2 Wathesalonike 2
TKU

2 Wathesalonike 2

2
Mambo Maovu Yatatokea
1Kaka na dada, tuna jambo la kuwaambia juu ya kuja kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Tunataka kuzungumza nanyi juu ya wakati huo tutakapokusanyika pamoja naye. 2Msikubali kufadhaishwa na kutiwa kuhofu ikiwa mtasikia kwamba siku ya Bwana tayari imekwishawadia. Wengine wanaweza kusema kwamba wazo hili limetoka kwetu katika jambo alilotuambia Roho, au tulilosema, au katika barua tuliyoiandika. 3Msidanganywe na chochote wanachoweza kusema kuhusu kuja kwa Bwana. Siku hiyo ya Bwana haitakuja mpaka itanguliwe na kukengeuka kwa wanadamu na kumwacha Mungu. Na siku hiyo haitakuja mpaka ajitokeze kwanza Mtu wa Uovu, yule ambaye ana uhakika kuwa ataangamizwa.#2:3 ataangamizwa Au “Kusababisha uharibifu”. Kwa maana ya kawaida, “ni mwana wa uharibifu”. 4Huyo atasimama kinyume na kujiweka mwenyewe juu ya kila kitu ambacho watu wanaabudu au kudhani kuwa kinafaa kuabudiwa. Ataenda na kuingia ndani ya Hekalu#2:4 Hekalu Pengine Hekalu katika Yerusalemu. Tazama Hekalu katika Orodha ya Maneno. na kukikalia kiti cha enzi, akidai kuwa yeye ni Mungu.
5Niliwaambia zaidi ya mara moja nilipokuwa huko kwamba mambo yote haya yangetokea. Je, mnakumbuka? 6Na mnafahamu kinachomzuia Mtu wa Uovu. Huyo hataruhusiwa kuonekana mpaka wakati sahihi utakapofika. 7Tayari nguvu ya uovu inatenda kazi ulimwenguni sasa. Lakini yupo mmoja anayeizuia nguvu hiyo. Na ataendelea kuizuia mpaka atakapoondolewa. 8Kisha huyo Mtu wa Uovu atatokea. Lakini Bwana Yesu atamuua kwa pumzi inayotoka katika kinywa chake. Bwana atakuja katika namna ambayo kila mtu atamwona, na huo utakuwa mwisho wa Mtu wa Uovu.
9Kuja kwa Mtu wa Uovu itakuwa kazi ya Shetani. Atakuja na nguvu kuu, na atafanya aina zote za miujiza ya uongo, ishara, na maajabu. 10Mtu wa Uovu atatumia kila aina ya uovu kuwatia ujinga wote walio njiani kuelekea kuangamia. Wamepotea kwa sababu walikataa kuupenda ujumbe wenye ukweli kuhusu Yesu na kuokolewa. 11Hivyo Mungu atawaacha wadanganyike hata kuamini uongo.#2:11 uongo Ina maana ya kuamini uongo (mkubwa) juu ya Muasi (ya kwamba Muasi ndiye Mungu). 12Wote watahukumiwa kwa sababu hawakuamini ujumbe wa kweli na kwa kuwa walifurahia kufanya maovu.
Mmechaguliwa kwa ajili ya Wokovu
13Ndugu zangu, ninyi ni watu mnaopendwa na Bwana. Na imetupasa tumshukuru Mungu daima kwa sababu yenu. Hayo ndiyo tunayotakiwa kuyatenda, kwa sababu Mungu aliwaita kuwa miongoni mwa watu#2:13 kuwa … watu Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza, “kuanzia mwanzo”. wa kwanza kuokolewa. Mmeokolewa na Roho aliyewafanya muwe watu wa Mungu walio watakatifu kupitia kuiamini kweli. 14Mungu aliwaita ninyi mpate wokovu. Aliwaita kwa kutumia Habari Njema tuliwahubiri. Mliitwa ili mshiriki katika utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo. 15Hivyo simameni imara na kuendelea kuamini mafundisho tuliyowapa tulipokuwa huko na kupitia barua yetu.
16-17Tunaomba kwamba Bwana Yesu Kristo na Mungu Baba yetu awafariji na kuwaimairisha katika kila jambo jema mnalotenda na kusema. Mungu alitupenda na kutupa kupitia neema matumaini ya ajabu na faraja isiyo na mwisho.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi

Toleo la Awali

© 2017 Bible League International

Learn More About Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi