Hekima ya Solomoni 3
BHNTLK

Hekima ya Solomoni 3

3
1Lakini watu wanyofu wako mikononi mwa Mungu,
Mateso yoyote hayatawapata kamwe.#3:1 Katika 3:1-9 tunaambiwa majaliwa yatakayowapata watu wema: Kifo chao cha mwili si kifo cha kuishia kwa kuwa hakimaanishi kutengwa mbali na Mungu.
2Kwa wapumbavu walionekana kwamba wamekufa
na kwamba kufariki#3:2 Kufariki: Ni sawa na kuondoka tu (yaani kutoka dunia hii). Rejea Luka 9:31. kwao kulikuwa jambo baya;
3kuondoka kwao kwetu kulidhaniwa kuwa uharibifu,
lakini ukweli ni kwamba wamo katika amani.
4Waonavyo watu ni kwamba wameadhibiwa,
lakini wanalo tumaini thabiti la kutokufa.
5Waliadhibiwa kidogo tu,
lakini sasa watapokea tuzo kubwa;
Mungu aliwajaribu akawapata wanastahili kuishi kwake.#3:5 Tofauti na mawazo yaliyokuwako wakati huo wa kale (rejea Yobu 5:17-27; Zab Meth 13:22), mwandishi anasisitiza kwamba si lazima mtu kupata tuzo hapa hapa duniani kwa mema anayotenda. Mtu mwema huteseka ili apate kuingia katika furaha ijayo. Rejea Sira 2:1-6; Rom 8:18; 2Kor 4:17.
6Aliwajaribu kama dhahabu katika tanuri,
akawapokea kama tambiko ya kuteketezwa.#3:6 Mateso ni majaribu ambayo kwayo Mungu huwatakasa waamini wake. Rejea Kumb 8:2-5; Zab 10; Yak 1:12; 1Pet 1:7.
7Wakati wa kupata tuzo utakapofika, watang'aa,
watameremeta kama vimulimuli katika nyasi kavu.
8Watayahukumu na kuyatawala makabila na mataifa,
naye Bwana atatawala juu yao milele.
9Wote wamwaminio Mungu watatambua ukweli wake;
wote walio waaminifu watakaa kwake kwa upendo,
maana huwajalia neema na huruma watakatifu wake,
na huwaangalia kwa wema hao aliowateua.
10Lakini wabaya wataadhibiwa kadiri ya fikira zao mbovu,
naam, wasiojali mambo ya uadilifu,
wote waliomwasi Bwana.#3:10 Tofauti na furaha ya milele ya watu wema, katika 3:10-12, mwandishi anaeleza adhabu walizowekewa watu waovu.
11Wote wanaodharau hekima au nidhamu wana bahati mbaya;
tumaini lao ni bure,
jasho lao haliwafaidii chochote;
na matendo yao ni ya bure.
12Wake zao huwa wapumbavu na watoto wao wapotovu;
wazawa wao watakuwa katika laana.
Umuhimu wa fadhila
13Heri mwanamke tasa ambaye hana hatia
ambaye hajahusika na muungano ulio dhambi;#3:13 Watoto tangu kale walifikiriwa kuwa ni baraka za Mungu (rejea Zab 127:3-5). Mwandishi anatamka wazi kwamaba kama mtu akiishi maisha adili, kutokuwa na watoto hakutamzuia kupata baraka za Mungu.
huyo atapata tuzo Mungu atakapohukumu roho za watu.#3:13 Hapo kale, kuwa tasa ilikuwa ni jambo la balaa kwa mwanamke (rejea Mwa 30:22-23; Luka 1:24-25). Lakini anayeishi maisha adili, hilo si balaa.
14Heri pia towashi#3:14 Towashi: Yaani watu ambao wamehasiwa (kwa kawaida na watu wengine) walikuwa marufuku kujumuika na jumuiya na hasa katika huduma ya kikuhani (rejea Kumb 23:2; Lawi 21:20). Lakini Isaya (Isa 56:3b-5) anatangaza kwamba na hao pia watashiriki baraka za Mungu. asiyevunja sheria kwa mikono yake,
ambaye hajafikiria maovu dhidi ya Bwana;
huyo atapata upendeleo maalumu kwa uaminifu wake,
na mahali pa furaha kuu katika hekalu la Bwana.
15Maana matunda ya kazi njema ni utukufu;
ni kama mizizi welekevu inayochipua daima.
16Lakini watoto wa wazinzi watakufa kabla ya kukomaa;
naam, wazawa wa wazinzi wataangamia.
17Na hata wakiishi sana hakuna atakayewajali,
na hatimaye uzee wao hautakuwa na heshima.
18Wakifa vijana hawatakuwa na tumaini,
wala hawatapata kitulizo wakati wa hukumu.
19Maana mwisho wa watu wasio waadilifu ni balaa tupu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza