142
Dua ya mtu aliyeachwa mpweke
(Utenzi wa Daudi alipokuwa pangoni. Sala)#142 Utenzi wa Daudi alipokuwa pangoni Sala: Tamko hili linalohusisha historia huenda linagusia kile kisa kinachoelezwa katika 1Sam 22:1-2 (taz pia anwani kwa Zab 57).
1Namlilia Mwenyezi-Mungu kwa sauti,
namsihi Mwenyezi-Mungu kwa sauti yangu.
2Namwekea malalamiko yangu,
namweleza taabu zangu.
3Ninapokaribia kukata tamaa kabisa,
yeye yupo, anajua mwenendo wangu.
Maadui wamenitegea mitego njiani mwangu.
4Nikiangalia upande wa kulia na kungojea,
naona hakuna mtu wa kunisaidia;
sina tena mahali pa kukimbilia,
hakuna mtu anayenijali.
5Nakulilia wewe, ee Mwenyezi-Mungu!
Wewe ni kimbilio langu la usalama;
wewe ni riziki yangu kuu katika nchi ya walio hai.#142:5 Riziki yangu kuu katika nchi ya walio hai: Maneno “riziki yangu kuu” yanajaribu kutafsiri kile ambacho katika Kiebrania ni “sehemu ya pekee anayopewa mtu kama mali yake yenye thamani kubwa.” Rejea 16:5 maelezo. Na kuhusu “nchi ya walio hai” yamkini Mwanazaburi alitaka kusema “katika maisha haya” au, “hapa duniani”.
6Usikilize kilio changu, maana nimekuwa hoi;
uniokoe na watesi wangu, maana wamenizidi nguvu.
7Unitoe humu kifungoni,#142:7 Kifungoni: Kama hapa si kifungoni kweli basi huenda Mwanazaburi alikuwa anagusia hali ya shida kabisa.
ili nipate kukushukuru.
Watu waadilifu watajiunga nami
kwa sababu umenitendea mema mengi.