Utangulizi
Vitabu vya 1 na 2 Samweli vilikuwa kitabu kimoja katika Biblia ya Kiebrania. Hii ni kwa sababu vinatengeneza historia ya moja kwa moja kuhusu maisha ya Samweli, Sauli na Daudi. Vilitenganishwa kuwa vitabu viwili kwa urahisi wa kusoma. Kitabu cha 1 Samweli kinahusu vita na Wafilisti, na mwishowe Sauli kushindwa kukabiliana na adui. Kitabu kinaanza kwa Israeli kukandamizwa na Wafilisti (taifa jirani wapenda vita) na kuchipuka kwa viongozi wawili wa zamani, yaani Samweli na Sauli. Samweli alikuwa kiongozi wa kidini, na mwishowe Sauli akawa mfalme. Ushindi wa mwanzo wa Sauli unaelezewa ukifuatia na kuanguka kwa maadili yake, na mwisho wake wa kuhuzunisha. Kusawazisha kuanguka kwa Sauli ni kuinuka kwa Daudi, kijana ambaye atachukua uongozi baada ya kifo cha Sauli.
Wazo Kuu
Kiini cha ujumbe unaoenea katika kitabu hiki ni kwamba Mwenyezi Mungu hawapi watu wake kinga dhidi ya mabadiliko katika maisha ya mwanadamu, ila anawapa neema ya kupambana na mambo hadi mwisho wa kuridhisha. Kuinuka na kuanguka kwa wafalme, wakati wa amani na vita; nyakati zote Mwenyezi Mungu habadiliki, na anatawala matukio ya wanadamu kwa njia ambayo wale wanaomtumaini wanapata faraja na ujasiri wa kuvumilia.
Mwandishi
Hajulikani.
Tarehe
Pengine karne ya 10 KK.
Mgawanyo
• Huduma ya mwanzo ya Samweli, na vita vya Wafilisti (1:1–7:17)
• Mafanikio ya mwanzo ya Mfalme Sauli (8:1–15:35)
• Kushuka kwa Sauli, na kupanda kwa Daudi (16:1–20:42)
• Sauli amtesa Daudi (21:1–24:22)
• Kukua kwa nguvu za Daudi, na kifo cha Sauli (25:1–31:13).