3
1Basi, Myahudi ana nini zaidi kuliko watu wengine? Au kutahiriwa kuna faida gani? 2Naam, iko faida kwa kila upande. Kwanza, Mungu aliwakabidhi Wayahudi ujumbe wake. 3Lakini itakuwaje iwapo baadhi yao hawakuwa waaminifu? Je, jambo hilo litaondoa uaminifu wa Mungu? 4Hata kidogo! Mungu hubaki mwaminifu daima, ingawaje kila binadamu ni mwongo. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo:
“Kila usemapo,
maneno yako ni ya kweli;
na katika hukumu,
wewe hushinda.”#3:4 Zab 51:4. Zaburi inayonukuliwa hapa inasema kwamba kama Mungu angewekwa mahakamani yeye daima angeonekana kuwa bila hatia yoyote.
5Lakini, ikiwa uovu wetu unathibitisha kwamba Mungu anatenda kwa haki, tutasema nini? Je, tutasema kwamba anakosa haki akituadhibu? (Hapa naongea kibinadamu). 6Hata kidogo! Ingekuwa hivyo, Mungu angewezaje kuuhukumu ulimwengu?
7Labda utasema: “Ikiwa ukosefu wa uaminifu kwa upande wangu unamdhihirisha Mungu kuwa mwaminifu zaidi na hivyo kumpatia utukufu, basi singepaswa kuhukumiwa kuwa mwenye dhambi!” 8Ni sawa na kusema: Tufanye maovu ili tupate mema!#3:8 Ni sawa na kusema: Tufanye maovu …mema: Baadhi ya wapinzani wa Paulo walikuwa wanasema kwamba Paulo anawatia watu moyo watende uovu na kukataa kutii sheria ya Mose, kwa vile Mungu huonesha mapendo yake kwa kuwasamehe. Hao wapinzani wa Paulo walitaka wafuasi wote wa Yesu wafuate sheria ya Mose na mapokeo mengine ambayo yaliongezwa na kuchukuliwa kuwa sehemu ya sheria ya Mose. Ndivyo wengine walivyotukashifu kwa kutushtaki kwamba tumefundisha hivyo. Watahukumiwa wanavyostahili!
Hakuna mtu yeyote aliye mwadilifu
9Tuseme nini, basi? Je, sisi Wayahudi ni bora kuliko wengine? Hata kidogo! Kwa maana nimekwisha bainisha hapo mwanzoni kwamba Wayahudi na watu wa mataifa mengine wote wako chini ya utawala wa dhambi. 10Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo:
“Hakuna hata mmoja aliye mwadilifu!#3:10 Hakuna hata mmoja aliye mwadilifu: Namna nyingine ya kusema alichotamka Paulo katika 9 kwamba Wayahudi na watu wa mataifa … wote wako chini ya utawala wa dhambi (taz Zab 14:1-3 na sambamba yake, yaani Zab 53:1-3) ambayo imenukuliwa kulingana na tafsiri ya Septuajinta.
11Hakuna mtu anayeelewa,
wala anayemtafuta Mungu.
12Wote wamepotoka
wote wamekosa;
hakuna atendaye mema,
hakuna hata mmoja.
13Makoo yao ni kama kaburi wazi,
ndimi zao zimejaa udanganyifu,
midomoni mwao mwatoka maneno yenye sumu kama ya nyoka.
14Vinywa vyao vimejaa laana chungu.
15Miguu yao iko mbioni kumwaga damu,
16popote waendapo husababisha maafa na mateso;
17njia ya amani hawaijui.
18Hawajali kabisa kumcha Mungu.”
19Tunajua kwamba sheria#3:19 Sheria: Yaani, sheria ya Mose ambayo kwa jumla ilitakiwa kuwaonesha watu namna Mungu anavyotaka watu waishi. huwahusu walio chini ya sheria hiyo, hata hawawezi kuwa na kisingizio chochote, na ulimwengu wote uko chini ya hukumu ya Mungu. 20Maana hakuna binadamu yeyote anayekubaliwa kuwa mwadilifu mbele yake Mungu kwa kushika sheria; kazi ya sheria ni kumwonesha tu mtu kwamba ametenda dhambi.
Kukubaliwa na Mungu kwa imani
21Lakini sasa, njia ya Mungu ya kuwakubali watu kuwa waadilifu imekwisha dhihirishwa, tena bila kutegemea sheria. Sheria na manabii#3:21 Sheria na manabii: Maneno hayo mawili ni mafungu makuu ya Maandiko ya A.K. Rejea Rom 1:17; 4:3. hushuhudia jambo hili. 22Mungu huwakubali watu kuwa waadilifu kwa njia ya imani yao kwa Yesu Kristo;#3:22 Kwa njia ya imani yao kwa Yesu Kristo: Gal 2:16. Mungu hufanya hivyo kwa wote wanaoamini; hakuna ubaguzi wowote. 23Watu wote wametenda dhambi na wametindikiwa utukufu wa Mungu.#3:23 Wote wametenda dhambi na wametindikiwa utukufu wa Mungu: Kutindikiwa utukufu wa Mungu hapa kunaweza kueleweka kwamba watu hawawezi kufuata sheria ya Mungu kikamilifu au hawawezi kuishi kwa kufuata matakwa yake (taz Kut 40:34; Zab 143:2 na Rom 5:2; 8:18). Wengine lakini wanafikiri hapa yahusu ule uhusiano wa mtu wa awali kabisa ambapo alikuwa ameumbwa kwa mfano na sura yake Mungu (Mwa 1:26-27; 1Kor 11:7). Binadamu aliupoteza uhusiano huo na Mungu kwa sababu ya dhambi. 24Lakini kwa zawadi ya neema ya Mungu, watu wote hukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Yesu Kristo#3:24 Watu …hukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Yesu Kristo: Mungu kwa kifo na ufufuo wa Yesu Kristo ulimwengu wote unakombolewa. Rejea Rom 8:23; 1Kor 1:30; Efe 1:7; Kol 1:14. anayewakomboa. 25Mungu alimtoa Yesu kusudi, kwa damu yake, awe njia ya kuwaondolea watu dhambi#3:25-26 Mungu alimtoa Yesu …kwa damu yake, awe njia ya kuwaondolea watu dhambi: Katika A.K. siku ya upatanisho kuhani alitoa tambiko ya mnyama na kurashia damu yake juu ya sanduku la agano ili kuondoa dhambi za watu wa Israeli (Lawi 16:14-16). Taz pia 1Kor 1:30; Efe 1:7-8; Ebr 9:15. zao kwa imani yao kwake. Alifanya hivyo ili apate kuonesha kwamba yeye ni mwadilifu. Hapo zamani Mungu alikuwa mvumilivu bila kuzijali dhambi za watu; 26sasa, wakati huu, anazikabili dhambi za watu apate kuonesha uadilifu wake. Kwa namna hiyo Mungu mwenyewe huonesha kwamba yeye ni mwadilifu na kwamba humfanya kuwa mwadilifu mtu yeyote anayemwamini Yesu.
27Basi, tunaweza kujivunia nini? Hakuna! Kwa nini? Je, kwa sababu ya kutimiza sheria? La! Bali kwa sababu tunaamini. 28Maana Mungu humkubali mtu kuwa mwadilifu kwa imani, wala si kwa kutimiza matakwa ya sheria.#3:28 Mungu humkubali mtu kuwa mwadilifu kwa imani …si kwa kutimiza … sheria: Mate 13:39; Rom 1:17; Gal 2:16; Efe 2:8-9; 2Tim 1:9; Tito 3:5. Neno la Kigiriki ambalo limetafsiriwa hapa kwa kumkubali mtu kuwa mwadilifu pengine linatafsiriwa kwa “kuthibitisha mtu kuwa haki”. Lakini watu wanakubaliwa kuwa na uhusiano mwema na Mungu kwa sababu wana imani, yaani wanalo tegemeo lao katika Yesu Kristo. 29Au je, Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu, ama pia wa watu wa mataifa mengine? Naam, wa watu wa mataifa mengine pia. 30Mungu ni mmoja, naye atawafanya Wayahudi kuwa waadilifu kwa imani yao, na watu wa mataifa mengine pia kwa imani yao. 31Je, tunaitumia imani kuibatilisha sheria?#3:31 Je, tunaitumia imani kuibatilisha sheria?: Paulo hapendi sheria ibatilshwe maana yenyewe inaonesha yale Mungu anayotaka. Tatizo kubwa analoliona Paulo ni kwamba watu wengine wanalichukulia jambo la kufuata sheria kuwa ni muhimu kuliko imani. Hata kidogo; bali tunaipa sheria thamani yake kamili.