Sira 1
BHNTLK

Sira 1

1
Sifa kwa Hekima
1 # 1:1 Dibaji ya mtafsiri: Huu utangulizi si sehemu ya kitabu cha awali cha Sira; hata hivyo unatupatia habari teletele kuhusu chanzo cha kitabu hicho. Hekima yote hutoka kwa Bwana,
nayo imo kwake hata milele.#1:1 Kitabu cha Sira kiliandikwa kwanza kwa Kiebrania, halafu aliyeandika dibaji hii alikitafsiri katika Kigiriki.
2Nani awezaye kuuhesabu mchanga wa pwani
au matone ya mvua?
Nani awezaye kuzihesabu siku za milele?
3Je, kimo cha mbingu ni kiasi gani?
Je, upana wa dunia ni kiasi gani?
Je, kina cha bahari ni kiasi gani?
Nani aujuaye umaarufu wa Hekima?
Nani awezaye kuyajibu maswali haya?
4Hekima iliumbwa kabla ya vitu vyote,
busara ilikuwako tangu zama zote.#1:4 Hati nyingine zina aya ya 5: Chanzo cha hekima ni neno la Mungu aliye juu; njia zake ni amri za milele.
6Nani aliyeoneshwa kitovu cha Hekima?
Nani anafahamu mafumbo ya Hekima?#1:6 Hati nyingine zina aya 7: Ujuzi wa hekima alijulishwa nani? Na uzoefu wake mwingi nani aliyepata kuuelewa?
8Yuko mmoja tu mwenye hekima wa kutisha sana,
ameketi katika kiti chake cha enzi - ndiye Bwana.
9Bwana mwenyewe ndiye aliyemuumba Hekima;
yeye ndiye aliyemwona na kumpima,
na kumjaza katika kazi zake zote.
10Hekima yumo katika kila kiumbe kadiri atoavyo Mungu;
Mungu humgawia kila mtu ampendaye.#1:10 Mhub 2:26; Sira 24:11-12. Hati nyingine zinaongeza hapa: Upendo wa Bwana ni hekima tukufu; huwapatia wale wanaojitokeza kutaka kuiomba.
11Kumcha Bwana#1:11 Kumcha Bwana: Neno kwa neno “kumwogopa Bwana”. Neno la Kiebrania, zaidi ya woga, huleta uchaji na heshima, upendo na utii kwa Mungu, jambo ambalo ndilo lililo kwa mtu aliye mwamini Mungu wa kweli. Hali hiyo ni sehemu muhimu ya hekima. Rejea aya 14. huleta fahari na sifa,
huleta furaha na taji ya shangwe.
12Kumcha Bwana kwaufurahisha moyo,
kwaleta shangwe, furaha na maisha marefu.#1:12 Hati nyingine za mkono zinaongeza: Kumcha Bwana ni zawadi ya Bwana; yeye pia hutayarisha njia imara kwa upendo.
13Amchaye Bwana atafanikiwa mwisho wake;
siku ya kufa kwake atabarikiwa.
14Kumcha Bwana ni mwanzo wa Hekima,
Hekima ameumbwa na waaminifu tangu tumboni mwa mama.
15Amejiwekea msingi wa kudumu kati ya watu,
na vizazi vijavyo vitamtegemea Hekima.
16Kumcha Bwana ni ukamilifu wa hekima,
Hekima huwatosheleza watu kwa matunda yake.
17Huzijaza nyumba zao bidhaa zote wanazohitaji
na bohari zao mazao yake.
18Kumcha Bwana ni kuvikwa taji la hekima,
Hekima huleta amani na afya nzuri.#1:18 Hati nyingine za mkono zinaongeza: Vitu hivyo viwili ni zawadi ya Mungu kwa amani; huwapa kutosheka kabisa wale wanaompenda.
19Bwana alimwona na kumpima,
alinyesha duniani maarifa na utambuzi,
na kuwapa fahari wale wanaomshikilia.
20Kumcha Bwana ni kitovu cha Hekima,
na matawi yake ni maisha marefu.#1:20 Baadhi ya hati zinaongeza aya 21: Kumheshimu Bwana huondoa dhambi; panapopatikana uchaji wa Bwana, huondoa hasira.
22Hasira isiyo halali haikubaliki,
maana hasira husababisha maangamizi ya mtu.
23Mvumilivu husubiri hadi wakati ufaao,
na hatimaye furaha itambubujikia.
24Huyo huzuia maneno yake hadi wakati ufaao,
ndipo watu wengi wataisifu busara yake.
25Bohari za Hekima zimejaa misemo ya busara,
lakini uchaji ni chukizo kwa mwenye dhambi.
26Ukitaka hekima zishike amri,
naye Bwana atakupa hekima,
27Maana kumcha Bwana ni hekima na nidhamu,
naye hupendezwa na uaminifu na upole.
28Usitupilie mbali kumcha Bwana,
wala usimwendee kwa moyo mdanganyifu.
29Usiwe mnafiki mbele ya watu;
uuchunge mdomo wako.
30Usijitukuze, la sivyo utaanguka
na kujiletea aibu wewe mwenyewe.
Bwana atazifunua siri zako
na kukuangusha mbele ya jumuiya,
kwa kuwa hukumwendea Bwana kwa uchaji,
na moyo wako ulikuwa umejaa udanganyifu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza