2
Maono ya tatu: Kamba ya kupimia#2:1-5 Kwa namna ya mfano, maono haya yana shabaha ya kueleza marekebisho ya Yerusalemu ambayo yatafanyika siku za usoni. Rejea Eze 40:2-3; Ufu 11:1; 21:15-17. Katika marekebisho hayo ya Yerusalemu maajabu yale ya wakati wa kutoka Misri yataonekana tena: Mwenyezi-Mungu ataonesha tena utukufu wake na kuwalinda watu wake kama kwa ukuta wa moto (Kut 13:21-22; 40:34; Eze 43:5).
1Katika maono mengine, nilimwona mtu aliyekuwa na kamba ya kupimia mkononi mwake. 2Basi, nikamwuliza, “Unakwenda wapi?” Naye akanijibu, “Ninakwenda kuupima urefu na upana wa mji wa Yerusalemu.”
3Yule malaika aliyezungumza nami akawa anamwendea malaika mwingine ambaye alikuwa anamjia. 4Basi, huyo malaika aliyezungumza nami akamwambia huyo mwenzake, “Kimbia ukamwambie yule kijana kwamba si lazima mji wa Yerusalemu uwe na kuta, la sivyo hapatakuwa na nafasi ya kuwatosha wakazi wake wengi na mifugo itakayokuwa ndani yake. 5Mwenyezi-Mungu asema kuwa yeye mwenyewe atakuwa ukuta wa moto kuulinda mji huo pande zote, naye atakaa humo kwa utukufu wake.”
Waliohamishwa wanaitwa warudi nyumbani#2:6-13 Katika sehemu hii Mungu anawapa moyo watu wake kuondoka Babuloni. Watu wengine wa mataifa nao pia watamwabudu Mungu wa Israeli (2:11).
6Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Haya! Kimbieni kutoka nchi ya kaskazini#2:6 Nchi ya kaskazini: Yaani Babuloni, ambayo iko kaskazini mwa Palestina na ni upande ambao manabii waliutaja kama mahali walipotoka maadui wa Waisraeli (Yer 3:18; 23:8). ambako mimi nilikuwa nimewatawanya kila upande. 7Haraka! Nyinyi nyote mnaokaa katika nchi ya Babuloni, kimbilieni huko mjini Siyoni!” 8Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ambaye kwa utukufu wake amenituma, asema hivi juu ya mataifa yaliyowateka nyara watu wake: “Hakika, anayewagusa nyinyi anagusa mboni ya jicho langu. 9Naam, nitachukua hatua dhidi ya hao waliowatekeni nyara, nao watatekwa nyara na wale waliowafanya watumwa wao.” Hapo ndipo mtakapojua kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi ndiye aliyenituma. 10Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Enyi watu wa Siyoni, imbeni na kufurahi#2:10 Imbeni na kufurahi: 9:9; taz pia Isa 52:9; 54:1; 65:18-19; Sef 3:14. kwa kuwa ninakuja na kukaa kati yenu. 11Mataifa mengi yatajiunga nami Mwenyezi-Mungu, nao watakuwa watu wangu;#2:11 Nao watakuwa watu wangu: Aya 11-12 zina mfululizo wa matamshi ya kale ya kinabii kwa ajili ya kusema juu ya wokovu wa mataifa pote ulimwenguni (taz pia Isa 2:2-4; Mika 4:1-3). nami nitakaa kati yenu.” Mambo hayo yatakapotukia ndipo mtakapojua kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi ndiye aliyenituma kwenu. 12Watu wa Yuda watakuwa tena mali ya pekee ya Mwenyezi-Mungu katika nchi takatifu, na mji wa Yerusalemu utakuwa tena mji wake aliouchagua.
13Enyi wanadamu wote, nyamazeni#2:13 Nyamazeni: Hab 2:20; Sef 1:7; Ufu 8:1. mbele ya Mwenyezi-Mungu, maana, yeye anakuja kutoka makao yake matakatifu.