Hekima ya Solomoni 6
BHNTLK

Hekima ya Solomoni 6

6
Jukumu la watawala
1Sikilizeni basi, enyi wafalme, mkaelewe;
jifunzeni, enyi waamuzi popote duniani.#6:1 Vulgata inaanza sura hii na nyongeza: “Kuwa na hekima ni bora kuliko kuwa na nguvu; afadhali kuwa mwenye busara kuliko kuwa shujaa”!
2Tegeni sikio nyinyi mnaotawala watu wengi,
na kujisifia wingi wa mataifa.
3Mamlaka hayo mlipewa na Bwana;
na utawala mliupata kwa Mungu#6:3 Utawala mliupata kwa Mungu: Meth 8:15-16; Rom 13:1. Mkuu.
Atazipima kazi zenu na kuchunguza mipango yenu.
4Maana, kama watumishi katika utawala wake, hamtawali kwa uadilifu,
kama hamshiki sheria,
wala kufuata mwongozo wa Mungu,
5yeye atawajia ghafla na kuwapeni adhabu kali,
maana adhabu kali huwapata aghalabu wenye madaraka.
6Watu wa kawaida wanaweza kusamehewa kutokana na huruma;
lakini wenye madaraka watakabiliwa na uchunguzi mkali.#6:6 Wenye madaraka …uchunguzi mkali: Ukali wa hukumu ya Mungu utategemea wajibu na majukumu aliyonayo mtu.
7Maana Bwana wa wote hamwogopi mtu yeyote,
ukuu wa mtu hauwezi kumfanya apendelee;#6:7 Bwana …ukuu wa mtu hauwezi kumfanya apendelee: Rejea Kumb 10:17; Sira 35:12; Rom 2:11.
Yeye mwenyewe aliwafanya wote, wakubwa na wadogo
na huangalia mahitaji ya wote kwa usawa.
8Lakini wenye madaraka watakabiliwa na uchunguzi mkali.
9Basi, maneno yangu yawahusu nyinyi wafalme,
ili mjifunze kuwa na hekima, msije mkakosa.#6:9 Hekima inayosemwa hapa inahusika hasa na kuendeleza haki na masilahi ya watu, na kwa sababu hiyo ni kitu cha kutafuta kwa upande wa watawala. Taz Sira 10:1.
10Maana wanaozingatia mambo matakatifu
watakubaliwa kuwa watakatifu.
Waliofunzwa hayo watapata humo cha kujitetea hukumuni.
11Basi, muwe na hamu ya mafundisho yangu;
yatamani yawaongoze nanyi mtapata nidhamu.
Thamani ya Hekima
12Hekima huangaza wala hafifii.
Wanaompenda Hekima humwona kwa urahisi,
wanaomtafuta Hekima humpata.
13Hekima hutangulia kujionesha kwa wale wanaomtaka.
14Ukiamka mapema asubuhi kumtafuta, hutataabika;
utamkuta anakungojea mlangoni pake.
15Kumsikiliza Hekima kwa makini ni kupata maarifa kamili.
Ukimtafuta usiku na mchana hutapata masumbuko.
16Hekima daima huwatafuta wale wanaomstahili;
njiani hujidhihirisha kwao kwa upendo,
yu pamoja nao katika kila wazo.
17Mwanzo wa Hekima ni hamu kubwa ya kufunzwa;#6:17 Mwanzo wa Hekima ni hamu kubwa ya kufunzwa: Taz 2Pet 1:5-7 maelezo.
kujali mafundisho ni kumpenda Hekima,
18kumpenda ni kushika sheria zake;#6:18 Kumpenda ni kushika sheria zake: Sira 2:15-16; Yoh 14:15.
kushika sheria zake ni uhakika wa kutokufa.
19na kutokufa kwamleta mtu karibu na Mungu.
20Hivyo hamu ya kumpata Hekima huongoza kwenye ufalme.
21Basi, enyi watawala wa watu,
kama mwafurahia viti vyenu vya enzi
na alama za mamlaka juu ya watu,
mheshimuni Hekima mpate kutawala milele.
Nia ya kuwashirikisha wengine Hekima
22Nitawaambieni Hekima ni nani na chanzo chake.
Sitawaficheni siri yoyote ile;
nitawaambieni historia yake yote tangu mwanzo wake,
na kudhihirisha wazi habari zake
bila kuacha ukweli wowote ule.
23Wivu ule mbaya kamwe hautakuwa mwenzangu,
maana Hekima hapatani na hali ya wivu.
24Wingi wa wenye Hekima ni wokovu kwa ulimwengu,
mfalme mwenye busara ni uthabiti wa watu wake.#6:24 Mfalme mwenye busara ni uthabiti wa watu wake: Meth 11:14. Taz Hek 6:9.
25Kwa hiyo basi, mfunzwe na maneno yangu,
nanyi mtapata faida.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza