, mfalme wa Bashani;
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
21Akachukua nchi zao akawapa watu wake;
kwa maana fadhili zake zadumu milele;
22ziwe riziki ya Israeli, mtumishi wake;
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
23Ndiye aliyetukumbuka wakati wa unyonge wetu;
kwa maana fadhili zake zadumu milele;
24akatuokoa kutoka maadui zetu;#136:24 Akatuokoa kutoka maadui zetu: Maadui hapa wanaweza kuwa Wamisri ikiwa kuokolewa huko ni kutoka Misri; la sivyo ni kuokolewa kutoka uhamishoni Babuloni, tukio ambalo lilichukuliwa pia kama hali mpya ya “Kutoka” (137:1-3).
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
25Ndiye akipaye kila kiumbe chenye uhai chakula;
kwa maana fadhili zake zadumu milele.
26Mshukuruni Mungu wa mbinguni;
kwa maana fadhili zake zadumu milele!

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza