140
Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi)
1Ee Mwenyezi-Mungu, uniokoe na watu wabaya,
unikinge na watu wakatili.
2Watu hao huwaza mabaya daima,
huzusha magomvi kila mara.
3Ndimi zao hatari kama za nyoka;
midomoni mwao mna maneno ya sumu kama ya joka.#140:3 Ndimi …joka: Hapa Mwanazaburi huenda anagusia maneno ya kusengenya ya hao watu au laana walizotoa dhidi yake. Mstari wa pili; “sumu kama ya joka” yamenukuliwa katika Rom 3:13.
4Ee Mwenyezi-Mungu, unilinde na makucha ya wabaya;
unikinge na watu wakatili
ambao wamepanga kuniangusha.#140:1-4 Watu wabaya …wakatili ambao wamepanga kuniangusha: Watu hao wanaitwa pia wenye kiburi (aya 5), wanaowasengenya wengine (aya 11).
5Wenye kiburi wamenitegea mitego,
wametandaza kamba kama wavu,
wameficha mitego njiani wanikamate.
6Namwambia Mwenyezi-Mungu, “Wewe ndiwe Mungu wangu.”
Usikilize, ee Mwenyezi-Mungu, sauti ya ombi langu.
7Ee Mwenyezi-Mungu, Bwana wangu, mkombozi wangu mkuu,
umenikinga salama wakati wa vita.
8Ee Mwenyezi-Mungu, usiwape waovu wanayotaka;
wala mipango yao mibaya usiifanikishe.
9Hao wanaonizingira wanainua vichwa;
uovu wa maneno yao uwapate wao wenyewe!
10Makaa ya moto yawaangukie;#140:10 Makaa ya moto yawaangukie: Mara nyingi katika Biblia adhabu ya Mungu inaandamana na moto kama vile katika ile adhabu ya watu wa Sodoma na Gomora (Mwa 19).
watumbukizwe mashimoni, wasiinuke tena.
11Wanaowasengenya wengine wasifanikiwe katika nchi;
uovu uwapate wakatili na kuwaangamiza mara!
12Najua Mwenyezi-Mungu hutetea kisa cha wanaoteswa,
na kuwapatia haki maskini.
13Hakika waadilifu watalisifu jina lako;
wanyofu watakaa kwako.