Sira 3
BHNTLK

Sira 3

3
Wajibu wa watoto kwa wazazi
1Wanangu sikilizeni mawaidha ya baba yenu.
Fanyeni ninayowaambia,
nanyi mtawekwa salama,
2maana Bwana amewapa kina baba mamlaka juu ya watoto wao,
na kuimarisha uwezo wa kina mama juu ya watoto wao.
3Anayemheshimu baba yake anajipatia msamaha wa dhambi zake.
4Anayemheshimu mama yake anajiwekea hazina kubwa.
5Anayemheshimu baba yake atafurahishwa na watoto wake mwenyewe,
na atakapomwomba Bwana, atasikilizwa.
6Anayemheshimu baba yake atapata maisha marefu,
anayempendeza mama yake anamtii Bwana.#3:6 Anayempendeza mama yake anamtii Bwana: Tafsiri kadiri ya makala ya Kisiria. Tafsiri ya Kigiriki ya Septuajinta (LXX) ina “Yeye anayemtii Bwana, atampa faraja mama yake”.
7Mtoto huyo, huwatumikia wazazi wake kama Bwana wake.#3:7 Mwanzoni mwa mstari huu hati nyingine zina: “Amchaye Bwana atamheshimu baba yake”.
8Mheshimu baba yako kwa maneno na matendo,
ili upate baraka kutoka kwake.
9Maana baraka za baba huimarisha nyumba za watoto,#3:9 Baraka ya baba kwa watoto wake, hasa wakati anakufa, ilikuwa na thamani kubwa sana miongoni mwa Waisraeli na pia miongoni mwa watu wengi wetu. Rejea Mwa 27:27-29 (Isaka); 48:15-20; 49:1-27 (Yakobo).
hali laana ya mama huing'oa misingi ya nyumba zao.#3:9 Hati nyingine za mkono huongeza hapa: “Kwa kuwa tuzo ni zawadi ya milele, pamoja na furaha”.
10Usijikuze mwenyewe kwa kumdharau baba yako.
maana kumdharau baba yako hakutakuletea faida.
11Maana fahari ya baba mtu ni fahari ya huyo mtoto,
na watoto wasiomheshimu mama yao ni balaa.
12Mwanangu, mtunze baba yako alipo mzee
wala usimhuzunishe muda wote aishipo.
13Hata akipungukiwa akili, umvumilie.
usimdharau kwa vile wewe una afya na nguvu.
14Bwana hatasahau wema wako kwa baba yako,
utakusaidia kukupatia msamaha wa dhambi zako.
15Wakati wa taabu Bwana atakumbuka wema wako.
Kama umande kwenye jua, dhambi zako zitatoweka.
16Anayemtupa baba yake anamkufuru Mungu;
anayemkasirisha mama yake analaaniwa na Bwana.
Unyenyekevu
17Mwanangu, uwe mpole katika shughuli zako,
nawe utapendwa na wale wanaokubaliwa na Mungu.
18Kadiri ulivyo mkuu, ndivyo unavyotakiwa kunyenyekea;
na hapo utapata kibali cha Bwana.#3:18 Hati nyingine za Kigiriki zina mstari wa 19: “Wengi hujitukuza na kujiona bora, lakini siri za Mungu hufunuliwa kwa wanyenyekevu”. Makala ya Kiebrania: “Huruma za Mungu ni kubwa, naye huwafunulia wanyenyekevu siri zake”.
20Nguvu ya Bwana ni kuu
lakini hutukuzwa na wanyenyekevu.
21Usitafute yaliyo magumu mno kwako,
wala kuchunguza yaliyo nje ya uwezo wako.
22Zingatia yale uliyopangiwa kufanya,
huhitaji kujihangaisha juu ya mambo yaliyofichika
23Usiingilie mambo yanayopita nguvu zako
maana hata hayo uliyooneshwa yanapita akili ya binadamu.
24Maana wengi wamepotoshwa kwa kujiona kuwa wajuzi sana,
maoni yao ya utundu yamepotosha akili zao.#3:24 Baadhi ya hati za mkono za Kigiriki zina aya: 25 “kama huna Macho huwezi kuona; usijitakie kuwa na akili kama hunayo”. Baada ya aya ya 27 Kiebrania kina: “Kama huna Macho huwezi kuona; kama huna akili huwezi kuwa na Hekima”.
26Mwenye kiburi ataishia vibaya mwishoni;
na apendaye hatari ataangamia huko.#3:26 Apendaye hatari ataangamia huko: Meth 28:14; Rom 2:5. Kiebrania kina: “apendaye anasa atabanwa nazo”.
27Mwenye kiburi atalemewa taabu;
mwenye dhambi#3:27 Mwenye dhambi: Kadiri ya tafsiri ya Kigiriki. Kiebrania si dhahiri. hujirundikia dhambi mfululizo.
28Mateso ya mwenye kiburi#3:28 Mateso ya mwenye kiburi: Kadiri ya makala za kale; Kiebrania kina: “Usijaribu kuponya jeraha la mwovu”. hayana matibabu.
maana uovu umeota na kutia mzizi ndani yake.
29Mwenye akili atazitafakari methali moyoni mwake;
kuwa mtu msikivu ndicho atakacho mwenye busara.
Kuwasaidia maskini
30Kama vile maji yazimavyo moto mkali
ndivyo na sadaka kwa maskini iletavyo msamaha wa dhambi.#3:30 Rejea Tob 4:7-11; 12:8-9; Sira 29:8-13. Neno la Kiebrania lililotafsiriwa hapa kama kuwapa maskini (au kusaidia maskini) awali lilikuwa na maana ya kutenda kwa uadilifu, kutenda mema. Kwa maana inayofanana na hiyo hutumia neno la Kigiriki lenye maana hiyo katika Mat 6:1.
31Amwoneaye huruma mwenzake hufikiria mbele,
wakati atakapopata taabu atasaidiwa.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza