Zaburi 146
BHNTLK

Zaburi 146

146
Sifa kwa Mungu Mwokozi#146 Zaburi 146-150 ni kufungu kinachoitwa “Zaburi za Haleluya” kwa sababu zinaanza na Kiebrania “Haleluya” maana yake “Msifuni Mwenyezi-Mungu” Taz 104:35. Baada ya kutangaza nia yake ya kumsifu Mungu (aya 1-2) Mwanazaburi anawaonya watu wake wasije kuwategemea viongozi wa kibinadamu (aya 3-4) ila waweke tegemeo lao na imani yao kwa Mungu ambaye upendo na nguvu yake vinaelezwa hasa kadiri ya ulinzi wake kwa wanyonge, maskini na waliokandamizwa na kudhulumiwa (aya 5-9).
1Msifuni Mwenyezi-Mungu!#146:1 Msifuni Mwenyezi-Mungu: Zaburi zote 146-150 huanza na kumalizia kwa mwito huo.
Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee nafsi yangu!
2Nitamsifu Mwenyezi-Mungu maisha yangu yote;
nitamwimbia Mungu wangu muda wote niishipo.
3Msiwategemee wakuu wa dunia;#146:3 Msiwategemee wakuu wa dunia: Tamko hili ni ujumbe mahsusi kabisa ambao ulitiliwa maanani na Wanazaburi (Zab 118:8-9) na manabii (Isa 2:22; 31:3; Yer 17:5). Lengo lake ni kwamba binadamu lazima aweke tegemeo lake kwa Mungu na sio kwa binadamu, mali, miungu n.k.
hao ni binadamu tu, hawawezi kuokoa.
4Binadamu akitoa pumzi yake ya mwisho,
anarudi mavumbini alimotoka;
na hapo mipango yake yote hutoweka.#146:4 Binadamu …anarudi mavumbini … hutoweka: Zab 104:29. Kifo ni ushindi wa mwisho juu ya kiburi na kujitakia kwa binadamu. Lakini kwa ushindi wake Kristo, kifo kimeshindwa (1Kor 15:54-57).
5Heri mtu anayesaidiwa na Mungu wa Yakobo,
mtu aliyeweka tumaini lake kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake,
6aliyeumba mbingu na dunia,
bahari na vyote vilivyomo.
Yeye hushika ahadi yake milele.
7Yeye huwapatia wanaoonewa haki zao,
huwapa wenye njaa chakula.
Mwenyezi-Mungu huwapa wafungwa uhuru,
8huwafungua macho vipofu.
Mwenyezi-Mungu huwainua waliokandamizwa;
huwapenda watu walio waadilifu.
9Mwenyezi-Mungu huwalinda wageni,
huwategemeza wajane na yatima;#146:7-9 Huwapatia wanaoonewa haki …wajane na yatima: Moja ya sifa ya pekee na ambayo inayomtofautisha Mungu wa kweli na miungu mingine ni kitendo chake cha kuwajali maskini, wanyonge na wanaokandamizwa. (Taz pia 9:8,9; 94:6; 102:17; 140:12).
lakini huipotosha njia ya waovu.
10Mwenyezi-Mungu atawala milele,
Mungu wako, ee Siyoni, ni mfalme vizazi vyote!
Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza