Hekima ya Solomoni 2
BHNTLK

Hekima ya Solomoni 2

2
1Katika upotovu wao huambiana:
“Maisha yetu ni mafupi na yenye taabu.
Kifo kinapowasili hakuna dawa ya kuepukana nacho.
Hakuna mtu aliyewahi kumtoa mwingine ahera.#2:1-20 Katika hoja za hao waovu inawezekana kuona sehemu tatu: Kukataa kwamba kuna maisha baada kifo (aya 1-5); na kutokana na hilo, cha thamani kwao ni anasa tu na kuwa na nguvu (aya 6-11); kuwatesa wale ambao hawana fikira kama zao au hawapatani na mawazo yao (aya 12-20).
2Sisi tulizaliwa kwa bahati tu,
tukisha kufa itakuwa kana kwamba hatukupata kuwapo.
Pumzi yetu ni kama moshi tu unaotoweka;
akili zetu ni ndogo tu zinazowashwa kwa mapigo ya mioyo yetu.#2:2 Watu waovu wana fikira za kidunia kuhusu uhai, fikira ambazo hukataa kwamba Mungu aliumba ulimwengu na kufikiri kwamba kila kitu huishia katika kifo.
3Cheche hiyo ikizimika, mwili wetu utageuka majivu,
na roho yetu itatoweka kama vile hewa.
4Jina letu litasahaulika punde si punde,
mambo tuliyotenda hayatakumbukwa;
maisha yetu yatatoweka kama nyayo za mawingu;
yatatawanywa kama ukungu unaofukuzwa na nuru ya jua,
unaoshindwa kustahimili joto la jua.
5Siku zetu ni kama kivuli kipitacho.
na tukisha kufa hatuwezi kurudi kutoka humo.
Siku ya kufa imepangwa wala hakuna atakayeweza kuirudisha.
6Hivyo na tujifurahishe kwa chochote kizuri kilichopo;
tuvitumie kabisa viumbe kama wakati wa ujana.
7Tujishibishe divai ya thamani na marashi,
tujichumie maua ya vuli yasitupite.
8Tujivike taji za waridi kabla hayajanyauka.
9Kila mmoja wetu ashiriki tamasha zetu,
tuache alama za anasa zetu zionekane kila mahali.
Maana ndivyo maisha yalivyo! Ndiyo tuliyopangiwa.
10“Maskini, hata akiwa mwema, tutamkandamiza;
naye mjane hatutamhurumia
wala kumjali mzee mwenye mvi.#2:10 Waovu kwa kukataa kuheshimu na kusaidia maskini, wajane na wazee, wanapuuza vitendo halisi vya uadilifu (rejea Lawi 19:32; Kumb 24:10-21).
11Nguvu zetu ndizo mwongozo wa haki,
mnyonge hana faida yeyote!
12Tena, tumvizie mtu mwema;
mtu huyo ni usumbufu kwetu na hutupinga.
Hutukaripia kila tunapovunja sheria;
hutushtaki kila tunapokiuka mwongozo.#2:12 Neno lililotafsiriwa hapa kama “mwema” mahala pengine katika kitabu hiki laweza kuwa pia na maana ya mtu wa haki na kumtaja pia mtu anayeishi kwa uadilifu kuhusu uhusiano wake na Mungu (aya 13) na uhusiano wake na jirani (aya 12).
13Mtu mwema hujitakia kumjua Mungu
na kujiita mtoto wake Bwana.#2:13 Mtoto wake Bwana: Rejea aya 16 na taz Sira 23:1 maelezo.
14Mtu wa namna hiyo amekuwa kwetu karipio la fikira zetu.
15Hata tu kumtazama ni mzigo kwetu;
maana anaishi tofauti na watu wengine
njia zake ni ngeni kabisa.
16Anatuona sisi kuwa kama madini hafifu;
huziepa njia zetu kama kukwepa uchafu.
Huuthamini kuwa heri mwisho wa mwadilifu,
na hujigamba kwamba Mungu ni Baba yake.
17Haya, na tuone kama maneno yake ni ya kweli!
Tuone yatakayompata wakati atakapokufa.
18Kama kweli yeye ni mwana wa Mungu, Mungu atamsaidia,
na kumkomboa makuchani mwa maadui zake.
19Haya! Tumtendee kikatili na kumtesa,
tuone alivyo mpole,
tuujaribu uvumilivu wake.
20Tutamhukumu kifo cha aibu
maana, kama alivyosema, Mungu atamwokoa!”
Mambo ya nje hudanganya
21Ndivyo wafikiriavyo waovu,
lakini wanajidanganya wenyewe.
Uovu wao umewapofusha.
22Hawajui mipango ya siri ya Mungu;
hawajawahi kutumaini kupata thawabu ya kuishi vema,
wala kulitambua tuzo la watu waishio bila hatia.
23Mungu aliumba watu waishi maisha ya milele
aliwafanya kwa mfano wa hali yake mwenyewe.#2:23 Mwa 1:26-27. Kwa vile binadamu aliumbwa kwa mfano wake Mungu, ni lazima lengo lake la mwisho liwe ni uhai. Rejea 13—15.
24Lakini kwa wivu wa Shetani kifo kiliingia duniani,
na wote walio upande wake hukipata.#2:24 Yule nyoka wa Mwa 3 anachukuliwa kama mfano wa Shetani.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza