Sira 16
BHNTLK

Sira 16

16
Mungu atawaadhibu wenye dhambi
1Usitamani kuwa na watoto wengi wasio na faida;
wala kujivunia watoto wa kiume wasiomcha Mungu.
2Wakiongezeka usifurahi kwa sababu yao,
isipokuwa kama wanamcha Bwana.
3Usiwe na imani juu ya kuendelea kwao kuishi;
usitegemee wingi wao.
Maana, mtoto mmoja ni bora kuliko elfu;
ni afadhali kufa bila mtoto,
kuliko kuwa na watoto wasiomcha Mungu.
4Mji utajaa watu kwa busara ya mtu mmoja,
lakini kwa kabila moja la wabaya utabaki mtupu.
5Macho yangu yameona mambo mengi kama haya;
masikio yangu yamesikia mambo ya ajabu kuliko hayo.
6Moto utawashwa katika kusanyiko la wenye dhambi,
ghadhabu iliwashwa katika taifa lililoasi.#16:6 Wenye dhambi …taifa lililoasi: Yamkini yahusu uasi wa Kora, Dathani na Abiramu (rejea Hes 16:1-35).
7Yale majitu ya zamani#16:7 Majitu ya zamani: Dokezo kwa visa kama vya wale majitu katika Mwa 6:1-7. hakuyasamehe,
majitu ambayo kwa kutegemea nguvu zao yaliasi.
8Mungu hakuwahurumia jirani za Loti,
watu ambao alichukizwa na kiburi chao.#16:8 Yahusu kuangamizwa kwa Sodoma na Gomora Mwa 19:1-25.
9Hakulionea huruma taifa lililopangiwa kuangamizwa,
taifa lililofutiliwa mbali kwa sababu ya dhambi zake;
10hata wale wanajeshi 600,000 wa miguu
ambao walikusanyika pamoja, wakaasi kwa kiburi chao.
11Hata kama kuna mtu mmoja mwenye kiburi,
itakuwa ajabu kama hataadhibiwa.
Maana Bwana ni mwenye huruma na ghadhabu.
Yeye ana nguvu kuu ya kusamehe na huwaka hasira;
na wale wasiotubu anawamwagia ghadhabu yake.
12Kama zilivyo kuu huruma zake ndivyo na karipio lake.
Yeye humhukumu mtu kulingana na matendo yake.#16:12 Humhukumu mtu kulingana na matendo yake: Rejea Yobu 34:11; Zab 62:12; Meth 24:12; Mat 16:27; Rom 2:6.
13Mwenye dhambi hataweza kutoroka na alichonyakua;
na tazamio la wanaomcha Mungu halitakuwa bure.
14Mwadilifu atapokea anayostahili,#16:14 Kiebrania: Mwadilifu … anayostahili; Kigiriki: “Atamfanya chumba cha kila tendo la huruma”.
kila mtu atapokea kulingana na matendo yake.#16:14 Hati nyingine huongeza aya 15: “Bwana alimfanya Farao awe na kiburi hata asimkiri Bwana; ili ulimwengu ufahamu kazi za Bwana. 16 Huruma zake ni wazi kwa viumbe vyote; alitenga kati ya mwanga wake na giza kwa kamba ya kupimia”.
17Usiseme, “Nitajificha mbali na Bwana;
na hamna yeyote huko juu atakayenikumbuka!
Kati ya watu wengi hivyo sitajulikana,
maana, nafsi yangu ni kitu gani kati ya viumbe visivyohesabika?”#16:17 Maneno haya hayana maana ya kwamba msemaji anakiri udogo wa binadamu, bali ni matamshi ambayo yanasema juu ya fikra za mpumbavu, kwani yeye anafikiri Mungu hajali juu ya matendo yake (aya 20-23).
18Tazama, mbingu na mbingu za juu kabisa,
kuzimu na dunia, vyote vitatetemeka,
wakati Bwana atakapokuja.
19Milima na misingi ya dunia hutetemeka,
wakati Bwana anapoviangalia.
20Lakini hakuna binadamu anayefikiri hayo;
ni nani awezaye kuelewa njia za Mungu?
21Usiseme: “Nikitenda dhambi hakuna anionaye.
Nikitenda hayo katika siri kuu nani atajua?
22Na nikitenda mema nani atayataja?
Nani anangojea apewe taarifa?
Yeye hukawia mno kutekeleza agano lake.”
23Ndivyo afikiriavyo mtu asiye na akili;
mtu mjinga aliyepotoshwa hufikiri kipumbavu.
Hekima ya Mungu katika maumbile
24Mwanangu, nisikilize ujifunze maarifa.
Tega sikio usikie maneno yangu.
25Nitakupa mafunzo mazitomazito,
nitakufundisha maarifa kwa usahihi.
26Mungu alipoumba kazi zake mwanzoni
alizifanya ziwepo na kuzipa mpango,
27akazipa mpango wa kufuata milele,
tangu mwanzo wake na vizazi vyote.
Hivyo hazitindikiwi wala kuchoka
na haziachi kutekeleza wajibu wao.
28Hakuna hata mojawapo inayosongana na nyingine
na wala haziachi kutii neno lake Mungu.
29Baada ya hayo yote Bwana aliiangalia dunia
akaijaza vitu vyake vizuri.
30Aliifunika dunia kwa kila aina ya viumbe,
ambavyo vitakufa na kurudi udongoni.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza