Zaburi 144
BHNTLK

Zaburi 144

144
Shukrani kwa ushindi
(Zaburi ya Daudi)
1Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, mwamba wangu,
anayeipa mikono yangu mazoezi ya vita,
na kuvifunza vidole vyangu kupigana.
2Yeye ni rafiki yangu amini na ngome yangu,
kinga yangu na mkombozi wangu;
yeye ni ngao yangu,#144:1-2 Mwenyezi-Mungu mwamba wangu …ngao yangu: Mwanazaburi anatumia maneno hayo kama mfano wa nguvu kuu (mwamba) na uwezo wake Mungu wa kulinda (ngao). kwake napata usalama;
huyashinda mataifa na kuyaweka chini yangu.
3Ee Mwenyezi-Mungu, mtu ni nini hata umjali?#144:3 Mtu ni nini hata umjali?: Aya hii inakumbusha Zab 8. Taz pia Yobu 7:17-18.
Mwanadamu ni nini hata umfikirie?
4Binadamu ni kama pumzi tu;
siku zake ni kama kivuli kipitacho.
5Uinamishe mbingu zako, ee Mwenyezi-Mungu, ushuke chini!
Uiguse milima nayo itoe moshi!#144:5-6 Aya 5 inakumbusha Zab 18:9 na aya 6 inakumbusha Zab 18:14. Vile vile aya 7 na 8 zinakumbusha Zab 18:16-17, 43-45.
6Lipusha umeme, uwatawanye maadui;
upige mishale yako, uwakimbize!
7Unyoshe mkono wako kutoka juu,
uniokoe na kuniondoa katika maji haya mengi;
uniondoe makuchani mwa wageni,
8ambao husema maneno ya uongo,
hunyosha mkono kushuhudia uongo.
9Nitakuimbia wimbo mpya, ee Mungu;
nitakupigia kinubi cha nyuzi kumi,
10wewe uwapaye wafalme ushindi,
umwokoaye Daudi mtumishi wako!#144:10 Umwokoaye Daudi mtumishi wako: Labda hapa Mwanazaburi anafikiria pia wazawa wa Daudi ambao watatawala badala yake (Yer 33:21).
11Uniokoe na upanga wa adui katili,
uniondoe makuchani mwa wageni,
ambao husema maneno ya uongo,
hunyosha mkono kushuhudia uongo.
12Wavulana wetu wakue kikamilifu kama mimea bustanini;
binti zetu wawe kama nguzo zilizochongwa kupambia ikulu.
13Ghala zetu zijae mazao ya kila aina.
Kondoo wetu mashambani wazae maelfu kwa maelfu.
14Mifugo yetu iwe na afya na nguvu;
isitupe mimba wala kuzaa kabla ya wakati.
Kusiwepo tena udhalimu mitaani mwetu.
15Heri taifa ambalo limejaliwa hayo!
Heri taifa ambalo Mungu wao ni Mwenyezi-Mungu!

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza