Zaburi 139
BHNTLK

Zaburi 139

139
Mungu ajua yote, aongoza yote
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi)
1Ee Mwenyezi-Mungu, wewe umenichunguza;
wewe wanijua mpaka ndani.
2Nikiketi au nikisimama,#139:2-3 Nikiketi au nikisimama: Taz pia “nikienda au nikipumzika” katika aya 3. Namna hii ya kusema ina shabaha ya kusisitiza kwa picha kwamba Mungu anajua kila kitu binadamu anachofakinya, hata mawazo yake. wewe wajua;
wajua kutoka mbali kila kitu ninachofikiria.
3Watambua nikienda au nikipumzika;
wewe wazijua shughuli zangu zote.
4Kabla sijasema neno lolote,
wewe, ee Mwenyezi-Mungu, walijua kabisa.
5Uko kila upande wangu,#139:5 Uko kila upande wangu: Yaani, kuchunga na kulinda. mbele na nyuma;
waniwekea mkono wako kunilinda.
6Maarifa yako yapita akili yangu;
ni makuu mno, siwezi kuyaelewa.
7Nikimbilie wapi ambako roho yako haiko?
Niende wapi ambako wewe huko?
8Nikipanda juu mbinguni, wewe upo;
nikijilaza chini kuzimu,#139:8 Mbinguni …kuzimu: Mwanazaburi anataja mahali pawili ambapo ni sehemu za mbali zaidi kuliko nyingine ulimwenguni ili kutamka dhahiri kwamba hakuna mahali anapoweza kwenda bila kulindwa na kuchungwa na Mungu. wewe upo.
9Nikiruka hadi mawio ya jua,
au hata mipakani mwa bahari,
10hata huko upo kuniongoza;
mkono wako wa kulia utanitegemeza.
11Kama ningeliomba giza linifunike,
giza linizunguke badala ya mwanga,
12kwako giza si giza hata kidogo,
na usiku wang'aa kama mchana;
kwako giza na mwanga ni mamoja.
13Wewe umeniumba, mwili wangu wote;
ulinitengeneza tumboni mwa mama yangu.
14Nakusifu maana nimefanywa kwa namna ya ajabu,
matendo yako ni ya ajabu;
wewe wanijua kabisakabisa.
15Umbo langu halikufichika kwako
nilipotungwa kwa siri na ustadi ndani ya dunia.#139:15 Nilipotungwa …mbali ndani ya dunia: Au, kama Mwanazaburi alikuwa anatumia maneno hayo kama mfano kutaja “tumbo la uzazi la mama”. Inawezekana pia kwamba namna hiyo ya kusema ni mtindo wa kishairi wa kueleza juu ya Mungu kama mwenye kutunga au kufuma.
16Wewe uliniona hata kabla sijazaliwa,
uliandika kila kitu kitabuni#139:16 Uliandika …kitabuni: Taz 40:7 maelezo. mwako;
siku zangu zote ulizipanga,
hata kabla ya kuweko ile ya kwanza.
17Ee Mungu, mawazo yako ni makuu mno;
hayawezi kabisa kuhesabika.
18Ningeyahesabu yangekuwa mengi kuliko mchanga.
Niamkapo, bado nipo pamoja nawe.#139:18 Niamkapo …nipo pamoja nawe: Tafsiri yamkini ya Kiebrania kigumu. Wengine wanatafsiri mstari huu wa pili wa aya hii kama kulingana na hati za mkono chache za kale ambapo badala ya “niamkapo” kuna kitenzi ambacho chaweza kutafsiriwa kama “nikimaliza” au “nikifika mwisho”.
19Laiti, ee Mungu, ungewaua watu waovu!
Laiti watu wauaji wangeondoka kwangu!#139:19-20 Mwanazaburi hapa anakuwa kama amekosa kuwa mvumilivu lakini sala yake ni sala inayoonesha uaminifu na tegemeo lake kwa Mungu na katika aya 20-22 maadui wa Mungu ni maadui wake pia.
20Wanasema vibaya juu yako;
wanasema maovu juu ya jina lako!
21Ee Mwenyezi-Mungu, nawachukia wanaokuchukia;
nawadharau sana wale wanaokuasi!
22Maadui zako ni maadui zangu;
ninawachukia kabisakabisa.
23Unichunguze, ee Mungu, unijue moyo wangu,
unipime, uyajue mawazo yangu.
24Uangalie kama mwenendo wangu ni mbaya,
uniongoze katika njia ya milele.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza