1 Wathesalonike Utangulizi
NMM

1 Wathesalonike Utangulizi

Utangulizi
Katika safari ya kwanza ya kueneza Injili ya Paulo, alitembelea Thesalonike ila ilimlazimu kutoroka kwa sababu ya upinzani mkubwa uliozuka kule (Matendo 17:1-9). Baada ya kwenda Athene na mwishowe kufika Korintho, Paulo alipata habari kutoka kwa Timotheo, ambaye alikuwa amemtuma kuulizia kuhusu Wathesalonike. Ingawa walikuwa wamepitia mateso, walikuwa wamesimama imara katika imani. Paulo aliandika waraka huu kuwafariji na kuwatia moyo waumini hao wachanga katika Al-Masihi. Aliwaandikia pia kudhibitisha imani yao katika mafundisho ya kimsingi ya kanisa kuhusu Mwenyezi Mungu, Roho Mtakatifu, Al-Masihi, maisha ya Ukristo, lakini hasa kuhusu Al-Masihi kuja mara ya pili. Yamkini waumini hawa walikuwa na wasiwasi kwamba Wakristo wenzao waliokuwa wamekufa hawangeweza kuufikia ufufuo wa wafu. Hivyo Paulo akawaandikia kuwahakikishia kwamba waliokufa wakiwa wanamwamini Al-Masihi watafufuka kwanza (4:16).
Wazo Kuu
Paulo anawafariji waumini wanaoteswa na kuwahakikishia kwamba Mwenyezi Mungu yu pamoja nao na ameahidi ushindi. Ushindi wa mwisho utakuwa wakati Al-Masihi atarudi, wakati Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni na kutukusanya sisi kwake ili tuwe naye milele (4:17). Tukifahamu haya, tunastahili kustahimili katika mateso na kuishi maisha ya kumcha Mwenyezi Mungu na yasiyo na lawama.
Mwandishi
Mtume Paulo.
Mahali
Korintho.
Tarehe
Mwaka wa 50 au 51 B.K.
Mgawanyo
• Shukrani za dhati za Paulo kwa Wathesalonike (1:1-10)
• Utetezi binafsi wa Paulo (2:1-16)
• Maelezo ya matukio tangu kuondoka Thesalonike (2:7–3:13)
• Kuwasihi kuishi maisha ya kumcha Mungu (4:1-12)
• Al-Masihi kuja mara ya pili (4:13–5:11)
• Maagizo ya mwisho (5:12-28).

Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu)

Copyright © 2018 by Biblica, Inc.®

All Rights Reserved Worldwide.

Learn More About Neno: Maandiko Matakatifu