Zaburi 138
BHNTLK

Zaburi 138

138
Sala ya shukrani#138 Zaburi hii ya sifa kwa Mungu inaanza na tamko la sifa na shukrani (aya 1-3) kisha Mwanazaburi anatangaza kwamba wafalme wote duniani nao pia watamsifu Mwenyezi-Mungu (aya 4-6) na mwishowe Mwanazaburi anamalizia kwa tamko la tegemeo katika ulinzi wa Mungu (aya 7-8).
1Nakushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, kwa moyo wangu wote,
naimba sifa zako mbele ya miungu.#138:1 miungu: Hapa kuna tatizo kubwa la ufafanuzi maana swali ni kwamba Mwanazaburi atamshukuru Mungu mbele ya miungu kwa maana gani? Labda yahusu “miungu ya uongo” kusudi iaibike. Maelezo yamkini kuliko yote ni kufikiri kwamba Mungu ameketi katika kiti chake cha enzi mbinguni kama Mungu Mkuu akizungukwa na miungu - malaika (taz 29:1; 82:1; 97:7). Tafsiri za kale kama vile Septuajinta na Vulgata kwa kweli zina “malaika”. Tafsiri ya kale ya Kisiria ina “wafalme”.
2Ninasujudu kuelekea hekalu lako#138:2 Kuelekea hekalu lako: Ishara inayoashiria kwamba Mwanazaburi yuko, kwa uchache sana, nje ya mji wa Yerusalemu lilipo hekalu. takatifu;
nalisifu jina lako,
kwa sababu ya fadhili zako na uaminifu wako;
kwa sababu umeweka jina lako na neno lako
juu ya kila kitu.#138:2 Umeweka jina lako na neno lako juu ya kila kitu: Makala ngumu ya Kiebrania ambamo inasemwa neno kwa neno: “amri yako ni kubwa kuliko jina lako lote”.
3Nilipokulilia, wewe ulinijibu;
umeniongezea nguvu zangu.
4Wafalme wote duniani watakusifu, ee Mwenyezi-Mungu,
kwa sababu wameyasikia maneno yako.
5Wataimba sifa za matendo yako, ee Mwenyezi-Mungu,
kwa maana utukufu wako ni mkuu.
6Ingawa wewe ee Mwenyezi-Mungu, uko juu ya wote,
unawaangalia kwa wema walio wanyonge;
nao wenye kiburi huwaona kutoka mbali.
7Hata nikikumbana na taabu, wewe wanilinda;
waunyosha mkono wako dhidi ya hasira ya maadui zangu wakali;
kwa nguvu yako kuu wanisalimisha.
8Ee Mwenyezi-Mungu, utatimiza yote uliyoniahidi.
Fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, zadumu milele.
Usisahau kazi ya mkono wako mwenyewe.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza