Zaburi 145
BHNTLK

Zaburi 145

145
Wimbo wa kumsifu Mungu
(Wimbo wa sifa wa Daudi)
1Nitakutukuza, ee Mungu wangu na mfalme wangu;
nitalitukuza jina lako daima na milele.
2Nitakutukuza kila siku;
nitalisifu jina lako daima na milele.
3Mwenyezi-Mungu ni mkuu, astahili sifa nyingi;
ukuu wake hauwezi kuchunguzika.#145:1-3 Nitakutukuza …ukuu wake hauwezi kuchunguzika: Katika aya hizi inaonekana wazi kwamba kumsifu Mungu si shauri la ibada tupu ila hutokana na moyo wa shukrani kwa sababu ya wema na nguvu yake.
4Kizazi hata kizazi, sifa za matendo yako zitasimuliwa,
watu watatangaza matendo yako makuu.
5Nitanena juu ya utukufu na fahari yako,
nitayatafakari matendo yako ya ajabu.
6Watu watatangaza ukuu wa matendo yako ya ajabu,
nami nitatangaza ukuu wako.
7Watatangaza sifa za wema wako mwingi,
na kuimba juu ya uadilifu wako.#145:4-7 Sifa za matendo yako …wema wako … uadilifu wako: Mwanazaburi anakumbuka na kutafakari matendo makuu ya Mungu katika historia ya Waisraeli; matendo ambayo yanapaswa kutangazwa kwa kila kizazi (71:18; 78:4).
8Mwenyezi-Mungu ni mwenye huruma na rehema;
hakasiriki ovyo, amejaa fadhili.
9Mwenyezi-Mungu ni mwema kwa wote,
ni mwenye huruma kwa viumbe vyake vyote.
10Viumbe vyako vyote vitakushukuru,#145:9-10 Mwenyezi-Mungu ni mwema kwa wote …viumbe vyako vyote vitakushukuru: Taz 96:11-12 maelezo. ee Mwenyezi-Mungu,
nao waaminifu wako watakutukuza.
11Watasema juu ya utukufu wa ufalme wako,
na kutangaza juu ya nguvu yako kuu,
12ili kila mtu ajue matendo yako makuu,
na fahari tukufu ya ufalme wako.
13Ufalme wako ni ufalme wa milele;
mamlaka yako yadumu vizazi vyote.#145:11-13 Ufalme wako …mamlaka yako yadumu vizazi vyote: Neno “ufalme” linatumiwa mara tatu hapa. Ufalme wa Mungu ni pale Mungu “anapotawala” (145:13) na mahali pale ambapo matakwa na malengo au nia yake vinatekelezwa. Taz pia 98:9.
Mwenyezi-Mungu ni mwaminifu katika ahadi zake zote,
ni mwema katika matendo yake yote.
14Mwenyezi-Mungu huwategemeza wote wanaoanguka;
huwainua wote waliokandamizwa.
15Viumbe vyote vinakutazama kwa hamu,
nawe wavipa chakula chao kwa wakati wake.
16Waufumbua mkono wako kwa ukarimu,
watosheleza mahitaji ya kila kiumbe hai.#145:16 Watosheleza mahitaji ya kila kiumbe hai: Sio tu binadamu bali kila kiumbe kinamtegemea Mungu kwa uhai na kuendelea kuishi (107:27-28). Watu wanapaswa kumtumainia Mungu pia na kutegemea msaada wake wa daima (Mat 6:25-38).
17Mwenyezi-Mungu ni mwadilifu katika njia zake zote;
ni mwema#145:17 Mwenyezi-Mungu ni mwadilifu …ni mwema: Uadilifu wake Mungu na wema wake au huruma havipingani ila vyote viwili vinaungana kufanikisha maisha ya watu wote (Yak 2:13). katika matendo yake yote.
18Mwenyezi-Mungu yuko karibu na wote wanaomwomba,
wote wanaomwomba kwa moyo mnyofu.
19Huwapatia mahitaji yao wote wanaomcha;
husikia kilio chao na kuwaokoa.
20Mwenyezi-Mungu huwalinda wote wanaompenda;
lakini atawaangamiza waovu wote.
21Nitatangaza sifa za Mwenyezi-Mungu;
viumbe vyote vilisifu jina lake takatifu,
milele na milele.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza