1
1Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Sefania mwana wa Kushi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amenia, mwana wa Hezekia,#1:1 Sefania …mwana wa Hezekia: Nasaba ya nabii Sefania ni ndefu kuliko nasaba nyingine za manabii. Kutaja ukoo wake hadi kizazi cha 4 aghalabu kunaonesha kwamba yeye alikuwa mtu maarufu. Jina la babu yake “Kushi” ni jina pia la nchi kwenye eneo la Afrika kaskazini ambapo sasa ni nchi za Misri Ethiopia, Eritrea na Sudani. wakati wa utawala wa mfalme Yosia mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda:
2Mwenyezi-Mungu asema:
“Nitavifagilia mbali viumbe vyote duniani:#1:2-23 Aya hizi ambazo zimeandikwa kishairi zahusu siku ya Mwenyezi-Mungu, jambo ambalo ni ujumbe mkuu wa nabii Sefania. Katika siku hiyo ambayo hapa inaelezwa kama siku kubwa ya tambiko (aya 7) Mungu atahukumu dunia yote (aya 2-3), ataangamiza ibada kwa miungu ya uongo (aya 4-7) na kuwaadhibu viongozi wa watu (aya 8-9), wafanyabiashara wabaya (aya 10-11) na wale wasiojali juu ya Mungu (aya 12). Taz Amo 5:18-20 maelezo.
3wanadamu, wanyama, ndege wa angani
na samaki wa baharini;
vyote nitaviangamiza.
Waovu#1:3 Waovu: Kiebrania: “wanaokwaza”. nitawaangamiza kabisa;
wanadamu nitawafagilia mbali duniani.
4Nitaunyosha mkono wangu#1:4 Nitaunyosha mkono wangu: Huu ni msemo unaotumika mara kwa mara katika Biblia kwa maana ya “nitaadhibu” (taz Isa 5:25; 23:11; Yer 6:12; 15:6; Eze 6:14; 14;9,13). dhidi ya nchi ya Yuda,
kadhalika na wakazi wote wa mji wa Yerusalemu.
Nitaangamiza mabaki yote ya Baali kutoka nchi hii,
na hakuna atakayetambua jina lao.
5Nitawaangamiza wote wanaosujudu juu ya paa,
wakiabudu jeshi la mbinguni.#1:5 Wanaosujudu …wakiabudu jeshi la mbinguni: Kisa cha namna hii kinapatikana pia katika Yer 8:2. “Jeshi la mbinguni” ni nyota na sayari angani.
Nitawaangamiza wale wanaoniabudu
na kuapa kwa jina langu,
hali wanaapa pia kwa jina la mungu Milkomu.#1:5 Milkomu: Huyo alikuwa mungu wa kitaifa katika nchi ya Waamoni (2Fal 23:13; Yer 49:1, 3). Kuapa kwa jina la mungu huyo ni kumtambua kuwa mungu (Kut 20:3-6).
6Nitawaangamiza wote walioniacha mimi Mwenyezi-Mungu
wote walioacha kunitafuta na kuniuliza shauri.”
7Nyamazeni mbele ya Bwana Mwenyezi-Mungu,#1:7 Nyamazeni …Mwenyezi-Mungu: Rejea Hab 2:20; Zek 2:13.
kwani siku ya Mwenyezi-Mungu iko karibu.
Mwenyezi-Mungu ameandaa tambiko,#1:7 Mwenyezi-Mungu ameandaa tambiko: Rejea Isa 34:6; Eze 39:17-18, na taz Yer 46:10 maelezo, ambapo pia inaelezwa hukumu ya Mungu pamoja na picha ya tambiko kubwa.
nao aliowaalika amewateua.
8Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Katika siku ile ya karamu yangu,
nitawaadhibu viongozi wa watu hao,
kadhalika na wana wa mfalme
pamoja na wote wanaoiga desturi za kigeni.
9Siku hiyo nitawaadhibu wote:
wanaoruka kizingiti cha nyumba#1:9 Wanaoruka kizingiti cha nyumba: Maneno haya yanataja vitendo vinavyofanana na kile kinachotajwa pia katika 1Sam 5:5. Huenda kitendo hicho kilikuwa namna ya ibada kwa miungu ya uongo kwenye malango au vizingiti vyao. kama wapagani,
wanaojaza nyumba ya bwana wao#1:9 Nyumba ya bwana wao: Au: hekalu la mungu wao. vitu vya dhuluma na wizi.
10“Siku hiyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu,
Kutasikika kilio kutoka Lango la Samaki,#1:10 Lango la Samaki: Mojawapo ya malango ya kuingia upande wa kaskazini mwa Yerusalemu (Neh 3:3; 12:39); liliitwa hivyo kwa sababu huko kulikuwa na soko ambako waliuza samaki (rejea Neh 13:16).
maombolezo kutoka Mtaa wa Pili,
na mlio mkubwa kutoka milimani.
11Lieni enyi wakazi wa Makteshi!#1:11 Makteshi: Eneo kusini mwa Yerusalemu lakini haijulikani hasa ni wapi.
Wafanyabiashara wote#1:11 Wafanyabiashara wote: Neno kwa neno katika makala ya Kiebrania ni “watu wote wa Kanaani”. Taz Hos 12:7. wameangamia,
wote wapimao fedha wamefutiliwa mbali.
12Wakati huo nitaupekua mji wa Yerusalemu kwa taa,#1:12 Nitaupekua mji wa Yerusalemu kwa taa: Baadhi ya wafafanuzi wa Maandiko Matakatifu wanafikiri kwamba nabii Sefania alipotamka ujumbe huu alifanya hivyo akiwa na taa mkononi.
nitawaadhibu wanaoishi wametulia kama machicha ya divai,
wote ambao husema mioyoni mwao:
‘Mwenyezi-Mungu hatafanya kitu: chema au kibaya.’#1:12 Mwenyezi-Mungu hatafanya kitu: chema au kibaya: Rejea Zab 10:4; 14:1; Isa 29:15; Yer 5:12; Amo 9:10; Mal 3:14-15. Hizo ni fikira za watu ambao nabii anawaona kwamba hawaamini kuwa Mungu huingilia mambo ya duniani humu, yaani watu wanaompuuza Mungu.
13Utajiri wao utanyakuliwa,
na nyumba zao zitaachwa tupu!
Watajijengea nyumba, lakini hawataishi humo.
Watapanda mizabibu, lakini hawatakunywa divai yake.”#1:13 Watapanda mizabibu, lakini hawatakunywa divai yake: Rejea Kumb 28:30; Amo 5:11; Mika 6:15.
14Ile siku kubwa ya Mwenyezi-Mungu#1:14-18 Siku kubwa ya Mwenyezi-Mungu: Isa 13:6; Eze 30:2-3; Yoe 1:15. imekaribia,
iko karibu na inakuja mbio.
Mlio wa siku ya Mwenyezi-Mungu ni wa uchungu;
hapo, shujaa atalia kwa sauti.
15Siku hiyo itakuwa siku ya ghadhabu,
ni siku ya dhiki na uchungu,
siku ya giza na huzuni;
siku ya uharibifu na maangamizi,
siku ya mawingu na giza nene.#1:15 Siku ya ghadhabu …siku ya giza … nene: Hiyo ni picha au mfano unaotumika katika maandishi ya manabii na yale yanayosimulia matukio ya mwisho wa nyakati (maandishi ya Kiapokalipti) kuhusu siku ya Mwenyezi-Mungu. Rejea Yoe 2:2; Amo 5:18,20.
16Siku hiyo ni ya mlio wa tarumbeta ya vita,
dhidi ya miji yenye ngome na kuta ndefu.
17Kwa kuwa watu wamemkosea Mwenyezi-Mungu,
yeye atawaletea dhiki kubwa,
hivyo kwamba watatembea kama vipofu.
Damu yao itamwagwa kama vumbi,
na miili yao kama mavi.
18Fedha yao wala dhahabu yao havitaweza kuwaokoa
katika siku hiyo ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu.
Kwa moto wa wivu wake
dunia yote itateketezwa.
Kwa ukamilifu na kwa namna ya kutisha
atawafanya wakazi wote duniani watoweke.