Zaburi 137
BHNTLK

Zaburi 137

137
Ombolezo ugenini#137 Mwanazaburi anaomboleza maafa yaliyowapata watu wake uhamishoni kule Babuloni. Si dhahiri kama mwandishi alikuwa bado huko uhamishoni wakati wa kutunga utenzi huu au ilikuwa baada ya mfalme Koreshi wa Persia kuwaruhusu Waisraeli warudi makwao (mwaka 538 K.K.).
1Kando ya mito ya Babuloni,#137:1 Mito ya Babuloni: Yaani mifereji na vijito vya mito ya Tigri na Eufrate. tulikaa,
tukawa tunalia tulipokumbuka Siyoni.
2Katika miti ya nchi ile,
tulitundika zeze zetu.
3Waliotuteka walitutaka tuwaimbie;
watesi wetu#137:3 Watesi wetu: Neno la Kiebrania lililotafsiriwa hapa kama “watesi” linatumika mara moja tu katika A.K. na wafafanuzi wa Maandiko hawaafikiani kuhusu maana yake. walitutaka tuwafurahishe:
“Tuimbieni mojawapo ya nyimbo za Siyoni!”#137:3 Nyimbo za Siyoni: Maana yake hapa ni au, “nyimbo kuhusu Siyoni” au nyimbo walizoimba kule Yerusalemu au katika hekalu. Maana hii ya mwisho ina uzito zaidi na swali litakalofuata (aya 4) linaeleweka zaidi kufuatana na maana hii.
4Twawezaje kuimba wimbo wa Mwenyezi-Mungu
katika nchi ya kigeni?
5Ee Yerusalemu, kama nikikusahau,
mkono wangu wa kulia na ukauke!
6Ulimi wangu na uwe mzito,
kama nisipokukumbuka wewe, ee Yerusalemu;
naam, nisipokuthamini kuliko furaha yangu kubwa!
7Ee Mwenyezi-Mungu, usisahau waliyotenda Waedomu,#137:7 Waliyotenda Waedomu: Huenda Waedomu walifurahi wakati mji wa Yerusalemu ulipoteketezwa na Wababuloni na wengi wa wakazi wake wakachukuliwa mateka. Taz Eze 35:5-15; Oba 10-14.
siku ile Yerusalemu ilipotekwa;
kumbuka waliyosema:
“Bomoeni mji wa Yerusalemu!
Ng'oeni hata na misingi yake!”
8Ee Babuloni, utaangamizwa!
Heri yule atakayekulipiza mabaya uliyotutenda!#137:8-9 Ufu 18:6. Kilio hiki cha kutatanisha cha kulipiza kisasi kilikuwa kawaida nyakati zile: jicho kwa jicho, jino kwa jino, jambo ambalo ilibidi A.J. litamke vingine kwa mafundisho yake Yesu Kristo juu ya upendo (Mat 5:38-48).
9Heri yule atakayewatwaa watoto wako
na kuwapondaponda mwambani!

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza