Zaburi 148
BHNTLK

Zaburi 148

148
Ulimwengu wote umsifu Mungu#148 Katika Zaburi hii ya sifa kwa Mungu Mwanazaburi anatoa mwito kwa viumbe vyote vyenye uhai na visivyo na uhai kumsifu Mwenyezi-Mungu: viumbe vyote pamoja na vile vya mbinguni (aya 1-6) na viumbe vyote na vitu duniani (aya 7-12) vitamsifu. Aya mbili za mwisho zinatoa sababu ya sifa hizo (aya 13-14): Yeye ni mkuu wa yote na amewaokoa watu wake. Zaburi inamalizia kama ilivyoanza kwa mwito: Msifuni Mwenyezi-Mungu.
1Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Msifuni Mwenyezi-Mungu kutoka mbinguni,
msifuni kutoka huko juu mbinguni.
2Msifuni, enyi malaika wake wote,
msifuni, enyi majeshi yake yote.#148:2 Majeshi yake yote: Kama inavyoonekana dhahiri katika mtindo wa kishairi mstari wa pili wa aya pili ni sambamba na mstari wa kwanza hivyo kwamba “majeshi …” na maneno mengine ya kutaja malaika.
3Msifuni, enyi jua na mwezi,
msifuni, enyi nyota zote zing'aazo.
4Msifuni, enyi mbingu za juu,
na maji yaliyo juu ya mbingu.#148:3-4 Jua na mwezi …mbingu za juu … maji yaliyo juu ya mbingu: Watu wengine wa kale na majirani wa Waisraeli waliabudu jua, mwezi na nyota kama miungu. Hapa Mwanazaburi anaviita vyote vimsifu Mwenyezi-Mungu maana hivyo vimeumbwa naye. Na kuhusu “mbingu za juu” na “maji yaliyo juu ya mbingu” ilifikiriwa kwamba anga lilikuwa ni kitu kama bakuli lililofundikizwa juu ya dunia ambayo nayo ilifikiriwa kuwa bapa au sawa. Ilifikiriwa kwamba juu ya anga hilo kulikuwa na maji (Mwa 1:6-7).
5Vyote vilisifu jina la Mwenyezi-Mungu,
maana yeye aliamuru, na vyote vikawa.
6Yeye aliviweka mahali pao daima,
kwa amri ambayo haiwezi kubatilishwa.
7Msifuni Mwenyezi-Mungu kutoka duniani;
enyi majoka ya baharini na vilindini, msifuni.#148:7-12 Aya hizi ni mwito kwa viumbe vyote duniani (pamoja na watu: watawala watoto na wazee) kumsifu Mungu. Orodha ya vitu vinavyotajwa hapa inakumbusha tena tukio la kuumbwa ulimwengu katika Mwa 1—2. Taz pia 74:13-14 kuhusu majoka ya baharini.
8Msifuni enyi moto, mvua ya mawe na theluji,
upepo wa tufani unaotimiza amri yake!
9Msifuni enyi milima na vilima,
miti ya matunda na misitu!
10Msifuni enyi wanyama wa porini na wafugwao,
viumbe vitambaavyo na ndege wote!
11Msifuni enyi wafalme na mataifa yote;
viongozi na watawala wote duniani!
12Msifuni enyi wavulana na wasichana;
wazee wote na watoto pia!
13Nyote lisifuni jina la Mwenyezi-Mungu,
maana jina lake peke yake latukuka;
utukufu wake wapita dunia na mbingu.
14Amewapa watu wake nguvu;
heshima kwa watu wote waaminifu,
watu wa Israeli wapenzi wake.
Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza