Ufunuo 2
TKU

Ufunuo 2

2
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Efeso
1“Andika hivi kwa malaika#2:1 malaika Ama mwakilishi wa kanisa. Pia katika mstari wa 8,12 na 18 na pia katika barua zinazofuata Sura 3:1,7 na 14. wa kanisa lililoko Efeso:
Huu ni ujumbe kutoka kwake yeye anayeshikilia nyota saba katika mkono wake wa kulia na kutembea katikati ya vinara vya taa saba vya dhahabu.
2Ninayajua matendo yako, unavyofanya kazi kwa bidii na usivyokata tamaa. Ninajua kwamba huwakubali watu waovu. Umewajaribu wote wanaojiita mitume lakini si mitume. Umegundua kuwa ni waongo. 3Huachi kujaribu. Umestahimili taabu kwa ajili ya jina langu na hujakata tamaa.
4Lakini nina neno hili nawe umeuacha upendo uliokuwa nao hapo mwanzo. 5Hivyo kumbuka ulipokuwa kabla ya kuanguka. Ugeuze moyo wako na utende yale uliyoyatenda mwanzoni. Usipobadilika, nitakuja kwako na kutoa kinara chako cha taa mahali pake. 6Lakini unafanya vizuri kuyachukia matendo ya Wanikolai.#2:6 Wanikolai Kikundi cha kidini kilichofuata mafundisho ya uongo. Pia katika mstari wa 15. Mimi pia nayachukia mambo wanayotenda.
7Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa. Wale watakaoshinda, nitawapa haki ya kula matunda kutoka kwenye mti wa uzima, ulio katika Bustani ya Mungu.
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Smirna
8Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna:
“Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye wa Kwanza na wa Mwisho, aliyekufa na akawa hai tena.
9Ninayajua matatizo yako, na ninajua kwamba wewe ni maskini, lakini hakika wewe ni tajiri! Ninayajua matusi unayoteseka kutoka kwa watu wanaojiita Wateule wa Mungu.#2:9 Wateule wa Mungu Kwa maana ya kawaida, “Wayahudi”. Pia katika 3:9. Lakini si Wayahudi halisi. Watu hao ni wa kundi#2:9 kundi Kwa maana ya kawaida, “sinagogi”. Pia katika 3:9. la Shetani. 10Usiogope mambo yatakayokupata hivi karibuni. Ninakwambia, Ibilisi atawafunga gerezani baadhi yenu ili kuipima imani yenu. Mtateseka kwa siku kumi, lakini iweni waaminifu, hata ikiwa mtatakiwa kufa. Mkiendelea kuwa waaminifu, nitawapa thawabu#2:10 thawabu Kwa maana ya kawaida, “taji”, ni shada la majani au matawi ya miti lililowekwa juu ya vichwa vya washindi wa riadha ili kuwaheshimu. Ni alama inayoonyesha ushindi na zawadi. ya uzima wa milele.
11Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa. Wale watakaoshinda hawatadhuriwa na mauti ya pili.
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Pergamo
12Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Pergamo:
Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye na upanga wenye makali kuwili unaotoka katika kinywa chake.
13Ninapafahamu mahali unapoishi. Unaishi mahali kilipo kiti cha enzi cha Shetani, lakini wewe ni mwaminifu kwangu. Hukukataa kueleza kuhusu imani yako kwangu hata wakati wa Antipa. Antipa alikuwa shahidi wangu mwaminifu#2:13 shahidi wangu mwaminifu Mtu anayehubiri ujumbe wa Mungu kwa uaminifu, hata nyakati za hatari. aliyeuawa katika mji wako, mji ambao shetani anaishi.
14Lakini nina vitu vichache kinyume nawe. Una watu huko wanaofuata mafundisho ya Balaamu. Balaamu alimfundisha Balaki namna ya kuwafanya watu wa Israeli kutenda dhambi. Walitenda dhambi kwa kula vyakula vilivyotolewa kwa ajili ya sanamu na kwa kufanya uzinzi. 15Ndivyo ilivyo hata kwa kundi lako. Una watu wanaofuata mafundisho ya Wanikolai. 16Hivyo igeuzeni mioyo yenu! Msipobadilika, nitakuja kwenu haraka na kupigana kinyume na watu hawa kwa kutumia upanga unaotoka katika kinywa changu.
17Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa!
Kila atakayeshinda nitampa mana iliyofichwa. Pia nitampa kila mshindi jiwe jeupe lililoandikwa jina jipya juu yake. Na hakuna atakayejua jina hili isipokuwa yule atakayepata jiwe hili.
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Thiatira
18Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira:
Huu ni ujumbe kutoka kwa Mwana wa Mungu, aliye na macho yanayong'aa kama moto na miguu kama shaba inayong'aa.
19Ninayajua matendo yako. Ninajua kuhusu upendo wako, imani yako, huduma yako na uvumilivu wako. Ninajua kwamba unafanya zaidi sasa kuliko ulivyofanya kwanza. 20Lakini ninalo hili kinyume nawe: Umemruhusu yule mwanamke Yezebeli afanye anachotaka. Anasema kwamba yeye ni nabii,#2:20 nabii Yezebeli alikuwa nabii mwongo. Alidai kuwa anazungumza kwa niaba ya Mungu, lakini hakuisema kweli ya Mungu. lakini anawapotosha watu wangu kwa mafundisho yake. Yezebeli huwaongoza watu wangu kutenda dhambi ya uzinzi na kula vyakula vilivyotolewa kwa sanamu. 21Nimempa muda ili aubadili moyo wake na kuiacha dhambi yake, lakini hataki kubadilika.
22Hivyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso. Na wale wote wanaozini naye watateseka sana. Nitafanya hivi sasa ikiwa hawataacha mambo anayofanya. 23Pia, nitawaua wafuasi wake. Ndipo makanisa yote wataona kuwa mimi ndiye ninayefahamu kile ambacho watu wanadhani na kufikiri. Na nitamlipa kila mmoja wenu kutokana na kile alichotenda.
24Lakini ninyi wengine mlioko Thiatira ambao hamjafuata mafundisho yake. Hamjajifunza mambo yanayoitwa ‘Siri za ndani za Shetani.’ Hivi ndivyo ninawaambia: Sitawatwika mzigo wowote. 25Shikeni katika kweli mliyo nayo tu mpaka nitakapo kuja.
26Nitawapa nguvu juu ya mataifa wale wote watakaoshinda na wakaendelea kutenda yale ninayotaka mpaka mwisho. 27Watayatawala mataifa kwa fimbo ya chuma. Watayavunja vipande vipande kama vyombo vya udongo wa mfinyanzi.#2:26-27 Mistari hii inafanana na Zab 2:8-9 (tafsiri ya Kiyunani). 28Watakuwa na nguvu ile ile niliyoipokea kutoka kwa Baba yangu, na nitawapa nyota ya asubuhi. 29Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi

Toleo la Awali

© 2017 Bible League International

Learn More About Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi