Zekaria 9
BHNTLK

Zekaria 9

9
Hukumu juu ya mataifa jirani
1Kauli ya Mwenyezi-Mungu:
Mwenyezi-Mungu ametamka siyo tu dhidi ya nchi ya Hadraki
bali pia dhidi ya Damasko.#9:1 Hadraki …Damasko: “Hadraki” ni mji wa Kiaramu kaskazini mwa nchi ya Siria. Nao mji Damasko ulikuwa mji mkuu wa Siria ya kale (Isa 17:1-3; Yer 49:23-27; Amo 1:3-5).
Maana nchi ya Aramu ni mali ya Mwenyezi-Mungu,
kama vile yalivyo makabila yote ya Israeli.#9:1—14:21 Sura 9 mpaka 14 zina mfululizo wa mahubiri ya nabii ambayo mada ni kuwekwa kwa utawala kamili wa Masiha. Tofauti na sehemu iliyotangulia (sura 1 mpaka 8), mahubiri haya ya kinabii hayakufumbwafumbwa. Sura 9—11 zinatangaza kitendo cha Mwenyezi Mungu nyakati za mwisho na ushindi dhidi ya maadui zake; sura 12—14 zinatilia mkazo wokovu na ushindi wa mwisho wa Yerusalemu wakati wa siku ya Mwenyezi-Mungu.
2Hali kadhalika mji wa Hamathi unaopakana na Hadraki;
na hata miji ya Tiro na Sidoni#9:2 Hamathi …Tiro na Sidoni: Watu wa “Hamathi” waliishi kaskazini ya Siria. “Tiro na Sidoni” ni miji ya pwani ya Mediteranea kaskazini mwa Palestina (Isa 23:1-18; Eze 26:1-28:26; Yoe 3:4-8; Amo 1:9-10; Mat 11:21-23; Luka 10:13-14).
ingawaje yajiona kuwa na hekima sana.
3Mji wa Tiro#9:3-4 Tiro: Mji huu wa Foinike ulikuwa umeendelea sana kiuchumi wakati huo na unatumiwa pengine kama kifano cha majivuno na kiburi (Eze 28:11-19). umejijengea ngome kumbwa,
umejirundikia fedha kama vumbi,
na dhahabu kama takataka barabarani.
4Lakini Bwana ataichukua mali yake yote,
utajiri wake atautumbukiza baharini,
na kuuteketeza mji huo kwa moto.
5Mji wa Ashkeloni utaona hayo na kuogopa,
nao mji wa Gaza utagaagaa kwa uchungu;
hata Ekroni, maana tumaini lake litatoweka.
Mji wa Gaza utapoteza mfalme wake,
nao Ashkeloni hautakaliwa na watu.
6Mji wa Ashdodi#9:5-6 Ashkeloni …Gaza … Ekroni … Ashdodi: Hii ilikuwa miji ya muungano wa Wafilisti kwenye mwambao wa bahari ya Mediteranea, kusini mwa Palestina (taz Yos 11:22; 13:3; taz pia Isa 14:29-31; Yer 47:1-7; Eze 25:15-17; Yoe 3:4-8; Amo 1:6-8; Sef 2:4-7). utakaliwa na machotara.
Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Kiburi cha Filistia nitakikomesha.
7Nitawakomesha kula nyama yenye damu,
na chakula ambacho ni chukizo.
Mabaki watakuwa mali yangu,
kama ukoo mmoja katika Yuda.
Watu wa Ekroni watakuwa kama Wayebusi.
8Mimi mwenyewe nitailinda nchi yangu,
nitazuia majeshi yasipitepite humo.
Hakuna mtu atakayewadhulumu tena watu wangu,
maana, kwa macho yangu mwenyewe,
nimeona jinsi walivyoteseka.”
Mfalme wa amani
9Shangilieni sana enyi watu wa Siyoni!
Paazeni sauti, enyi watu wa Yerusalemu!
Tazama, mfalme wenu anawajieni,
anakuja kwa shangwe na ushindi!
Ni mpole, amepanda punda,
mwanapunda, mtoto wa punda.#9:9 Sehemu ya aya hii imekaririwa katika Mat 21:5 na Yoh 12:15 na inasisitiza juu ya unyenyekevu ambao mteule wa Mungu au Masiha alikuwa nao ingawa alikuwa amepewa cheo kikuu cha kifalme. Matumizi ya maneno “amepanda punda, mwanapunda, mtoto wa punda” na sio amepanda farasi au gari la kukokotwa kunatilia mkazo mazingira yake ya amani.
10Atatokomeza magari ya vita nchini Efraimu,
na farasi wa vita kutoka mjini Yerusalemu;
pinde za vita zitavunjiliwa mbali.
Naye ataleta amani miongoni mwa mataifa;
utawala wake utaenea toka bahari hata bahari,
toka mto Eufrate hata miisho ya dunia.#9:10 Utawala huo mpya utakaoongozwa na huyo mteule wa Mungu (au Masiha) sio tu kwamba utakuwa wa amani (aya ya 9) bali pia utauafiki ulimwengu wote (rejea Zab 46:8-10; 72:7-8; Isa 2:1-5; 11:6-9; Hos 2:18; Mika 4:1-4. Taz pia Efe 2:14-18).
Kurudishwa kwa watu wa Mungu
11Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Kwa sababu ya agano langu nanyi,
agano lililothibitishwa kwa damu,
nitawakomboa wafungwa wenu
walio kama wamefungwa katika shimo tupu.
12Enyi wafungwa wenye tumaini;
rudini kwenye ngome yenu.
Sasa mimi ninawatangazieni:
nitawarudishieni mema maradufu.
13Yuda nitamtumia kama uta wangu;
Efraimu nimemfanya mshale wangu.
Ee Siyoni! Watu wako nitawatumia kama upanga
kuwashambulia watu wa Ugiriki;
watakuwa kama upanga wa shujaa.”
14Mwenyezi-Mungu atawatokea watu wake;
atafyatua mishale yake kama umeme.
Bwana Mwenyezi-Mungu atapiga tarumbeta;
atafika pamoja na kimbunga cha kusini.
15Mwenyezi-Mungu wa majeshi atawalinda watu wake,
nao watawaangamiza maadui zao.
Watapiga kelele vitani kama walevi
wataimwaga damu ya maadui zao.
Itatiririka kama damu ya tambiko
iliyomiminwa madhabahuni kutoka bakulini.#9:15 Maana ya aya hii katika Kiebrania si dhahiri.
16Wakati huo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, atawaokoa,
maana wao ni kundi lake;
nao watang'aa katika nchi yake
kama mawe ya thamani katika taji.
17Jinsi gani uzuri na urembo wake ulivyo!
Wavulana na wasichana watanawiri
kwa wingi wa nafaka na divai mpya.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993

The Bible Society of Kenya 1993

Learn More About Biblia Habari Njema: Toleo la Kujifunza