11
Kuanguka kwa wenye nguvu#11:1-3 Utenzi huu una ujumbe dhidi ya wachungaji, yaani watu wenye nguvu waliokuwa maadui wa Israeli na ambao wanatajwa kwa mifano: “mierezi ya Lebanoni” na “mialoni ya Bashani” na “pori la mto Yordani” (Zek 10:3; rejea Isa 2:11-13; 10:33-34).
1Fungua milango yako, ewe Lebanoni
ili moto uiteketeze mierezi yako!
2Ombolezeni, enyi misunobari,
kwa kuwa mierezi imeteketea.
Miti hiyo mitukufu imeharibiwa!
Enyi mialoni ya Bashani, ombolezeni,
kwa kuwa msitu mnene umekatwa!
3Sikia maombolezo ya watawala!
Fahari yao imeharibiwa!
Sikia ngurumo za simba!
Pori la mto Yordani limeharibiwa!
Wachungaji wawili#11:4-17 Sehemu hii ni ya namna ya methali kuhusu namna mbili za wachungaji. Ni utenzi mgumu kuufafanua. Mchungaji wa kwanza (4-14) anajitolea kuchunga kondoo hata na kuchukiwa na wenyewe; wa pili (15-17) anaamua kuwaachilia mbali kondoo kwa namna isiyokubalika (aya 15). Kondoo wanawakilisha watu wa Israeli ambao wamekandamizwa na wachungaji wabaya yaani wafalme na watawala wao. Taz aya 1-3 maelezo; na rejea pia Yer 23:1-2; Eze 34:1-10.
4Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, alisema hivi: “Jifanye mchungaji wa kondoo waendao kuchinjwa. 5Wanunuzi#11:5 Wanunuzi: Hawa wanaweza kuwa wanawakilisha watawala wa nchi za nje baada ya ushindi wa Aleksanda Mkuu (taz 9:1-8). Nao wauzaji yamkini ni maofisa wa Wayahudi wanaotumikia wakuu wa nje. wao wanawachinja lakini hawaadhibiwi; na wauzaji wao wanasema, ‘Na ashukuriwe Mwenyezi-Mungu! Sasa tumetajirika’. Hata wachungaji wenyewe hawawaonei huruma. 6Mimi Mwenyezi-Mungu nasema kwamba, sitawahurumia tena wakazi wa dunia. Nitamwacha kila mtu mikononi mwa mwenzake, na kila raia mikononi mwa mfalme wake. Nao wataiangamiza dunia, nami sitamwokoa yeyote mikononi mwao.”
7Basi, nikawa mchungaji wa kondoo waliokuwa wanakwenda kuchinjwa, kwani niliajiriwa na wale waliofanya biashara ya kondoo.#11:7 Wale waliofanya biashara ya kondoo: Tafsiri kulingana na makala moja ya Kale ya Kigiriki. Kiebrania kina, “yaani kondoo maskini”. Nikachukua fimbo mbili: moja nikaiita “Fadhili,” na nyingine nikaiita “Umoja,” nikaenda kuchunga kondoo. 8Kwa muda wa mwezi mmoja, nikaua wachungaji watatu#11:8 Wachungaji watatu: Hawa bila shaka ni watawala wabaya wa kiserikali na kidini ambao hatuwezi kuwajua kwa uhakika. wabaya. Tena uvumilivu wangu kwa kondoo ukaniishia, nao kwa upande wao, wakanichukia. 9Basi, nikawaambia, “Sitakuwa mchungaji wenu tena. Atakayekufa na afe! Atakayeangamia na aangamie! Na wale watakaobaki na watafunane wao kwa wao.” 10Nikaichukua ile fimbo yangu niliyoiita “Fadhili,” nikaivunja, kuonesha kwamba agano alilofanya Mwenyezi-Mungu na watu wake limevunjwa.#11:10 Kitendo cha kuvunja ile fimbo kinamaanisha kwamba Mungu amebatilisha lile agano alilofanya na watu wake na hivyo hatawalinda tena watu wake. Taz Hos 1:9 maelezo. 11Na agano hilo likavunjwa siku hiyohiyo. Wale wafanyabiashara ya kondoo waliokuwa wananiangalia, wakajua kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa ameongea kwa matendo yangu. 12Kisha nikawaambia, “Kama mnaona kuwa ni sawa, nilipeni ujira wangu; lakini kama mnaona sivyo, basi kaeni nao.” Basi, wakanipimia vipande thelathini vya fedha mshahara wangu.#11:12-13 Kwa jinsi inavyosemwa hapa, yaonekana kwamba hivyo vipande thelathini vya fedha ni kitu kidogo ambacho nabii anaweza kuwaachia bila kuathirika. “Vipande thelathini vya fedha” ilikuwa bei ya mtumwa (Kut 21:32). Sehemu ya aya ya 12 imekaririwa katika Mat 26:15, na katika Mat 27:9-10. 13Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Ziweke katika hazina ya hekalu.”#11:13 Ziweke …hekalu: Makala ya Kiebrania: “mpe mfinyanzi”. Mshahara huo ulikuwa ni malipo halali kwa kazi yangu. Hivyo nikachukua hivyo vipande thelathini vya fedha, nikazitia katika hazina ya hekalu la Mwenyezi-Mungu. 14Kisha nikaivunja ile fimbo yangu ya pili niliyoiita “Umoja;” na hivyo nikauvunja umoja kati ya Yuda na Israeli.#11:14 Baadhi ya wafafanuzi wa Maandiko wanaona hapa kitendo kinachoashiria mafarakano kati ya Wayahudi na Wasamaria. Tunajua kutoka historia kwamba Wasamaria walijenga hekalu lao juu ya mlima Gerizimu mnamo mwaka 328 kushindana na hekalu la Yerusalemu. Taz Yoh 4:20 maelezo.
15Mwenyezi-Mungu akaniambia tena, “Jifanye tena mchungaji, lakini safari hii uwe kama mchungaji mbaya!#11:15 Mchungaji mbaya: Nabii anaambiwa ajifanye kuwa mchungaji mbaya bila shaka kumwakilisha mtawala mmoja mbaya ambaye hatuwezi kumtambulisha kwa uhakika. 16Maana nitaleta nchini mchungaji asiyemjali kondoo anayeangamia, au kumtafuta kondoo anayetangatanga, au kumtibu aliyejeruhiwa wala kumlisha aliye hai: bali atakula wale kondoo wanono, hata kwato zao.
17“Ole wake mchungaji mbaya,
ambaye anawaacha kondoo wake!
Upanga na uukate mkono wake,
na jicho lake la kulia na ling'olewe!
Mkono wake na udhoofike,
jicho lake la kulia na lipofuke.”