Utangulizi
Paulo alikuwa ameanzisha kanisa katika mji wa Ugiriki wa Korintho katika safari yake ya pili ya kueneza Injili (Matendo 18:1-8), lakini mambo yalikuwa yameharibika sana baada ya kuondoka kwake. Alihisi ilikuwa muhimu kuwaandikia kuhusu matatizo mengi yaliyokuwa yamejitokeza.
Walikuwa na matatizo mbalimbali, baadhi yao yakiwa kama: walipinga utume wake; walitumia vibaya Meza ya Bwana; walijiuliza kuhusu kula nyama iliyokuwa imetolewa dhabihu kwa sanamu; walishtakiana wenyewe mahakamani; waliruhusu uasherati; walikana ufufuo; walibishana kuhusu ndoa. Paulo alihisi kwamba lazima angekabiliana na hali hiyo, la sivyo mambo kule Korintho yangevurugika. Wakati Paulo anashughulikia kwa utaratibu matatizo haya, anagusia misingi ya mafundisho muhimu katika Imani.
Wazo Kuu
Sababu kuu ya Paulo kuandika waraka huu ilikuwa kurekebisha dhuluma zilizokuwa wazi katika kanisa la Korintho, akionyesha umuhimu wa jinsi tunavyoishi. Haitoshi kusema sisi ni Wakristo, lakini pia lazima matendo yetu yaambatane na Ukristo. Kutofanya hivyo ni kukosea heshima jina la Al-Masihi. Paulo pia anasisitiza kutosheleka kikamilifu kwake Al-Masihi kwa muumini. Katika Al-Masihi tunafanyika safi, watakatifu na wa kukubalika mbele za Mwenyezi Mungu (1:30).
Mwandishi
Mtume Paulo.
Mahali
Efeso.
Tarehe
56 B.K.
Mgawanyo
• Salamu za Paulo (1:1-9)
• Tatizo la migawanyiko kanisani (1:10–4:21)
• Tatizo la kujamiiana kwa maharimu (5:1-13)
• Tatizo la kushtakiana mahakamani (6:1-11)
• Tatizo la uasherati (6:12-20)
• Matatizo yanayohusiana na ndoa (7:1-40)
• Matatizo kuhusu ibada za sanamu (8:1–11:1)
• Matatizo katika kuabudu (11:2–14:40)
• Matatizo kuhusu ufufuo wa wafu (15:1-58)
• Hitimisho (16:1-24).