Utangulizi
Mtume Petro aliandika barua hii karibu na siku za mwisho za maisha yake, kwa kusudi la kuwafariji na kuwatia moyo Wayahudi Wakristo waliokuwa wakiishi Asia Ndogo. Anasema kwamba kuteseka ni sehemu ya maisha ya Ukristo, na kwamba Mwenyezi Mungu amewawekea zawadi isiyoharibika wale wanaomtumainia. Kama kuna yeyote aliyekuwa akitafakari kuirudi dini ya Kiyahudi ili kuepuka mateso, Petro anasema kwamba kanisa sasa ndilo taifa teule na ukuhani wa Mwenyezi Mungu (2:9). Kwa hivyo wazo lolote la kurudi dini ya Kiyahudi lilikuwa halina maana. Kisha Petro anatoa mfano wa Al-Masihi ambaye aliteseka, na anawatahadharisha Wakristo kujiandaa kwa mateso kama hayo. Maagizo kwa vikundi kadhaa vya Kikristo yanafikisha kikomo kitabu hiki.
Wazo Kuu
Somo kuu la 1 Petro ni ushindi kupitia mateso. Wakristo wa hapo mwanzo waliishi maisha magumu, mara nyingi wakilipa gharama ya imani yao kupitia maisha yao. Lakini barua hii inatuonyesha kwamba jambo hili ni la thamani, haijalishi gharama ni ipi. Mwenyezi Mungu anajua yote yanayotokea, na katika mpango wake wa milele atayafanya yote kwa wema wetu. Twapaswa kuweka tumaini letu kwake, huku macho yetu yakiwa yameangalia juu mbinguni, tukifahamu makao yetu ni huko, sio hapa duniani.
Mwandishi
Mtume Petro.
Mahali
Hapajulikani, huenda ni Rumi.
Tarehe
Kama 63 au 64 B.K.
Mgawanyo
• Utukufu wa wokovu kutoka kwa Al-Masihi (1:1-25)
• Utiifu wa Mkristo (2:1-10)
• Kuteseka, na mfano wa Al-Masihi (2:11-25)
• Jinsi ya kuishi kama Mkristo nyumbani na duniani (3:1-17)
• Mateso, na mfano wa Al-Masihi (3:18–4:19)
• Huduma ya Kikristo, na maneno ya mwisho (5:1-14).