Tobiti 13
BHNTLK

Tobiti 13

13
Wimbo wa Tobiti
1Basi, Tobiti akasema utenzi huu:#13:1 Utenzi unaofuata, licha ya mazingira ya simulizi lenyewe, unarejea kwa kitendo cha Mungu ambacho kinahusu kwa jumla historia ya Waisraeli. Sehemu ya kwanza (aya 1-10a) inatilia maanani mazingira yote ya Waisraeli wakiwa wametawanywa miongoni mwa mataifa.
“Atukuzwe Mungu aishiye milele,
maana utawala wake wadumu nyakati zote.
2Yeye huadhibu na kusamehe;
huwaporomosha watu chini katika makao ya wafu,
kisha huwanyanyua humo maangamizini;
hakuna awezaye kuukwepa mkono wake.
3“Enyi watu wa Israeli, msifuni mbele ya mataifa,
maana kama amewatawanya miongoni mwao,
4humohumo amewaonesha nyinyi ukuu wake.
Mtukuzeni mbele ya viumbe vyote.
Yeye ni Bwana na Mungu wetu;
yeye ni Baba#13:4 Bwana …Baba: Taz Sira 23:1 yetu na Mungu milele na milele.
5“Ingawa huwaadhibu kwa uovu wenu,
atawahurumieni nyinyi nyote;
atawakusanya kutoka kila taifa
kila mahali mlikotawanywa.#13:5 Atawakusanya kutoka kila taifa …mlikotawanywa: Kumb 30:3.
6“Kama mkimrudia Mungu kwa moyo na roho yote,
mkaishi kwa ukweli#13:6 Mkimrudia Mungu …mkaishi kwa ukweli: Kumb 30:2. mbele yake,
yeye naye atawarudieni
wala hatawaficheni tena uso wake.
7Kumbukeni jinsi alivyowatendeeni vema,
na kumshukuru kwa sauti.
Mtukuzeni Bwana mwenye haki;
mheshimuni Mfalme wa milele.
8“Mimi, naimba sifa zake uhamishoni,
nadhihirisha uwezo na ukuu wake
miongoni mwa taifa lenye dhambi.
Enyi wenye dhambi mrudieni Bwana,
fanyeni mambo ya haki mbele yake.
Huenda atawaonesha wema wake
na kuwaoneeni huruma tena.#13:8 Waisraeli ambao wametawanywa kati ya mataifa mengine watageuka na kuwa mashahidi wa Mungu wa kweli na kuitwa waongoke.
9“Kwa upande wangu mimi namtukuza Mungu;
nafsi yangu yashangilia kwake Mfalme wa mbingu.
10“Kila mmoja na atangaze ukuu wake
na kuimba sifa zake huko Yerusalemu.#13:10 Sehemu ya pili ya utenzi huu (10b-18) inabadili mtazamo ulio katika sehemu iliyotangulia. Hii inahusu kuangamizwa kwa Yerusalemu (tukio ambalo ni la siku za uhosi kadiri ya Tobiti, lakini kwa huyo aliyeweka maandishi haya katika hali yake ya sasa ni tukio lililokwisha fanyika).
“Ewe Yerusalemu, mji mtakatifu,
Mungu amekuadhibu kwa makosa ya watu wako,
lakini atawahurumia watu watendao yaliyo sawa.
11Mshukuru Bwana maana ni mwadilifu,
mtukuze Mfalme wa milele;
hekalu lake lijengwe upya kwako kwa furaha;
12awafurahishe watu wako wote walio uhamishoni,
awaangalie kwa upendo wote walio taabuni,
mpaka vizazi vyote vijavyo.
13“Mwanga mwangavu itaziangaza nchi zote duniani;
mataifa mengi yatakuja kutoka mbali,
wakazi wa nchi zote za mbali duniani
watakuja kulitukuza jina takatifu la Mungu wako.
Watakuja na zawadi kwa mfalme wa mbinguni.
Kwako vizazi na vizazi vitatangaza furaha yao
na jina lako wewe mteule litadumu milele,
katika vizazi vyote vijavyo.
14Na walaaniwe wote watakaokutisha!
Walaaniwe wote watakaokuharibu na kuangusha kuta zako
wote watakaovunja minara na kuchoma nyumba zako!
Lakini wabarikiwe daima wote watakaokujenga.
15“Furahi, kwa sababu ya watu wako waadilifu;
maana watakusanywa pamoja kutoka uhamishoni
na kumtukuza Bwana wa nyakati zote.
“Heri yao wote wakupendao
na kufurahia ustawi wako.
16Heri yao wote wanaohuzunika juu ya adhabu yako
maana watafurahi pamoja nawe upesi,
watashuhudia furaha yako milele.
“Nafsi yangu yamtukuza Mungu, Mfalme mkuu;
17Maana Yerusalemu utajengwa upya,
na makao yake yatakuwa humo milele.
“Nitakuwa na furaha kiasi gani
wanangu watakapoona utukufu wako
na kumshukuru Mfalme wa mbinguni!
“Milango yako Yerusalemu itatengenezwa
kwa mawe ya johari na zumaridi,
na kuta zako zote kwa mawe ya thamani;
Minara yako itajengwa kwa dhahabu,
na maboma yake kwa dhahabu safi.
Barabara zako zitasakafiwa
kwa mawe ya hakiki na vito vya Ofiri.
18Malango yako yatajaa nyimbo za shangwe;
na katika nyumba zako zote kutaimbwa:
‘Asifiwe Mungu!#13:18 Asifiwe Mungu: Tamko hili katika Kigiriki ni “Aleluya”, tamko lililochukuliwa kutoka Kiebrania “Haleluya” (Msifuni Yahweh) na lenye maana hiyo. Linatokea mara kwa mara katika Zaburi (rejea Zab 104:35). Taz pia Ufu 19:1. Sehemu yote ya 13:10-18 inasikika kwa namna moja au nyingine katika Isa 44:26-28; 54:11-12; 60:1-22; Zek 1:16; Ufu 21:10-21. Atukuzwe Mungu wa Israeli!’
Kwako Yerusalemu, watalisifu jina lake takatifu
milele na milele.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza