Sira 14
BHNTLK

Sira 14

14
1Heri mtu asiyekosea kwa ulimi wake;
hahitaji kusikitika kuwa amekosa.
2Heri mtu ambaye dhamiri yake haimshtaki,
na ambaye hajakata tamaa.
Matumizi ya mali
3Si sawa kwa mtu mchoyo kuwa tajiri.
Utajiri una maana gani kwa mtu bahili?
4Mtu anayekusanya mali kwa kujinyima mwenyewe,
anawakusanyia watu wengine.
Hao wataiponda mali yake katika anasa.
5Aliye bahili kwake mwenyewe atakuwa mkarimu kwa nani,
kama hafurahii utajiri wake mwenyewe?
6Hakuna mtu bahili kuliko anayejichukia mwenyewe;
ndivyo ubaya wake unavyomlipa yeye mwenyewe.
7Hata kama akitenda wema, hutenda kwa ajali.
na mwishowe hujulisha hali yake duni.#14:7-8 Aya hizi zimetafsiriwa kulingana na makala ya Kigiriki; nazo hazimo katika Kiebrania.
8Mtu mwenye kijicho ni mwovu;
huangalia pembeni na kuwadharau watu.
9Jicho la mchoyo haliridhiki na kile alicho nacho,
na uchoyo huidhoofisha roho.
10Mtu mchoyo ni bahili wa chakula,
haweki chakula mezani pake.
11Mwanangu, tumia vitu vyako kukufurahisha uwezavyo,
na mtolee Bwana tambiko zitakiwazo.
12Kumbuka kwamba kifo hakitakawia,
na kwamba hujatangaziwa kauli ya kuzimu.#14:12 Makala ya Kiebrania inaongeza hapa: “katika ufalme wa wafu hakutakuwa na furaha”.
13Mtendee rafiki yako mema kabla hujafa;
uwe mkarimu na kumpa kadiri ya uwezo wako.
14Usijinyime siku moja ya furaha,
usiache sehemu yako ya furaha halali ikuponyoke.
15Siku moja utawaachia wengine matunda ya jasho lako;
yote uliyochuma kwa kazi ngumu yatagawanywa kwa kura.
16Wape wengine na kupokea kwao ujifurahishe moyo,
maana mtu hatazamii starehe huko kuzimu.
17Viumbe vyote hai huchakaa kama vazi,
maana kauli ya tangu zama ni: “Lazima mtakufa!”
18Kama vile majani katika mti uliotanda matawi:
hupukutika yakaanguka na mengine huota,
ndivyo ilivyo kwa binadamu wenye mwili na damu:
mmoja hufa na mwingine huzaliwa.
19Kila kilichotengenezwa huchakaa na kutoweka,
naye mtengenezaji hutoweka na kazi yake.#14:19 Katika maoni ya kawaida ya A.K., maisha hukoma kwa kifo (Mhub 1:3-4). Huko baadaye hamna uwezekano wa furaha (Zab 6:5; 88:10-12; 115:17; Isa 38:18). Ni katika baadhi ya makala hasa zile za baadaye, ndipo tunapokuta wazo la uhai baada ya kifo (Zab 16:10; Dan 12:2-3; 2Mak 7:9,14,23; Hek 3:1-9). Ukweli huu utadhihirika wazi katika A.J. (Mat 13:43; 1Kor 15; Ufu 21—22).
Furaha ya kuwa na Hekima
20Heri mtu anayetafakari juu ya Hekima#14:20 Heri mtu anayetafakari juu ya Hekima: Sira 19:20; 24:22.
mtu anayefikiri kwa busara.
21Yule anayezifikiria njia za Hekima,
na kuwaza na kuwazua pia juu ya siri zake.#14:21 Taz 4:11-19 maelezo.
22Mtu amtafutaye Hekima kama vile mwindaji,
na kukaa kwenye njia zake kumngojea.
23Mwenye kuchungulia madirishani mwake,
na kusikiliza milangoni mwake.
24Mwenye makazi yake karibu na nyumba yake
na kufunga kigingi cha hema lake ukutani mwake.
25Mwenye kusimika hema lake karibu naye
na kukaa katika makao yake mazuri.
26Huweka watoto wake chini ya ulinzi wake,
na kupumzika chini ya matawi yake.#14:26 Na kupumzika chini ya matawi yake: Hapa hekima inapewa picha ya mti wenye kivuli.
27Kwake atapata kivuli cha kumkinga na joto,
na kukaa katika fahari yake.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza